Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nami fursa jioni ya leo niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii na hasa kuwasemea wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kuhusu miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuhakikisha anawahudumia Watanzania ipasavyo hususan katika eneo hili la ujenzi wa miundombinu ya usafiri na barabara na mambo mengine hapa nchini kwetu. Pia nimpongeze kwa ukamilishaji wa Ikulu ya nchi, na sasa tunasema nchi iko Dodoma. Kwa hiyo, naomba pia nitumie fursa hii kulisema hilo, kwa sababu ni jambo ambalo kwa miaka nenda rudi lilikuwa mishipa katika nchi yetu. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti, hotuba yake na utendaji wake mzuri pamoja na Manaibu wake wote wawili, Katibu Mkuu na Watendaji kwa ujumla, bila kumsahau Meneja wa TANROADS kule mkoani kwetu Singida, ni mtu very humble, msikivu na pia ni mfuatiliaji, ni mpokeaji wa simu zetu tunapokuwa na changamoto, maana yake sisi kule barabara zetu nyingi ni za vumbi, kwa hiyo, simu ya Meneja wa Mkoa ni iko ubavuni kila dakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama jioni ya leo, naomba nizungumzie jambo kubwa moja kwa muda wangu wote. Barabara inayotoka Singida Mjini inakwenda Njuki - Ilongero ambapo ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida, inakwenda Mtinko hadi Haydom. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara na vilevile ni kiungo pia cha ile barabara inayokwenda mpaka Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba angalau upembuzi yakinifu wa barabara hiyo umekamilika, lakini kwa masikitiko makubwa, nataka niseme tu wazi hapa kwamba mimi nitaondoka hapa nikiwa na machozi na majonzi makubwa nikiwarudishia wananchi wenzangu kilio kule kwamba hatujapata hata kilometa moja ya lami kwenye hii barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nieleze umuhimu wa hii barabara. Kwanza inakwenda kwenye Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ambapo kuna watumishi zaidi ya 3,000 walioko pale Makao Makuu ya Wilaya, wanaitumia hii barabara kila siku zaidi ya mara tatu, lakini wanapata shida kwa sababu ya ubovu, ina mashimo. Kama haitoshi, barabara hii inakwenda kwenye Hospitali ya Wilaya iliyoko pale Ilongero, lakini mpaka kesho hii barabara ni mbovu, ni mashimo matupu, watu wanapata shida. Kama haitoshi, barabara hii inawahudumia wananchi wanaokwenda Hospitali ya Haydom, ukanda wote huu wa kati; Mkalama, Jimboni kwangu Singida Kaskazini, Hanang, wote wanakwenda kwenye hii Hospitali ya Haydom, tunapata huduma kule, lakini ni mavumbi, mashimo. Sasa sijui tuongee lugha gani ili mtuelewe leo ndugu zangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inakwenda kwenye hospitali moja muhimu sana ya St. Carolus iliyopo pale Mtinko Mji Mdogo, lakini kila tukizungumza hapa hamtuelewi. Kama hiyo, haitoshi hii barabara iko kwenye ukanda wa uzalishaji mazao makubwa ya biashara na ya chakula, yanapita kwenye hii barabara. Vitunguu tunavyovisema hapa, vinapita kwenye hii barabara, alizeti inapita kwenye hii Barabara, mpaka na hawa kuku tunaowala hapa kila siku wanapita kwenye hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa cha kusikitisha zaidi, hii barabara ni ahadi ya tangu wakati wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Amekuja Mzee Mwinyi pale Ilongero akaahidi akasema tutaijenga kwa lami, amekuja Hayati Mkapa akaahidi hii Barabara, tena wanakujaga kuombea kura pale. Wanaombea kura hii Barabara. Amekuja Mzee Kikwete ameombea kura hii barabara, amekuja Hayati Dkt. John Magufuli, alisema kabisa tutakuja, tutaweka lami kwenye hii Barabara. Hata Rais wetu wa hivi sasa ambaye wakati huo alikuwa Makamu wa Rais, alikuja akaahidi akasema tutawawekea lami barabara hii. Kigugumizi kiko wapi? Shida ni nini kwenye hii barabara mnatutesa namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii barabara mwaka huu ionekane kwenye bajeti, tuweke lami hii barabara. Kama imeshindikana, tupeni basi kilometa hizi kumi ziende mpaka Makao Makuu ya Halmashauri, watumishi wanakimbia, wanakataa kukaa ofisini. Kila baada ya miezi miwili, anaripoti, wanaondoka, au nitoe machozi hapa ndiyo ninyi muone naongea ya kueleweka hapa? Nitoe machozi? Au nipande juu ya hii meza? Tatizo ni nini? Kwa nini hamtuelewi wananchi wa Singida Kaskazini tunapowaeleza kuhusu hii barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii barabara isipoonekana, nisipoona hata kilomita kumi angalau ifike kwenye Makao Makuu ya Halmashauri, Mheshimiwa Waziri nachukua mshahara wako, tutakutana na wananchi kule Singida Kaskazini. Utaenda kuwaeleza mwenyewe, kwa nini hutupi fedha kwenye hii barabara. Kama mna mpango mwingine labda mtuambie leo. Sisi tunalipa kodi, tena wananchi wa Singida Kaskazini ni waaminifu kweli kwenye Serikali hii, ni wapigakura waaminifu kweli kwa Serikali hii ya CCM, tunaomba mtupe hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba chonde chonde tupate lami kwenye hii barabara. Nami leo hii naomba iwe ni mara ya mwisho kuzungumzia barabara ya Singida – Ilongero - Haydom. Baada ya hapa naomba sana nisizungumze tena kuhusu hii barabara. Nimechoka, nimeuliza maswali ya msingi, maswali ya nyongeza, majibu yanakuja ya pinduapindua kila siku. This will be my last time to talk about this road. Naomba niongee Kinyaturu ndiyo mtanielewa, maana yake Kiswahili hamnielewi. Naomba niongee Kinyaturu hapa pengine Waziri utanielewa. Niongee Kinyaturu hapa? This will be my last time to talk about this road. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Singida Kaskazini wamechoka kudanganywa kuanzia, Hayati Nyerere! Sasa ninyi mnataka kuwafanya viongozi waliopita kuwa ni waongo! Marehemu ni waongo kweli! Ina maana viongozi wa nchi hii wakubwa ni waongo! Tekelezeni ahadi za viongozi wa kitaifa wanazoahidi wanapokuja kwenye maeneo yetu. Viongozi wanapokuja wanapoongea na wananchi, sisi ndio tunaachiwa mizigo tunaowawakilisha. Tunaambiwa ninyi mbona hamwaambii viongozi? Sisi ndio…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii barabara iwekwe lami. Mheshimiwa Waziri amenisikia, tena Waziri wa Fedha na wewe uko hapa, nakuomba sana brother, tusaidie hela, hela!

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Lete hela ile Barabara tuweke lami punda wapiti vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Wananchi wanateseka, lakini Mheshimiwa Waziri kesho Shilingi yako naondoka nayo.