Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, pia nimpongeze Waziri pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Mawaziri wote wawili kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sasa Mheshimiwa Waziri kwamba kuna mchakato ambao unaendelea kwenye Jimbo langu ni wa kulipa fidia ya wakazi wa Kata ya Kipawa, ambao sasa hivi imefikia sehemu nzuri nafikiri kwamba wameshaenda watu wa Wizara ya Miundombinu kufanya uhakiki na ninajua watakapomalizika hawa basi itaenda Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba hili jambo sasa lifikie mwisho na ninawashukuru sana katika miaka yote karibu miaka 30, ambayo mmeweza sasa hivi kufanya tathmini lakini pia na kuhakikishia kwamba hawa watu mnawalipa kwa mwaka huu na tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais. Wakazi wa Kata ya Kipawa Jimbo la Segerea wamenituma nije nitoe shukrani zao, kwanza kwa kuwafanyia tathmini mpya lakini kwa kuwaonesha kwamba watalipwa mwaka huu, nimshukuru sana Mkurugenzi wa Airport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo naomba pia nishukuru kwa mara ya kwanza barabara yetu ya Kinyerezi – Bonyokwa – Kimara sasa ipo kwenye bajeti. Barabara hii kwa muda mrefu sana tumeiongelea ambayo ni kilometa sita point ngapi hizo. Tumeiongelea kwa muda mrefu sana kwamba tunaomba hii barabara ijengwe, hii barabara ni muhimu sana, kwa sababu hii barabara imepita kwenye Majimbo matatu na hii barabara ikijengwa Mheshimiwa Waziri itatusaidia sana wakazi wa Segerea lakini pia Jimbo la Ubungo lakini pia Jimbo la Kibamba, kwa hiyo tunaomba kama mlivyoiweka kwenye bajeti tunaomba basi wananchi wetu waweze kuiona imeanza kujengwa ili na sisi sasa tujue kwamba tatizo la miundombinu katika haya Majimbo yetu matatu yanakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na madereva taxi wa airport terminal two. Terminal two pale kumekuwa na malalamiko mengi sana Mheshimiwa Waziri, madereva taxi wa terminal two. Jambo la kwanza wanacholalamikia ni kuhusiana na kwamba hawaruhusiwi kutoka terminal two kwenda terminal three. Kwa hiyo, tunaomba muwaruhusu waende terminal three kwa sababu baadhi ya hawa madereva taxi wa Jimbo la Segerea Mheshimiwa Waziri wengi wao wamechukua mikopo baada ya kuona terminal three inajengwa. Kwa hiyo, sasa hivi tunavyoendelea kuwazuia inawapa shida sana, tunaomba muwaruhusu na wenyewe waende terminal three waweze kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika terminal two pia Mheshimiwa Waziri tozo zimekuwa nyingi kwa hawa madereva taxi. Tozo zimekuwa nyingi wanakuwa wanalipa michango midogo midogo mingi, naomba kama itawezekana Mheshimiwa Waziri hawa watu waweze kupunguziwa hizi tozo, tozo ni nyingi sana na wanavyoendelea kuwekewa tozo nyingi, ndiyo wanafanya abiria waweze kuchukua taxi kwa bei ya ghali na wengine sasa kuchukua hizi ambazo zinaitwa Uber. Kwa hiyo, tunaomba sana muangalie hizo tozo pia kuangalia ni jinsi gani wanaweza wakaungana na wenzao terminal three. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri nililokuwa nataka kuongelea ni kuhusiana na barabara ya Banana – Kitunda. Mheshimiwa Waziri hii barabara ni barabara ambayo inapitisha magari 5,000 au 8,000 kwa siku. Hii ni barabara kubwa sana ni barabara ya TANROADS sasa hivi ina hali mbaya sana kwa sababu ni barabara ya lami, lami imekwisha mpaka jana Mwenyekiti wa eneo hilo anaomba grader apitishe juu ya lami kutokana na yale mashimo. Kwa hiyo, tunaomba sana hii barabara iangaliwe kwa sababu ndiyo barabara ambayo inaenda mpaka Jimbo la Ukonga tukizingatia kabisa Jimbo la Ukonga ndilo lenye wananchi wengi wanaokaa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hii barabara iangaliwe kwa sababu ndiyo barabara ambayo inaenda mpaka Jimbo la Ukonga, tukizingatia kabisa Jimbo la Ukonga ndilo lenye wananchi wengi wanaokaa kule. Kwa hiyo, ukifika pale, sehemu ambayo unaitwa Matembele Mheshimiwa Waziri sehemu ambayo unaweza kwenda kwa dakika mbili, inabidi uende kwa dakika 20 kunatokana na yale mashimo lakini pia kutokana na wingi wa magari. Kwa hiyo tunaomba sana mtuangalizie hii barabara kama mnaweza kuifanyia maintenance ili iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Mheshimiwa Waziri ni barabara ambayo ni ya Tabata - Kinyerezi. Hii barabara pia inapitisha magari mengi na ni barabara ya TANROADS, imezidiwa. Nimeona mmeweka ‘X’ kwenye baadhi ya nyumba, lakini sasa hatujajua wale wananchi wanauliza, kwamba pamoja na kuwekewa ‘X’ huu mradi utaanza lini? Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba mnapofikia kuwawekea wananchi ‘X’ tuwe tayari tumeshajua wanaondoka lini na wanalipwa lini? Kwa sababu mnapowawekea ‘X’ wanaanza sasa yale maswali, kwamba tumeshawekewa ‘X’, miradi yao mingi haiwezi kuendelea, wanaanza kujiandaa kwa kuondoka, lakini pia hamjui mkishaweka ‘X’ mnakuwa mmeshaondoka. Kwa hiyo, tunaomba sana sana, hii ‘X’ ikiwekwa tuwe tumeshakaa na wananchi tunawaambia mradi unaanza lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho ninalotaka kuliongelea ni kuhusiana na SGR. Namshukuru sana na ninawapongeza sana SGR kwa kazi kubwa wanayooifanya. SGR imepita kwenye jimbo langu, kwenye kata tatu; Kipawa, Vingunguti, Mnyamani, na Buguruni. Hizi sehemu zote Mheshimiwa Waziri zimezibwa. Hatukatai maendeleo, tunakubali kwamba maendeleo yawepo na yakija maendeleo ni lazima tupate usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa ambayo wanaifanya SGR, nawapongeza sana na nampongeza Mkurugenzi, lakini tunaomba katika hizi kata tatu tupatiwe sehemu moja ya kupitia. Kwa sababu sasa hivi mtu kama anatoka Mbezi inabidi azunguke aende mpaka Ukonga ndiyo aende Airport. Kwa hiyo, tungepatiwa sehemu moja ya kupita kwa sababu hii miradi, wataalam walisema itaisha baada ya miezi sita, lakini tulienda pale tukazunguka, miezi sita mpaka sasa hivi imeisha na mpaka sasa hivi watu bado wanaendelea kupata usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, wanafunzi wameshajitengenezea sehemu nyingine za hatari za kupita. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Mkurugenzi pamoja na Ma-engineer wa SGR waangalie katika hizi kata tatu, ni sehemu gani wanaweza wakaitengeneza kwa haraka ili sisi tuweze kupita hiyo sehemu? Kwa sababu sehemu zote zimezibwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)