Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na uhai wa kuweza kusimama mbele ya Bunge letu hili Tukufu na kwa kuanza mchango wangu. Nianze kwa kumpongeza Rais wetu, Mama yetu kipenzi Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kuwa na miradi mikubwa ya barabara yenye jumla ya kilometa 2,035, ambayo itagharimu zaidi ya trilioni 3.7 na ikatekelezwa kwa wakati mmoja. Hivyo basi nichukue fursa hii kumpongeza mama kwa kuona umuhimu wa kuweza kuifungua Tanzania yetu ili tuweze kukua kiuchumi. Kwa sababu panapokuwa na miundombinu mizuri ni moja kwa moja unachochea uchumi wa nchi yako. Rais Mheshimiwa Dkt. Samia anakwenda kufanikiwa katika hili nampongeza na namtia nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wetu wa Ujenzi, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Naibu Mawaziri wake na Watendaji wote wa Wizara hii ya Ujenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya. Sisi tuko nyuma yao kwa yale yote watakayoyafanya ambayo wanajua yatakuwa yanaleta tija katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendeele kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kilometa 107.4 ya barabara ya kutoka Njombe pale Ramadhani kwenda Makete. Barabara ilishakamilika ilishaanza kufanya kazi, lakini kuna changamoto ndogo ndogo, tunaomba sasa wale wananchi ambao hawakulipwa fidia waweze kumaliza kulipwa fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia tunaendelea kuishukuru Serikali kwa Barabara ya Mawengi – Lusitu, kilometa 50 kule Ludewa, lakini vile vile Lusitu - Itoni kilometa 50 kwenye Jimbo lile la Njombe Mjini kilometa 50, kazi inaendelea pale mkandarasi yuko site, lakini bado tunasisitiza changamoto ya kulipwa wananchi wetu fidia. Wananchi wanafurahia barabara, lakini bado wanakuwa na machungu ya kutokulipwa fidia. Tunaomba hili Wizara ilimalize ili tusiwe na dosari katika utekelezaji wa kazi hii nzuri inayofanywa na Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya kutoka Makambako kilometa 295 kwenda Songea. Hii barabara ni mbovu sana imejengwa tangu mwaka 1980. Barabara hii ina mashimo mengi, ni nyembamba inasababisha ajali nyingi, ni hatari hata kwa misafara ya Viongozi wa Kitaifa, ni hatari kwa wananchi, tumeona vifo vingi vinatokea katika barabara hii. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa kusini, barabara hii ikiboreshwa ikitengenezwa kwa kiwango cha lami upya itasaidia hata ule usafirishaji wa makaa ya mawe ambayo yanaendelea kusafirishwa hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa katika bajeti ijayo angalau waangalie kile kipande cha Makambo kuishia pale Njombe Mjini kwenye makutano ya Mkoa wa Njombe na Songea panaitwa Lukumburu, waangalie sana kipande hicho ni muhimu sana na waweze kukitengeneza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niombe ombi rasmi la barabara hii ambayo tumekuwa tukiizungumza tangu mwaka 2010. Barabara ya Ramadhani – Ndandu - Iyayi kutokea Mbeya, hii barabara haina pesa kabisa na tunaomba iingie kwenye mpango mahususi ya kutafutiwa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ina sifa inaunganisha mkoa na mkoa, kwa maana Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Mbeya, lakini imekuwa inajengwa kilometa tano tano inakuwa haileti tija, haina maana. Hebu ifike wakati sasa tuweke umakini katika barabara hii, ipewe pesa ya kutosha na ijengwe kwa mwenendo mzuri ili iweze kukamilika mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Kibena - Stop Lupembe, tunamshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kujengewa kilometa 51 na hivi sasa kilometa 25 kutoka Kibena - Nyombo imeshaanza kuandaliwa, iko mwishoni katika kuandaa tenda. Tunaomba lakini wafanye haraka haraka ili kusudi barabara hii iweze kukamilika. Barabara hii ni muhimu inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Morogoro, itafunguka kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Makete - Kitulo – Mbeya, kilometa 96, tulishapata mkandarasi lakini kinachosubiriwa ni advance payment ili mkandarasi huyu aweze kuanza kazi, kwa sababu ule mkataba ulishasainiwa tangu Desemba mwaka 2022. Tunaomba waanze haraka kule Makete mvua ni nyingi sana. Tuanze mapema kabla mvua za Novemba hazijaanza kunyesha, sasa hivi mvua zimetulia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Matamba – Kitulo, kilometa 51, barabara ya kimkakati ya kwenda kwenye Hifadhi ya Kitulo, barabara hii ni muhimu katika kufungua utalii wa Nyanda za Juu Kusini. Kuna Barabara ya Mlangali – Lupila – Ikonda, barabara hii tayari wameshajenga madaraja mazuri na barabara hii ni barabara ya kiusalama kutoka Mkoa wa Ruvuma, Njombe kwenda Mbeya. Tunaomba waiwekee umuhimu barabara hii ili iweze kujengwa katika kiwango cha lami na kuweza kuwasaidia sio lazima mtu anatoka Ruvuma anaenda Mbeya, aanze kuzunguka huku Njombe aende Makambako apite Igawa, ndio aende tena Mbeya, hapana barabara hii ni nzuri kwa shortcut ya kutoka Ruvuma kwenda…

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie katika suala la airport; Njombe tunahitaji airport ni muhimu sana, sisi ni wazalishaji wakubwa wa zao la parachichi. Kuna ndege ya mizigo inakuja na katika wazalishaji wakubwa wa horticulture ikiwepo parachichi, mbogamboga pamoja na maua ni Mkoa wa Njombe. Kuna umuhimu sana wa Kiwanja cha Ndege cha Njombe kukamilika ili kusudi tuweze kusafirisha bidhaa hizi na kumfikia mlaji zikiwa na ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)