Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi. Nianze kwa kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ambapo amekuwa Rais wa mfano ndani ya nchi na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Mbarawa amekuwa ni Waziri msikivu, mchapakazi na mnyenyekevu pamoja na timu yake. Naomba moja kwa moja nijielekeze katika mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi naweza kusema ni moyo wa uchumi katika nchi yetu. Hatuwezi kukuza uchumi wa nchi kama miundombinu ya usafirishaji wa watu na bidhaa ni mibovu. Duniani kote katika biashara wanategemea zaidi ya asilimia 98 mawasiliano ya usafirishaji wa bidhaa kwa anga, barabara yaani nchi kavu, majini yaani meli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kuongelea bandari yetu. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kwa mujibu wa Sheria Namba 7 ya Mwaka 2019 inaruhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi katika shughuli za utendaji wa bandari tangu mwaka 2000 kimkataba. Ushauri wangu kwa Serikali, naishauri Serikali iingie mkataba na kampuni yenye uwezo, ili kuongeza ufanisi, tija na mapato kwa Serikali, ili kuepusha hasara kwa wafanyabiashara na ucheleweshaji wa mizigo yao, ma-container huko bandarini na kwenye kupakua mizigo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Dar-es-Salaam ina changamoto nyingi sana, naweza nikazitaja chache; baadhi ya changamoto ni haina viwango vya tija kwa huduma za bandari, mifumo ya TEHAMA haisomani, idadi ndogo ya miundombinu ya kuendesha bandari. Vilevile Bandari ya Dar-es-Salaam imefikia ukomo kuhudumia shehena kubwa za mizigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia wenzetu, mfano majirani zetu Kenya, Bandari ya Mombasa au Durban South Africa, wanafanya kazi vizuri sana, lakini Bandari ya Dar-es-Salaam ni sawasawa mfano unachukua kirikuu hapa unakipeleka kuchukua magunia ya mahindi Soko la Kimataifa la Kibaigwa huku mpinzani wako anaenda na semi-trailer kuchukua yale magunia. Kweli hiyo inawezekana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile imekuwa kero sana kwa wafanyabiashara, tumeona hata huu mgomo wa juzi Kariakoo. Vilevile bandari hii imekuwa inasababisha uchelewashaji huu, wafanyabiashara wanasubiri ma-container yao kuyatoa wiki tatu, mwezi, wengine mpaka miezi miwili, hali inayosababisha mitaji ya wafanyabiashara inakata, hali ya maisha inapanda kuanzia kwa wafanyabiashara wa juu mpaka wa chini, bidhaa zinapanda, imekuwa shida tupu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa kuwa bandari ukitoa mzigo Korea mpaka Dubai unatumia Dola 500 tu, lakini ukitoa Dubai mpaka hapa ni zaidi ya Dola 4,000 na hapa ni karibu, tubadilike. Sasa ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Waziri, leo hii kwa kweli, shilingi yake itakuwa halali yangu. Nataka kufahamu kwa nini Serikali inasuasua kuruhusu sekta binafsi kushiriki katika uendeshaji wa bandari? Kesho Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha, shilingi yake ni halali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja katika barabara. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais ametenga zaidi ya shilingi trilioni tatu kwa ajili ya kuunganisha barabara katika mikoa saba. Pamoja na Mkoa wangu wa Arusha zimeguswa barabara nyingi sana, lakini kuna kipande ambacho Makamu wa Rais juzi ameenda kuzindua Waso mpaka Sale, lakini hiki cha Sale mpaka Mto wa Mbu naomba barabara hii ijengwe kwa haraka sana. Wananchi wanaotoka Loliondo kule wamekuwa wakipata shida sana, wanakaa njiani hata siku tatu vilevile lile ni eneo kwa ajili ya watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona mama anatangaza Royal Tour, lakini pia na hizi barabara nazo tuangalie tuzipe kipaumbele. Barabara ya Sale mpaka Mto wa Mbu naomba Mheshimiwa Waziri aipe kipaumbele sana barabara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije moja kwa moja upande wa reli. Naipongeza miradi ya ujenzi wa reli za kisasa, SGR, lakini kinachonisikitisha Lot 1 na Lot 2 kwa nini mpaka sasa hivi hazijakamilika? Kadogosa tunamwamini utendaji wake, tunajua ni mtendaji mzuri sana, lakini hapa tatizo ni nini? Watanzania wana hamu na reli yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashauri, reli hii itakapokamilika, naomba waalikwe sekta binafsi nao ikiwezekana waendeshe reli hii. Serikali imeshaweka nguvu zake kwenye miundombinu, lakini itakapokuja sekta binafsi itasaidia ushindani wa kibiashara, pia kukuza mnyororo wa ajira, pia kuongeza ushindani hatimaye ubora wa kukuza kipato kwa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kupongeza Air Tanzania. Tumeona Rais mwanamke, tumeona kuna marubani pale wanang’aa wanawake. Nimemwona Captain Hilda Ringo, Captain Salha na wengine. Tumeona ma-air hostess wamependeza kweli, wana kiwango cha kimataifa. Niwapongeze sana, wapige kazi waendelee kuiletea nchi yetu sifa, waendelee kuhudumia vizuri. Tunajua na wenyewe wanapokea wageni mbalimbali wakiwemo na watalii, waendelee kutangaza nchi yetu, wafanye kazi, wamependeza sana na ni warembo kiwango cha kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)