Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Misungwi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALEXANDER P. MNYETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia kwa kazi nzuri na kubwa anayoendelea kuifanya kwenye taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina barabara ambayo imesemwa kwenye ilani ya mwaka 2000, ikasemwa kwenye ilani ya mwaka 2005, ikasemwa kwenye ilani ya mwaka 2010, ikasemwa 2015, imesemwa 2020, na barabara hii haikuwahi kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Waziri Mbarawa, kwa kuwasikia wana misungwi, kwamba barabara yao ya Ng’wanangwa – Misasi – Kahama sasa inakwenda kujengwa kwa kiwango cha lami. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya wana misungwi kukushukuru sana Mheshimiwa Waziri, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwamba barabara hii sasa inakwenda kujengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina faida nyingi na ndiyo maana faida hizi zimepelekea sasa Serikali kwenda kuijenga kwa kiwango cha lami, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Unajua tumekuwa tukimshukuru Mheshimiwa Rais, wengine wanahisi tunajipendekeza. Kama barabara imeshindwa kujengwa miaka yote hiyo Mama Samia amekuja kujenga kwa nini tusiseme ahsante? Tunashukuru sana, wananchi wa Misungwi wanashukuru na tutaendelea kushukuru sana kwa sababu Rais, huyu ameamua kuijenga barabara hii na tayari; juzi nilikuwa na kikao na Mheshimiwa Waziri, amepiga simu nikiwepo kuagiza tenda itangazwe wiki ijayo, tunashukuru sana. Kwa niaba ya wana Misungwi tunashukuru sana kwa habari hiyo. Kwa kweli tuna Imani kubwa sana na wewe Profesa na kazi hii tuna imani sasa wiki ijayo barabara inakwenda kutangazwa na mkandarasi apatikane mwadilifu na barabara iende ikajengwe ili wana misungwi waweze kupanua uchumi kwenye wilaya yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nataka nishauri. Tuna miji mikubwa ambayo inayokua kwa kasi, Mheshimiwa Waziri anaifahamu, na tumekwisha omba habari ya taa hizi za barabarani. Tuna miji yetu kama ya Misasi, Mbarika, Misungwi, Igongwa, Usagara tupate taa za barabarani ambazo zinabadilisha hata ile sura za miji yetu ambayo inakuwa kwa speed.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo pia ni siku ya kutoa shukrani zetu tu. Wana misungwi kila tulipokuwa tukiomba mambo haya yanafanyika. Fidia ya watu ambao barabara ilipokuwa inajengwa kutoka Usagala mpaka Geita wamelia kwa muda mrefu lakini leo watu hao tayari wamekwishapewa fidia yao, tunaishukuru sana Serikali hii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, kwa kweli tunakushukuru sana lakini pia tukushukuru sana, juzi tumesaini mkataba wa ujenzi wa kivuko kipya cha kutoka Mbarika mpka Buyagu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiposhukuru kwa haya sijui tusubiri vitu gani ili tuweze kushukuru? Kila ambacho tumeomba Serikali ya awamu ya sita mmetekeleza. Tumeomba fidia mmetupa, tumeomba barabara mmetupa, tumeomba kivuko mmetupa, tukimshukuru Mheshimiwa Rais, mnasema tunajipendekeza; tufanye nini sasa zaidi ya hayo? Kwa sababu yote tuliyokuwa tunaomba, yote tuliyohitaji yafanyike Mheshimiwa Rais amekubali kuyafanya, zaidi ya hapo tufanye nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Serikali na muendelee kuchapa kazi kwa style hiyo kwa sababu sisi kwa niaba ya wananchi wetu tunaona mnayoyafanya na tunaamini kila tunayoyaomba mnaendelea kuyatekeleza kadri ya mwongozo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa makini sana kuhusu bandari. Sisi ni wanasiasa lakini pia tunafanya na vibiashara vidogo vidogo. Tunapata adha kubwa sana tunapoagiza mizigo yetu kupitia kwenye Bandari yako ya Dar es salaam. Mimi ninaishi Mwanza, tunapoagiza mizigo kutoka China, Japan na maeneo mengine, mzigo unaweza ukakaa bandarini hata mwezi mzima haujapata mzigo wako. Hiii ni aibu, kama mimi Mtanzania nachukua muda wote huo hao wa nchi jirani wao wana maisha gani? Mheshimiwa Waziri, naomba utumie u-profesa wako kwenye hii bandari ili tuone matunda ya degree nne yako wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunamuomba Mheshimiwa Waziri, dunia imeshabadilika, dunia sasa hivi iko kwenye ushirikiano kati ya Serikali na watu binafsi, kati ya Serikali na Serikali na ndiko dunia ilikofikia. Nenda Marekani, Japan kote wanafanya ushirikiano; lakini sisi tuking’ang’ana Serikali kwa sisi wenyewe hatuwezi kufanya, kwa sababu hata tunavyovifanya sisi wenyewe vimetushinda. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Pofesa Mbarawa, tuna Imani kubwa sana na wewe nenda ukalitafakari jambo hili vizuri uone nchi inakwenda kunufaika vipi ili tuweze kupata tija katika taifa letu. Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Waziri uwezo wako tunaufahmu hakika tunajua kwamba jambo hili litakwenda vizuri na tunaomba utulize sana akili ili nchi iweze kunufaika na bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hiyo naunga mkono hoja.