Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Lakini awali ya yote kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaendelea kuifanya katika Taifa hili kwenye sekta hii na sekta nyingine zote. Dunia inajua, Afrika inatambua na Watanzania tunajua hilo, kwamba Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nichukue fursa hii vile vile kumpongeza Mheshimiwa Waziri, yeye pamoja na Naibu Mawaziri wake waendelee kuwa wanyenyekevu hivi hivi na mabega yao yaendelee kuwa chini. Tunashukuru sana kwa ushirikiano mzuri ambao mnaendelea kuutoa kwa Wabunge wote ambao tuko ndani humu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila, nimpongeze sana Mkurugenzi Mtendaji wa TASAC kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Tunahitaji vijana wa namna hii wenye uwezo mkubwa wa kuweza kuleta mawazo yaliyo chanya katika kuweza kuibadilisha nchi hii. Lakini vilevile nimpongeze Mkurugenzi wa TPA, anafanya kazi nzuri sana yeye pamoja na wasaidizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa jimboni tunakimbiza Mwenge wa Uhuru. Wakati nikiwa jimboni tulifika katika kata moja inaitwa Kata ya Mahege. Pale watu wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa walikuwa wanapata chakula, lakini nilikuta pale mkutano nimeandaliwa akiwepo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, mzee wangu alikuwepo pale pamoja na Katibu Mzee wangu Mketo walikuwa wako pale, na wananchi wamejumuika kwa pamoja. Lengo la mkutano ule walimuhitaji Mwenyekiti wa Chama, Mbunge pamoja na Katibu.

Mimi niseme tu nimshumuru sana Mwenyekiti wangu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya, Comrade Juma Kassim Ndaluke kwa hekima kubwa aliyo nayo yeye pamoja na Katibu wangu Zacharia na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alikuwepo pale. Lengo kubwa la mkutano ule wananchi wale walikuwenda kuniuliza swali moja; hivi Mbunge, kuongea unaongea hivi hata unashindwa kuruka sarakasi na wewe upate barabara hii ya Bungu – Nyamisati? Mbona wenzio wanaruka sarakasi wanafanikiwa wewe una shida gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu, nimshukuru sana Mwenyekiti wangu wa Chama Wilaya alitumia hekima kukimaliza kikao kile kwa muda mfupi sana. Aliwaambia wananchi wale pamoja na Katibu wa Chama na Mwenyekiti wake, kwamba yeye ndiye msimamizi wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kibiti. Kwa tafsiri hiyo aliniagiza kwamba Mbunge umekimbiza mwenge leo, lakini nakusamehe usikae kwenye mkesha huu nakuomba nenda Bungeni, tunajua kuna bajeti inaendelea kule ya Wizara hii, kwa hiyo, nenda kalisemee hili kwa msisitizo wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri, Bungu – Nyamisati kimekuwa ni kilio cha muda mrefu sana. Sawa mimi utaalamu wa kuruka sarakasi sina basi hata haya ninayozungumza Profesa Mbarawa huyaelewi? Sasa nizungumze lugha gani ili niweze kueleweka? Maana nikizungumza Kindengereko huwezi kufahamu, mimi siwezi kuruka sarakasi, ninachoweza kufanya nicheze ngoma ya kwetu kinyafumbili labda unaweza ukanielewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shida kubwa sana katika barabara ile, kuna vifo vinatokea. Nataka niseme tu Mbunge mwenzangu wa Jimbo la Mafia ambaye ni Waziri vilevile, juzi saa 10.00 usiku alinipigia simu akiniambia Mpembenwe kuna shida katika ile barabara, kuna lori limekaa vibaya pale, kwa hiyo, wananchi wanapata tabu na mvua ilikuwa inanyesha. Haya ni matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu lichukuliwe jambo hili on a serious note. Wananchi wa Jimbo la Kibiti tunahitaji barabara hii, kwa sababu hizi habari za upembuzi yakinifu, usanifu wa kina tumechoka. Wazee wale watakwenda kunihukumu. Yuko pale ndugu yangu Mketo, Katibu wa chama, ni mkorofi kweli kweli, lakini wananchi wa pale nao ni shida moja kwa moja. Mimi pamoja na wananchi wangu tunaomba tusaidiwe katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, naomba nizungumze jambo moja la msingi katika Wizara hii na huu utakuwa ni mchango wangu mmoja tu. Naomba nizungumze kuhusiana na suala zima la Bandari yetu ya hapa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singapore ilipata uhuru mwaka 1965, lakini katika miaka 50 ya nyuma ambayo imepita capital income ya Singapore ilikuwa chini ya dola 324. Mwaka 1975 Singapore per capita income ikawa imebadilika, tunazungumzia dola 60,000 nendeni mkaangalie kule mtapata taarifa hizo. Nini maana yake? Maana yake ni kwamba strategically wameweza kuitumia bandari vizuri ili kuhakikisha kwamba inakwenda kuchangia vizuri kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana, Mheshimiwa Rais amezungumza katika nyakati tofauti katika hafla tofauti za Kiserikali akiwa anaonesha hisia zake za hali ya juu za kutoridhishwa kwake na jinsi gani performance ya bandari yetu inavyoshindwa kuchangia ipasavyo katika pato letu la Taifa. Niombe, sheria tumezitunga sisi wenyewe hapa na sisi wenyewe ndio tumezipitisha sheria hizi, hivi suala hili la PPP lina shida gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemfuatilia vizuri sana Mheshimiwa Profesa Mbarawa katika hotuba yake, wametenga hela bilioni 88 katika kuweza kufanya kuboresha pale, this is a joke, bilioni 88 haiwezi ikatuambia kitu chochote. Asilimia 46 ndio pekee inapatikana kutoka katika mapato yetu ya makusanyo ya TRA pale bandarini, kwenye mipaka yetu na maeneo mengine. Tunataka kuiona sasa bandari inatoka katika hatua moja inakwenda kwenye hatua nyingine. Nami niseme tu, tumefanya jaribio hilo, pale Tanga kuna fedha zimetumika na Serikali tumeweza kupanua Bandari ya Tanga kwa namna moja ama nyingine. Kwa tafsiri hiyo maana yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoka sasa katika metric tones 750,000 tunakimbilia metric tones 3,000,000. Haya yanaweza kufanyika kwenye bandari yetu ya Dar es Salaam. Katika hotuba Mheshimiwa Waziri ametuambia tonnage zilizokuwa zinapita pale ni milioni 20, bado hazitoshi Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Naamini, sisi Waswahili tumezoea kusema mzigo mzito mkabidhi Mnyamwezi, lakini naamini hata Wapemba vilevile mzigo mzito wanaumudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa aje hapa na mpango mkakati wa kuweza kuangalia suala zima la PPP tuweze kuwekeza ili sasa tuweze kuona tunakwenda kutatua kero za wananchi kule katika majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wote wamesimama hapa wanazungumza suala la barabara. Wabunge wamesimama katika Wizara zilizopita wanazungumza masuala ya dawa, vituo vya afya na mambo mengine; fedha iko pale bandarini kwa hiyo, tuchangamke tuweze kuhakikisha tunaleta utaratibu uliokuwa sahihi ili sasa tuweze kuona wanakuja hapa wawekezaji wanakwenda kuwekeza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kitu kimoja; juzi niliweza kuwasiliana na Mwalimu wangu, Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, aliniuliza hivi Mheshimiwa Mpembenwe una nini la kusema kuhusiana na suala zima la bandari pale? Nikamwambia mimi naangalia katika eneo moja tu, katika economic perspective. Akaniambia hapana, mbali ya economic perspective angalia vilevile suala zima la mambo ya operation, pale pana shida, halafu angalia vilevile suala zima la ownership. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la operation ametoka kuongea hapa ndugu yangu Mheshimiwa Kilumbe; amesema kwamba, pamoja na matatizo yote ya TICTS, lakini fedha walizokuwa wanatoa ni nyingi kuliko zilizokuwa zinapatikana kwa kupitia Mamlaka yetu ya Bandari. Kwa hiyo, niwaombe sana, Serikali waje na mpango mkakati wasiogope, sisi ndio tumetunga sheria. Kama leo Profesa anasimama hapa anatuambia barabara hii inajengwa kwa EC + whatever F, barabara hii inajengwa, why can’t we do this pale bandarini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana tuliowapata sasa hivi Mkurugenzi Mtendaji anafanya kazi vizuri pamoja na wasaidizi wake. Twendeni tuwape moyo vijana hawa. Hizi ndio brain tunazohihitaji katika nchi hii ili tuweze kuibadilisha. Tusikae na yale mawazo ya kizamani eti tunakwenda kuuza nchi, nchi itauzwa na Mtanzania mwenyewe? Hiki kitu hakiwezekani. Kwa hiyo, niwaombe waje na mpango mkakati, ili sasa tuweze kuona bandari yetu ile inakwenda kuchangia pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, life expectance ya pale Singapore ya watu kuishi unazungumzia miaka 83, kwa nini? Watu wanakula bata. Bandari inatengeneza fedha za kutosha, wananchi wana- enjoy maisha. Hatuzungumzii economic growth isipokuwa tunazungumzia economic development, ndio maana life expectance ya wananchi wa Singapore ni miaka 83. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mtanzania wa kawaida atahangaika hangaika, akishamaliza miaka 60, 60 au 62 akisha- retire tunachukua kamba tatu, safari imeisha. Nini? Ni kwa sababu uchumi wetu unakua, lakini kukua kwake sio uchumi endelevu. Tunapozungumzia economic growth kuna tofauti kubwa sana na economic development. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Profesa Mbarawa ajitahidi na wataalam wake, waje na mpango mkakati tuweze kuhakikisha tunakwenda kuboresha bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)