Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya katika sekta hii ya ujenzi hasa ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara, miundombinu, umaliziaji wa madaraja makubwa kama Tanzanite na pia kule Kigongo, Busisi, unaweza kuona ujenzi wa treni ya umeme ambao unaendelea kutoka Dar es Salaam, Dodoma, Tabora - Mwaza, Tabora - Kigoma mpaka Katavi. Pia, nampongeza Waziri kwa kusimamia kwa ukaribu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi amemsikia vizuri sana mwenzangu Mheshimiwa Ighondo hapa, amezungumza juu ya barabara yake. Nafikiri Mheshimiwa Waziri yuko na sisi hapa, maana yake tunapozungumza hoja zetu na masikitiko makubwa ya wananchi, tunayawasilisha sisi wawakilishi wake hapa ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Choma Chankola kuja Ziba, Ziba - Nkinga, Nkinga kwenda Huge kupitia Ndala ni ahadi Waheshimiwa Marais waliopita, zimekuwepo na bado zinaendelea kuwepo. Kama alivyosema Mheshimiwa Ighondo, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alituahidi, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alituahidi, pia hata alipokuja Makamu wa Rais wakati ule na sasa ni Rais, aliahidi pia barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ya Choma – Ziba, Ziba - Nkinga siyo tu ni muhimu kwa uchumi wa eneo letu kwa Mkoa wa Tabora, pia ni barabara ambayo ndani yake kuna Hospitali kubwa ya Rufaa ya Nkinga, na Chuo cha walimu pale Ndala. Kwa hiyo, unaweza ukaona umuhimu wa barabara hii. Vile vile ni njia fupi sana ambayo inatumiwa na wakazi wengi kusafiri na kusafirisha mizigo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, ametuahidi mara nyingi, wakati mwingine anatuambia atatupatia kilometa kumi, anampigia simu na Mtendaji Mkuu, lakini hatuoni. Safari hii akatuambia atatuingizia fedha kwenye bajeti hii, hatuoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni mpaka tufanye nini? Mpaka turuke sarakasi kama wengine wanavyofanya? Haiwezekani! Tunamwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tufikirie na sisi, tupate hizo kilometa za barabara. Sisi tuna haki, tunalipa kodi kama wanavyolipa kodi watu wengine, tupeni hizo kilometa za barabara tuweze kupunguza adha za watu wetu katika maeneo yetu. Imekuwa ni ahadi, hasa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi barabara hii imo, 2025 na tunaamini tena 2025 - 2030 sijui tutaenda kuwaambia tena tutatengeneza, kwa sababu imeshakuwemo vipindi viwili vya Ilani ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, tunaomba sana ulipe uzito, isifike uchaguzi barabara hii haijaanza kufanya kazi. Litakuwa ni jambo ambalo siyo la kiungwana na tutakuwa hatujawatendea haki wananchi wa Jimbo la Manonga, Wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri sehemu nyingine ambayo napenda nichangie katika Wizara hii ya Uchukuzi, kumekuwepo na mamlaka nyingi za udhibiti ndani yake. Naweza nikazungumza kidogo Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi na hili liko dunia nzima, kuwepo kwa mamlaka nyingi za udhibiti kama zilivyo ada ya kawaida, na hili ni lengo la kuhakikisha kwamba tunadhibiti masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uchukuzi tunaweza kufanya maboresho katika hizi mamlaka, tukaunda angalau tuwe na tume, tukaunda idara. Napenda tutunge sheria ya udhibiti wa usafirishaji wa mizigo hatari. Najua ziko mamlaka nyingi zinazofuatilia kwa karibu hii mizigo hatari. Mfano, mizigo hatari hii tunaweza tukazungumza petrol. Petrol ni miongoni mwa mizigo hatari, petrol ni nishati, ina mamlaka ya EWURA; petrol ni kemikali ambayo inasimamiwa na Mamlaka GCLA; pia petrol inapokuja bandarini inakuwa chini ya mamlaka ya TASAC; pia petrol inapotembezwa ndani ya nchi, inapozungushwa inakuwa chini ya LATRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa napendekeza tuwe na chombo kimoja ambacho kinaweza kuwa na sheria na kanuni, kikawa na vitu vyote hivi kama vile ambavyo wenzetu Marekani wanayo Idara ya Usafirishaji inayo-deal na masuala haya ya usafirishaji. Inayo kodi kabisa na sheria imetungiwa. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kuiga kwa wenzetu siyo vibaya, hasa kwa mizigo hatari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mfano wa pili, tumeweza kuangalia usafirishaji wa virushi na vipeto. Hivi vifurushi na vipeto pia unaweza kuona vina mamlaka nyingi. Kwa mfano, vifurushi na vipeto viko TCRA, kama ukiwa unasafirisha mizigo hatari, iko GCLA. Pia kama inahusu masuala ya afya, iko Wizara ya Afya; na pia kama inasambazwa ndani ya nchi, iko LATRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba tuhakikishe kwamba ili hii sekta ya uchukuzi iwe na mfumo ambao unasimamiwa vizuri kuondoa hii mikanganyiko na hatari nyingi ambazo inaweza kusababishwa, na kuondoa kudumaza kwa sekta yenyewe, maana yake sekta ya usafirishaji ikidumaa department nyingine zinadumaa zaidi. Kwa hiyo, nashauri kwamba tutunge Sheria ya Kudhibiti Usafirishaji wa vifurushi na vipeto kwa njia ya barabara, kutoka TCRA na hii isimamiwe na LATRA.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Seif Gulamali.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Ahsante sana.