Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. KABWE Z.R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia na nina maeneo makuu mawili tu maeneo mengine ni madogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza jana Mheshimiwa Chenge alitu-challenge hapa tulete vifungu gani vya sheria ambavyo vimekiukwa katika utaratibu wa bajeti. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kwamba mwezi Februari Bunge lilikaa kama Kamati ya Mipango na kupitisha ceiling za bajeti na bajeti guidelines. Katika bajeti guidelines ambazo tulipitisha hapa mwezi Julai thamani ya bajeti ilikuwa ni shilingi trilioni 23 lakini bajeti ambayo tunaijadili sasa hivi ni shilingi trilioni 29 na Bunge halijakaa wakati mwingine wowote ule kama Kamati ya Mipango na kuweza kurekebisha hizo bajeti guidelines.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge watazame Sheria ya Bajeti, Na. 11 ya mwaka 2015, vifungu vya nane (8), tisa (9) na 19 ambavyo vyote vinaeleza ni utaratibu gani ambao unapaswa kufuatwa ili Bunge liweze kujadili bajeti kwa mujibu wa sheria. Vinginevyo hapo tutajadiliana mpaka mwisho, tutafika mwisho kumbe tumevunja sheria moja kwa moja. Kwa hiyo, naomba jambo hilo liweze kutazamwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nichangie ni kuhusu Wizara ya TAMISEMI, eneo la kodi za majengo. Kama ambavyo mzungumzaji aliyepita amezungumza na Kamati imesema kwamba sasa hivi Serikali kupitia TRA inaenda kukusanya Kodi ya Majengo, lakini huko nyuma tulijaribu kwa Manispaa za Dar es Salaam kuwapa TRA, lakini haikuwa na mafanikio ambayo yalikuwa yanafikiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Manispaa zetu zikanyang‟anywa mamlaka ya kukusanya kodi zake yenyewe. Kama kuna jambo ambalo Serikali inaliona ni makosa yaani labda kodi inayokusanywa ni kidogo ni vizuri Manispaa zikajengewa uwezo ziweze kuzikusanya kodi hizi, kuwanyang‟anya chanzo hiki cha mapato itakuwa ni kuua Manispaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nifahamu na Waziri atufahamishe, sasa hivi kuna Manispaa nyingi sana ambazo zinaongozwa na Vyama vya Upinzani, huu ni mkakati wa kuziua Manispaa hizi zisifanye kazi yake au ni nia njema? Naomba nipate ufafanuzi kuhusu jambo hili. Maana yake Manispaa yangu ya Kigoma Mjini iko chini ya Upinzani, je, mnataka kutunyang‟anya 50 percent ya mapato yetu na fedha hizi zisirudi? Manispaa za Dar es Salaam, Iringa, Mbeya na kadhalika, zote ziko chini ya Upinzani, lengo lenu ni kuzinyima zisifanye kazi zisionyeshe kwamba zinaweza zikatenda tofauti na Manispaa zinazoongozwa na Chama cha Mapinduzi? Naomba kupata ufafanuzi wa maeneo kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo sasa hivi sehemu yake iko mahakamani na sitoligusia kwa sababu ni mambo ambayo yako mahakamani hatupaswi kuyazungumzia. Mwaka 2013, Serikali ilikopa fedha zaidi ya dola za Kimarekani milioni 600, kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, kupitia hatifungani ambayo wataalam wote duniani wanasema ilikuwa ni ghali na kimsingi tunapaswa kuwa tumeanza kuilipa kuanzia mwezi Februari mwaka huu. Itakapofika mwaka 2020, hatifungani hii itakuwa tumepaswa kuwa tumeilipa yote na kiwango cha fedha kutokana na riba ambayo tumepewa tutakachoenda kulipa ni dola za Kimarekani milioni 897 zaidi ya shilingi trilioni mbili ambazo ndiyo nchi italipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatifungani hii imeonekana inarushwa, waliopelekwa mahakamani ni waliowezesha rushwa, mtoa rushwa hayupo mahakamani? Mpokea rushwa hayupo Mahakamani? Kwa sababu waliopata biashara hii ni Standard Bank ya Uingereza. Tungependa kuona TAKUKURU wakiishtaki Standard Bank ya Uingereza na kuna maslahi ya Taifa katika Jambo hili . Ukiishtaki benki hii unapata faida mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kwanza ikigundulika walitoa rushwa, kwa ajili ya kupata biashara walioifanya Tanzania, Tanzania itafutiwa deni lote la shilingi trilioni mbili. Faida ya pili itakuwa ni salamu kwa makampuni mengine ya Kimataifa kutokuja kuhonga nchini ili kupata biashara. Sasa maslahi ya TAKUKURU ni nini? Maslahi ya TAKUKURU ni kupata picha za watu wamebeba ndoo wamepelekwa mahakamani au maslahi ya TAKUKURU ni nchi kuepuka deni kubwa kiasi hiki. Kwa hiyo, naomba Waziri atakapokuja kutueleza hapa alione hili kwa mapana yake tuna deni la trilioni mbili ambalo tukiweza kuwafikisha mahakamani Standard Bank, tukathibitisha waliohonga ili kupata biashara ile, linafutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyozunguma na nitawasilisha mezani nyaraka kadhaa, mojawapo ni barua ya Watanzania 2000 duniani kote wameandika kwa taasisi ya Serious Proud Office ya Uingereza, kutaka kesi ile ifunguliwe upya. Hawa ni Watanzania wenye uzalendo wako nje wameandika kutaka kesi ile ifunguliwe upya, TAKUKURU haifanyi chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yuko hapa, bahati nzuri amekuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu muda mrefu atazame hili jambo, lina maslahi mapana ya Taifa. Msifurahi tu kukamata watu wa Dola milioni sita, kuna trilioni mbili za kuokoa na tayari kuna Watanzania wameshatuanzishia hili? Nawaomba Serikali iungane Mkono na hawa Watanzania, TAKUKURU ianze uchunguzi dhidi ya benki hii ya Uingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana ndani ya Ofisi ya TAKUKURU; kuna washauri wa kutoka Uingereza wanaoishauri TAKUKURU kuhusu kesi hiyo. Sasa mnaweza mkaona namna gani ambavyo mgongano wa maslahi unaingia katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jambo hili litazamwe na naamini kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU yuko hapa, hili ni jambo ambalo linaweza likaiokoa nchi na likatuma salamu na tukawa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika; ambayo inatuma salamu kwa makampuni ya Kimataifa kwamba msije kuhonga watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuvutavuta miguu kwa Serikali, naomba Bunge lichukue jukumu hili. Sababu Serikali inaweza ikafanya, lakini ikaonekana Serikali za nchi maskini hizi ukizikopa hazilipi. Bunge lichukue hili jukumu. Kanuni ya 120(2) ya Bunge, naomba tuitumie Kanuni hiyo kuomba Bunge hili mara baada ya hoja hii kwisha; tuunde Kamati Teule kwenda kuchunguza jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia nchi itapata faida kubwa sana; na tutakuwa na sifa Kimataifa kuzuia makampuni makubwa ya Kimataifa kuja kuhongahonga watu wetu, kupata biashara; kama hii biashara ambayo ilifanyika na tutaokoa trilioni mbili ya Pato la Taifa; kwa hiyo naomba jambo hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kulikuwa na uchunguzi unaoendelea kuhusu IPTL Tegeta ESCROW. Taarifa zote ambazo TAKUKURU wanazitoa ya kupeleka watu Mahakamani, hili jambo haliguswi; kulikuwa kuna maazimio ya Bunge hapa kwamba suala hili lichunguzwe na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alishatangazia umma uchunguzi umekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini watu waliohusika na Tegeta ESCROW hawajafikishwa mahakamani mpaka sasa? Kinachoogopwa ni nini? Ni kwamba kuna majipu yanaonekana, mengine ya mgongoni hayaonekani, hamwezi kuyatumbua? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo tunapoteza bilioni nane kila mwezi tunailipa kampuni ya matapeli; ambayo iliiba fedha Benki Kuu; wakatumia fedha zile kuchukua mkopo wanazalisha umeme eight billion every month tunawalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini TAKUKURU hawajawafikisha watu hawa mahakamani mpaka sasa? Naomba jambo hili pia liweze kuangaliwa ili tuweze kuhakikisha kwamba nchi inapata faida inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale ambayo sijayasema, nitayawasilisha kama hati za kuwasilisha mezani ili hatua stahili ziweze kuchukuliwa. Nashukuru sana.