Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Nami namshukuru Mungu kwa kuniwezesha jioni ya leo kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kujadili na kuishauri Serikali katika bajeti hii ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachangia masuala machache tu. Kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri wetu wa Wizara hii, Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa kwa kazi anazozifanya kwa weledi mkubwa na uadilifu mkubwa sana, na manaibu wake wawili ambao anaongoza nao, Makatibu Wakuu wote wawili na Naibu Makatibu Wakuu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nasimama kuipongeza Serikali kwa kutekeleza ahadi zake ambazo imekuwa ni mara chache, lakini mara hii kwa Awamu hii ya Sita katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi, nataka niseme, kongole sana watu wa Wizara ya Ujenzi. Tumeona barabara za kilomita 56 ambazo juzi juzi tu tumesaini, lakini barabara za Mji wetu wa Itigi kilomita kumi na kilomita 56 tuna kilomita kama sitini na kitu ambazo zinatekelezwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo upungufu pamoja na shukurani hizi, unapojenga barabara kuna matukio yanajitokeza. Pale kwenye barabara ya Itigi kumetokea shida kidogo, kuna watu baada ya kutengeneza ile barabara kumesukumiwa kama changamoto kidogo. Tulishaongea na Mheshimiwa Waziri na anajua, lakini kama Mtendaji Mkuu mtusaidie wale wananchi mwakani tena wasipate taabu ile ambayo wamepata mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri na kuzungumzia kidogo kuhusu LATRA. LATRA imeboreshwa, ameteuliwa Mtendaji Mkuu mpya, tunaona mafanikio yake, lakini usimamizi na kusikiliza maoni ya wadau. Wamekuwa wasikivu mara hii kuliko mara zote kule nyuma. Ninayo rai moja, wanapoenda kutunga kanuni, tunahitaji zitungwe kanuni kwa maslahi mapana ya nchi. Tuangalie zaidi wananchi kuwawezesha kuliko kuwakomoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na tabia kwamba wanapoachiwa mamlaka kutunga hizi kanuni, wanakuja na kanuni ambazo siyo rafiki kwa wananchi ili kutengeneza adhabu nyingi kwa wadau. Naomba sana nishauri LATRA mara hii, mje kama wadau ambao mtawawezesha Watanzania masikini ambao wana nia ya kujikwamua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja moja, eti mtu akiwa na bodi ya kachina, hawezi kuweka engine ya nchi nyingine. Bodi ni bodi tu, engine yake ilishakufa, angalia ubora wa chombo kile ambacho kimeenda kubeba wananchi wa nchi hii, ndio kitu cha msingi. Kabadilisha difu, kafunga ya Mitsubishi, ina hasara gani? Tunataka tuone je, kile chombo katika ufanyaji wake wa kazi, kitafanya kazi vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo katika magari ya mizigo, na hivyo hivyo katika vyombo vingine. Tuangalie ufanisi, tusiangalie kutoka kwa mtengenezaji. Watengenezaji wengine vitu vingine wameshindwa, wanakuja na sura nzuri ya bodi, engine mbovu, miaka mitano imekufa. Utachukua engine ya Mchina uende kuweka? Unachukua engine ambayo ni nzuri, engine ya Mzungu, unaifunga pale, gari ile inafanya kazi vizuri. Nilikuwa na rai hiyo nilitaka niwashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo ambalo linaendelea, VTS ina miaka sita karibu saba sasa, lakini VTS hii haijathibitishwa na Mamlaka ya Ubora (TBS), lakini ni sharti la leseni. Linakujaje sharti la leseni, kitu ambacho ni delicate? Kwa hiyo, naomba wafungue milango mingine kwa watu wengine waweze kuleta vyombo ambavyo ni bora. Kama ni sharti la leseni, basi TBS wathibitishe, lakini ukaguzi wa magari udhibitiwe na TBS. Tusije na vitu vipya tukaharibu nchi ikawa ni milolongo na milolongo na milolongo. Ahsante Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo la hawa wakandarasi ambao wanajenga reli yetu. Wakandarasi hawa kwenye local content hawapo kabisa. Wao wenyewe ni mkandarasi mkuu, yeye mwenyewe ndiye anayeunda kampuni tanzu, anaweka Mtanzania mmoja bosheni, anaonekana ni mbia kumbe hamna lolote. Ipo hiyo Lot 1, Lot 2 na Lot 3, wanajua. Makampuni tanzu yapo, lakini ni ya Waturuki hao hao. Tunaomba sana lifanyiwe kazi, ikiwezekana TAKUKURU waingilie kati, waangalie hili jambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo jambo lingine ambalo nashauri leo, nataka nichangie, ni suala la namna gani bandari yetu itakwenda kufanya kazi na kuzihudumia hizi nchi ambazo zinategemea bandari hii? Leo hii watu wa Lubumbashi ambao ndio tegemeo letu, mizigo yao imeshaanza kwenda Durban. Kutoka Lubumbashi kuja Dar es Salaam, kuna tofauti ya kilomita 900, lakini mtu yuko tayari kwenda Durban kwa sababu hakuna usumbufu, yuko tayari kwenda Nakala kwa sababu hakuna usumbufu. Ipo sababu, sisi pia hata barabarani kuna usumbufu mkubwa sana, lakini LATRA wanaweka masharti mengine magumu kwa wasafirishaji. Kwa hiyo, nashauri twendeni tukatengeneze miundombinu rafiki, sheria rafiki kwa ajili ya bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari yetu, tunategemea sana hizi nchi, lakini tulitakiwa tuzitegemee sana nchi ambazo tumezikomboa. Tumepigana vita Uganda, leo tunasafirisha mizigo ya Uganda kwa asilimia mbili tu. Sababu ni nini? Bandari ya Mombasa wamefungua Dry Porty pale Kampala. Ukipakia mizigo yako pale, bandari ndiyo wanachukua ile mizigo aidha ni kwa treni, kwa Barabara, wanafikisha kwenye Bandari ya Mombasa. Wakishapakia ule mzigo kwenye meli, unaletewa draft uko Kampala. Ukishamaliza kuangalia draft yako kama vitu ulivyoweka ni sawa, una-print-iwa bill pale pale Kampala. Sisi msafirishaji wa DRC anatoka Lubumbashi inabidi aje Dar es Salaam, achuke draft, aangalie mzigo wake unakoenda, kusaini kama ni sawa, ndiyo a-print-iwe bill, aanze safari ya kurudi DRC. Lazima tuwe wabunifu, tutoke katika zama zile tulizokuwa nazo zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kufungua dry port kweli Lubumbashi? Wanatutegemea, ukachukua mizigo nauli zile zile ukaziingiza gharama za usafirishaji kwa yule mteja, badala ya kusafiri, bandari inakuwa na mzigo ule, inafikisha Bandari ya Dar es Salaam; halafu pale pale Lubumbashi ana-print draft, baada ya draft ikitoka, akapata bill yake pale pale. Utampunguzia risk ya kusafiri kwa barabara kwa gari yake au kwa ndege, unatengeneza mteja mwingine kesho na kesho kutwa. Leo watu wanakwenda Durban kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenytekiti, naomba kushauri Serikali yetu tubadilike, twendeni na wakati, tuifanye nchi hii iwe nchi kwa maslahi mapana ya nchi hii. Yapo mengine, muda hautoshi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)