Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jambo la kwanza kabisa nipende kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wangu wa Mji wa Tunduma kwa kunipa nafasi hii ya kuhakikisha kwamba nakuwa Mbunge, nawawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nataka kuzungumza ni utawala bora. Tunapozungumzia utawala bora katika nchi hii hakuna. Jmbo lingine tunasema kwamba tunakaa kwa amani hatukai kwa amani bali tunakaliana kwa amani katika nchi hii; ndicho ambacho kinaonekana katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninazungumza haya kwa sababu nina mifano mingi sana ambayo nataka kuitoa mbele yako. Mfano wa kwanza nilivyosema kwamba hakuna utawala bora, nimeona katika uchaguzi kwa ajili wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, uchaguzi umefanyika tarehe 25/10 kupata Madiwani lakini Meya wa Jiji Dar es Salaam amekuja kupatika mwezi Machi, 2016. Jambo hili linaonesha ni jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi haiko tayari kuheshimu utawala bora na pia kuheshimu demokrasia katika Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni aibu kubwa pia kwa Kiongozi wa Kitaifa kushindwa kuwaheshimu viongozi wa chini. Alivyokwenda kuzindua na kufungua miradi ya maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam alishindwa kumtambulisha Meya wa Jiji la Dar es Salaam na kumpa nafasi ili aweze kuzungumza ili kuwakilisha Jiji la Dar es Salaam. Jambo hili linanikumbusha mbali sana, namkumbuka sana Mwalimu Nyerere aliwaheshimu mpaka Wenyeviti wa Mtaa na Madiwani katika maeneo waliyokuwa wakiishi. Nashangaa utawala wa Dkt. Magufuli umekuwa unadharau viongozi wadogo na wao wakitegemewa kuheshimiwa baadaye jambo hili litakuwa ni ndoto kwao kwa sababu hawaheshimu utawala bora na demokrasia hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni madai ya Walimu. Kila wakati tunasikia Chama cha Mapinduzi wanajinasibu kwamba kuna elimu ya bure, mimi nasikitika sana katika Taifa hili hakuna Mtanzania hata mmoja anayependa elimu ya bure wala kitu cha bure. Tunasema elimu inayotolewa sasa hivi itolewe kwa kodi za Watanzania na siyo elimu ya bure. Kwa hiyo, tafsiri kuanzia leo tunahitaji elimu inayotokana na kodi za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tusitegemee kupata elimu bora kama Walimu wanakuwa na madai makubwa, hawawezi kutimiziwa haja zao za kupata mishahara na wakati maisha yao na mishahara yao pia ni midogo. Ni vizuri Serikali hii ikajaribu kutazama kwanza huduma za Walimu ambao wanatoa elimu lakini pia ikaangalia ni namna gani inaweza ikaboresha maslahi ya Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusiana na mambo ya TAKUKURU. TAKUKURU ni taasisi muhimu sana katika Taifa hili na kama kweli tunahitaji uwazi na tunahitaji utendaji kazi mzuri ambao utaondoa mashaka ya rushwa katika nchi hii ni lazima TAKUKURU wapewe nafasi ya kuwa na uwezo wa kupeleka shtaka mahakamani bila kumpelekea mtu yeyote kufanya uchunguzi. Jambo hili katika rekodi mbalimbali linaonyesha kwamba kesi nyingi ambazo TAKUKURU wanajaribu kupeleka mahakamani wanashindwa kwa sababu kesi zile zinaandaliwa na watu ambao hawakuhusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ushauri huu Vyama vya Upinzani vinatoa kila wakati ndani ya Bunge ni vizuri mkasikiliza kwa sababu tunatoa kwa faida ya Taifa hili na si kwa faida yetu sisi. Inaonekana kwamba hakuna hata siku moja mmesimama mkakubali kusikiliza ushauri huu na mnaendelea kuanzisha taasisi ambazo hazina meno, wala hazina tija na haziwezi kutekeleza majukumu yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika suala la biashara. Nchi yoyote duniani haiwezi kuendelea kama wafanyabiashara wake wataendelea kuwa maskini na watakuwa hawatengenezewi mazingira mazuri ya kufanya biashara. Taifa hili wafanyabiashara wamekuwa kama wanyonge katika Taifa lao, wafanyabiashara sasa hivi wameshindwa kuangiza mizigo nje kwa sababu ya taratibu mbalimbali ambazo haziwapi nafasi ya kufanya biashara na kuwa na mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mataifa mengi duniani yanaandaa wafanyabiashara ili waweze kupata mitaji na baadaye wawe walipa kodi wakubwa katika Taifa lao. Nchi yetu ya Tanzania imeonekana kwamba sasa wafanyabiashara wote wanaoibuka katika Taifa hili wamekuwa wanabanwa na wanashindwa kutekeleza wajibu wao vizuri. Tunasema Serikali lazima ibadilike, iwatazame wafanyabiashara na iwaandae vizuri ili waweze kuwa wafanyabiashara wakubwa na waweze kulinufaisha Taifa hili na waweze kuwa walipa kodi katika Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia ni kutoa mfano wa Bandari ya Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam sasa inakwenda kufa siyo muda mrefu kwa sababu tumeshindwa kuingia kwenye ushindani wa kibandari na mataifa yaliyoko jirani na sisi. Angalia leo katika takwimu za mizigo ambayo inashuka katika Bandari ya Dar es Salaam, Zambia peke yake ni asilimia 34 ya mizigo imeshapungua wanashusha katika Bandari ya Beira. Kwa maana hiyo tumeshindwa kuingia kwenye ushindani wa kibandari kwa sababu ya kuweka masharti ambayo hayana tija kwenye bandari zetu. Lazima tufike mahali tubadike na tutazame ni namna gani tunaweza tukajenga uchumi bora kama tutaendelea kuua vyanzo vya mapato ambavyo tunavyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Kongo ni karibuni asilimia 46 wameacha kupita pale. Sababu ni kwamba Wizara ya Uchukuzi wameingia mkataba na Congo DRC Lubumbashi kuhakikisha kwamba mizigo yote wanayokuja kuchukua katika bandari ya Dar es Salaam wawe wanalipia kwanza. Wakongo wameona huu ni upuuzi, wameamua kuhamia kwenye Bandari ya Beira na sasa hivi wanapita kule wanaendelea na shughuli zao. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali inapoanzisha jambo ijaribu kupima na kutathmini jambo hili lina hasara gani katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tumepata taarifa na tunasikia kwenye vyombo vya habari Mheshimiwa Rais anawaambia vijana waende vijijini wakalime. Vijana kwenda kulima vijijini kunahitaji pia maandalizi ya kutosha, je, wana mashamba, wamewezeshwa kiasi gani kwamba wanaweza wakafika kijijini na wakaanza kulima kilimo chenye tija na kujiletea maendeleo? Tunaomba sasa Serikali ya Chama cha Mapinduzi wanapotoa matamko wajaribu kutazama ni nini ambacho wanamaanisha, wasiwaswage wananchi na kueleza kwamba ni lazima waende kijijini, hata yule mwananchi ambaye yuko kijijini anayelima haoni tija ya kuendelea kulima kwa sababu hakuna masoko ambayo yako na pia haelewi ni namna gani ya kulima kwa sababu tija hakuna katika kilimo hiki. Tunaomba Serikali ijipange, iwawezeshe Watanzania ili kuhakikisha kwamba Watanzania hawa hata kama wanakwenda kulima watakwenda kulima kilimo chenye tija ambacho kitawasaidia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunasikia matangazo mbalimali kuhusiana na vifo vya kina mama na watoto. Leo hii katika taarifa hii inaonesha kwamba mpaka 2018 watahakikisha kwamba kuna punguzo la vifo vya akina mama na watoto kwa asilimia 20, jambo hili ni aibu sana. Kwa kweli kifo kinafika mahala tunaweka takwimu za kupunguza asilimia 20, ni mambo ya ajabu kabisa. Lazima tufike mahali tujadili, hivi leo kama Wabunge wangekuwa wanatuwekea hapa wanasema jamani Wabunge tunakufa sana humu tupunguze asilimia 20 kwa bajeti ambayo tunaiweka, kila mmoja angekataa kwamba afadhali tuweke bajeti asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa tutazame jambo hili kwa umakini zaidi, tuangalie maisha ya watu, tuangalie maisha ya wananchi wetu kama kuna tatizo la kuweka fedha kidogo, fedha iongezwe kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanasaidia akina mama na watoto ili waendelee kuwa wazima na watu wanaobeba ujauzito wawe na uhakika kuzaa watoto na watoto wao kuwa hai muda wote. Jambo hili tunaona lazima lifanyike haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni matangazo ya television kukatishwa…
Bado Mheshimiwa, kengele ilikuwa bado Mheshimiwa.