Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii ambayo inaunganisha nchi na inaunganisha uchumi. Naomba nianze kwa kumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu kwa jinsi ambayo amekuwa akiitendea haki Wizara hii ambayo ina miradi mikubwa yenye fedha nyingi na imeendelea bila kusimama na muda siyo mrefu nchi yetu itakuwa ipo katika hali ya juu sana katika miundombinu katika Afrika. Nimpongeze sana mtendaji wake mkubwa ambaye ni Waziri kwa jinsi ambavyo wanaitendea haki Wizara yao, wanafanya kazi vizuri na kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Waziri, katika siku chache zilizopita amenikumbuka na mimi katika jimbo langu, amekubali tena kwa moyo mweupe katika bajeti hii kwamba atanipatia kilometa kumi za lami pamoja na taa katika Mji wangu wa Nduguti pale Wilaya mpya, katika barabara ambayo inatoka Iguguno kuelekea Bariadi mpaka Simiyu kupitia Sibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na kunipa hii, basi mipango yake ya kuhakikisha anaunganisha barabara hii kutoka Iguguno mpaka Simiyu asiiache mbali, kwa sababu ni barabara ya kiuchumi, kiasi kikubwa cha pamba kinachotoka Mkoa wa Mara, Mkoa wa Simiyu wanapita barabara hii na wanakuwa wameokoa kilomita nyingi sana badala ya kuzungukia Mwanza mpaka Shinyanga. Kwa hiyo, naomba ahakikishe barabara hii inaunganika ili wananchi wangu wa Mkalama na wa Mkoa wa Mara na Bariadi waweze kuunganishwa na nchi kirahisi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, reli yetu inayotoka Manyoni kwenda Singida, kipande hiki kimesahaulika. Sehemu kubwa ya reli ya zamani imekarabatiwa na inafanya kazi. Mpaka leo kwenda kaskazini kule, watu wanaenda kwa treni, lakini kipande hiki muhimu sana kilichojengwa tangu enzi ya mkoloni kimesahaulika. Hii reli ni muhimu sana inaweza kuwa feeder road ya kupeleka mizigo kwenye SGR pale Manyoni. Kwa hiyo, nakuomba sana katika bajeti za ukarabati wa reli, kipande cha reli cha kutoka Manyoni kwenda Singida…

MHE. ELIBARIKI I. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa Taarifa.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji, kaka yangu Mheshimiwa Francis kwamba, siyo tu reli hii imesahaulika, bali Wana-Singida wanatamani kuona kipande cha SGR kinatoka Manyoni na kufika Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa mchangiaji taarifa kwamba vitunguu vyote wanavyokula mikoa karibu ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam, viazi vyote wanavyokula mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam, vinatoka Singida. Kwa hiyo, kwa kuikumbuka reli hii, itakuwa imeleta ukombozi mkubwa sana kwa mikoa hii mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa mchangiaji taarifa hii.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Francis, taarifa.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa mikono miwili. Rafiki yangu Mheshimiwa Kingu amesahau, na kuku wote wa kienyeji katika nchi hii wanatoka njia hiyo. Kwa hiyo, kipande hiki ni cha muhimu. Hata ng’ombe, barabara zinaharibika kwa kupakia ng’ombe. Kwa hiyo, wakija na reli itakuwa ni vizuri. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kipande hiki mkikumbuke, kinajenga uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tena nimwombe Mheshimiwa Waziri, katika reli yetu ya SGR, huduma karibu zitaanza. Nawaomba sana, wananchi wameisubiri reli hii kwa hamu kwamba huduma ya usafiri sasa itakuwa ni nyepesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napata hofu kidogo, niliona uwezekano wa nauli zitakabvyokuwa, watu wa chini naona kama watakuwa wanapata shida. Naomba sana, ziwepo category zote za nauli. Starehe ya juu kabisa tunaotaka kulipa mamilioni sijui malaki, ziwepo; wale wa uwezo wa kati iwepo, vile vile ziwepo madaraja ya chini kabisa ambayo wananchi wanaweza wakapanda, wakatumia. Wote kwa pamoja kwa uwezo wetu tuweze kutumia reli hii ya SGR itakapoanza kufanya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jamii huduma zote zipo. Leo hii wako akina dada wanaovaa wigi la bei ndogo, lakini wapo wanaovaa wigi la Shlingi laki tano. Leo hii wapo watu wanavaa suti za mtumba na wengine wanavaa suti ya mamilioni, ili mradi ipo, wewe utaenda kwa uwezo wako. Kwa hiyo, naomba katika SGR, yale mabehewa yatakapoanza kufanya kazi, ziwepo nauli za bei ya chini, wananchi wa kawaida wapande; ya kati na ya juu yenye starehe zote iwepo, ili mtu apande kutokana na uwezo wake. Isije wananchi wetu wa hali ya chini wakawa wanaangalia tu treni ya SGR inakwenda kwa kasi, wanaiona kwa macho, wao wanahangaika na usafiri wa kutumia saa nyingi kufika maeneo ambayo wanataka kwenda. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hili waliangalie sana huduma itakapoweza kuanza wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo namwomba Mheshimiwa waziri, nashukuru kwamba barabara nyingi zinajengwa, lakini mpaka sasa nasikitika, bado kila barabara kubwa ukiiona, utaona wakandarasi ni Wachina, Wazungu ama vyovyote. Wakandarasi wetu wa ndani bado hawajapata kazi kubwa. Najua kitakachosemwa kikubwa ni mtaji. Hebu niombe kama Wizara, tuangalie namna ya kuwaunganisha Wakandarasi wetu wa ndani, ili waweze kuchukua kazi kubwa ili nasi fedha zetu za kigeni na uchumi wetu uweze kubaki ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba kwenye kilimo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Francis Mtinga.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nilikuwa naomba tu nimalizie kwamba nashukuru pale kwenye bwawa langu la msingi, mradi wa Shilingi bilioni 34 wamepewa Wakandarasi wazawa. Kwa hiyo, hata kwenye barabara kubwa kubwa wakipewa wazalendo tutaendelea kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)