Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Deus Clement Sangu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa fursa hii, nami kuwa katika orodha ya wachangiaji kwenye bajeti hii muhimu ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimwia Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa katika sekta hii ya uchukuzi. Ameijali, na amekuwa akiijali kila wakati na kuipa bajeti ya kutosha kuendesha mambo yao wakati kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Profesa Mbarawa na wasaidizi wake Manaibu, kazi yao ni nzuri na tunawapongeza sana. Vile vile watendaji walio chini yake, Katibu Mkuu na Watendaji wa Taasisi zilizo chini yao, nikianza na TPA pale, na bahati nzuri tuna kijana mzuri pale MD wa TPA Mbossa, na ndugu yangu Mativila wa TANROADS na wengine wote wanafanya kazi nzuri, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchango wangu leo nitakuwa na mambo mawili muhimu. La kwanza, nitaongelea mambo ya Mkoa wangu wa Rukwa, na pili nitakuja kushauri mambo makubwa kwa mustakabali wa Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, juzi alikuja mkoani kwetu kwa ajili ya kuanza mkataba wa kuanza ujenzi wa ndege pale Sumbawanga, halikadhalika Barabara yangu ile ya kutoka Mutendo – Muze ya zaidi ya Shilingi bilioni 45 pamoja na Barabara ya Mathai kwenda Kasesha, tukupongeze, na kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutujali kwa kiwango kikubwa Mkoa wa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo, kuna jambo ambalo ameliongea hapa kwa msisitizo mkubwa kwenye hotuba yake, nilikuwa namsikia kwa umakini Profesa, juu ya meli kwenye Ziwa Tanganyika. Sisi uchumi wa mikoa mitatu hiyo kwa pamoja kwa maana ya Rukwa, Katavi na Kigoma tunategemea sana hiyo meli lili ika-boost uchumi wa maeneo hayo matatu. Ni sehemu ambayo nchi tunazopakana nazo kwa maana ya Burundi, DRC na maeneo mengine kama Zambia, yana bidhaa nyingi wanazozitegemea kutoa mikoa hiyo mitatu niliyoitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu sana. Mwaka jana tulimpigia kelele hapa Bungeni juu ya meli, akatuahidi. Hivi leo amesema mwezi ujao Juni, mkandarasi ataanza kazi. Bahati nzuri, commitment aliyoifanya hapa iko kwenye interval ambayo tutakuwa humu Bungeni, na tutakuwa hatujachangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wananchi wana matumini makubwa na ahadi aliyotoa leo. Unaona katika maeneo mengine wana meli tano, sita, saba, lakini Ziwa Tanganyika lime-collapse, na ni ziwa ambalo linatu-link na nchi ambayo tukiwekeza vizuri, mikoa hii ita-boost na tutaongeza pato la Taifa. Kwa hiyo, naomba jambo la meli, tuko serious tumekaa nawe katika vikao vingi, naamini baada ya bajeti tena tutakaa utupe mpangokazi ili sisi wawakilishi wa maeneo hayo, tuwe na Imani sasa kwamba mnaenda ku-address tatizo la Lake Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba Profesa, Barabara ya Ntendo – Muze ile alienda kufanyia endorsement kwa maana ya kwenda kumkabidhi mkandarasi, kazi inaendelea vizuri, lakini kwa bonde langu la Ziwa Rukwa ambapo Barabara yote hii kwa urefu ni kilometa 200, Ntendo – Muze mpaka Kilyamatundu ni Kilometa 200. Kule ndani ya bonde la Ziwa Rukwa sasa hivi kuna shughuli kubwa inaendelea ya exploration, ambayo tuna wawekezaji wa gesi ya Helium, ambao wame-invest zaidi ya kufanya tu utafiti zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 30.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii Barabara ina umuhimu mkubwa kwa sababu uchimbaji unaanza wa majaribio mwezi wa Nane. Kwa projections zilizopo, helium iliyopo bonde la Ziwa Rukwa inaenda kutupatia pato la Taifa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 100, ndani ya miaka mitano tutakuwa tuna-hit Dola za Kimarekani milioni 500. Kwa hiyo, hata hii investment tutakayoiweka kwenye Barabara hii itarudi ndani ya muda mfumi kwa sababu uchimbaji wa gesi ya Helium itakayofanyika pale itakuwa na impact kubwa, siyo tu kwa Mkoa wa Rukwa, lakini itakuwa na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hii Barabara tuiongezee sasa bajeti. Ina umuhimu, sio kwa Mkoa wa Rukwa lakini uchumi mkubwa wa Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Profesa, hili jambo akalimalize, kipande kile akiongezee hela, kilometa 200 zote ziwe kwenye operation zikamilike kutoka Muze mpaka Kilyamatundu pale na baadaye kwenda Kasansa kwa ndugu yangu pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuongelea mambo ya jimboni, nije kwenye mambo muhimu ya kitaifa, na hapa profesa naomba tusikilizane kwa umakini. Kuna mambo mawili ambayo yamekuwa yaneleta dosari kubwa sana kwenye Wizara hii na dosari hii imekuwa ya muda mrefu na kila mwaka unavyoendelea dosari hii inazidi kuwa kubwa. Mambo mawili, riba kwa wakandarasi. Riba kwa wakandarasi imekuwa ni jambo ambalo linaumiza taifa hili. Mwaka 2021/2022 wa fedha uliokwisha, tutachulia tu shirika moja kama TRC, tulilipa riba ya Dola za Kimarekani 1.34 kwa sababu tu tumeshindwa kulipa certificate 24, na Profesa haya mambo yako ndani ya uwezo wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna jamnbo la VAT exemption, ucheleweshaji, na haya yanafanyika kwenye Wizara ya Fedha ya ndugu yangu Mwigulu Nchemba, yanaletwa pale exemption zinachelewa. Mwaka jana. na nachukulia mfano wa TRC, tulilipa bilioni 8.35, kwa ajili ya kwamba exemption (riba) imechelewa. Sasa Profesa, leo hii nataka kesho utakapokuwa una wind-up bajeti yako utueleze umejipangaje kuondoa tatizo la kulipa penalty na hizo riba zisizokuwa na msingi? La sivyo, mimi binafsi nitataka shilingi yako utueleze umejipangaje. Bado tunakusubiri Novemba, baada ya kuja kujadili hapa ripoti ya CAG. Hizi taasisi zako zinapewa bilioni nyingi za fedha na riba inapotokea ni billions of money, ukizisoma zimekuwa zinakuwa kila mwaka. Sasa hii inatupelekea sisi ambao tunakuja ndani ya Bunge hili na pengine wewe mwenyewe tatizo hili halikuumi; ninaamini sasa kwa sauti yangu leo humu Bungeni utakwenda ku- take action, mfute riba, kwa sababu miradi mingine riba haina maana. Tunakuwa tumepewa fedha za mikopo na World Bank au taasisi nyingine, fedha iko pale, sasa mnapataje riba ilhali hela zipo, kazi imefanyika mme-certify, mnashindwaje kulipa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia VAT exemption haiwezi kuwa tatizo kwenye nchi, ni internal communication ndani ya Serikali, Wizara yako na Wizara ya Fedha; na bahati nzuri fedha hizi zinatoka Wizara ya Fedha zinakuja kwako kwenda kwenye utekelezaji lakini VAT ambayo iko ndani ya uwezo wetu inatusababishia tulipe riba ya bilioni nane na bilioni nyingi za fedha. Kwa kweli profesa hili hatutakuelewa, tunaomba mje mtuambie mmejipangaje kwenye Serikali ili kukomesha tatizo la riba kwa wakandarasi ambalo linagharimu taifa na VAT exemption hizi ambazo ziko chini ya uwezo wetu kama Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niongelee suala lingine, variation kwenye Miradi. Miradi hii inakuwa designed, maana tunafanya upembuzi yakinifu, tunakwenda kwenye detailed designed, tunakwenda kutanga za tenda, ghafla unakuta kuna variation zinakwenda asilimia 20, 30, 40, na baadaye unasema au kulikuwa na mchezo wa ku-skip baadhi ya item ili tuje tutumie room ya variation kufanya mambo yetu? Profesa hili jambo ukapitie kwenye taasisi zako kwenye miradi mikubwa kama vile TRC, TANROAD, ATCL na taasisi zote, huko una mabilioni ya fedha. Suala la variation limekuwa ni ugonjwa mkubwa ambao hauleti afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nafikiri muda umekwisha nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)