Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu. Kilichonisimamisha hapa ni kushukuru. Kwa kweli katika watu ambao wanatakiwa kushukuru sana na mimi ni miongoni mwao baada ya kuiona Barabara yangu ya Masasi – Nachingwea – Liwale na hii Barabara ya Nangurukuru – Liwale, kilomita 50 niseme ahsante sana, kwani sisi tumefundishwa kwamba asiyejua kumshukuru mtu mwenzie basi hata mwenyezi Mungu hawezi kumshukuru. Hivyo, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake wote wawili na watendaji wote wa Wizara hii, kwa kweli wamenitendea haki mwaka huu kwenye bajeti, nawashukuru sana. Kama ilivyo ada wanasema kushukuru ni kuomba tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli mama anavyoamua kuifungua nchi hii, niwaombe sana Watanzania na wasaidizi wake hasa wasaidizi wake, tumsaidie mama. Mama anakwenda kujenga SGR, ananunua ndege, anajenga bandari ya uvuvi, kama Bandari yetu hii ya Dar es salaam itabaki vile ilivyo, tutakuwa hatuja mtendea haki. Tuna shida gani? Tumesomesha Engineers, Wanasheria, tunavutavuta miguu kwenda kuiboresha bandari yetu kwa sababu ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana sambamba na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. Si tumesema tuna PPP hapa jamani, sasa tunavuta mguu kwa nini? Hivyo SGR tumeijenga kutoka Dar es Salaam mpaka Kigoma. Kama bandari yenyewe ndiyo ile ambayo kwa watu wengine wanaita mwalo, kule Mwanza wanaitwa mwalo kama mwalo tu hivi. Niwaombe sana tusivute miguu, kwenye hili watendaji wa Serikali wanaomsaidia Mama tusivute mguu, twende PPP tuboreshe Bandari yetu ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kuna barabara wanayoijenga hii ya Masasi kwenda Mtwara wanaendelea kuiboresha na kuitengeneza, lakini barabara ile wasipojenga hii reli ya kutoka Mbambabay kwenda Mtwara barabara hii itaendelea kuteseka, kwa sababu kule makaa ya mawe yanayopita kwenye hiyo barabara wanakwenda kuichakaza hii Barabara. Nawaomba sana, sana hii reli ya Mtwara Mbambabay ijengwe, ni reli imetajwa muda mrefu imezungumzwa sana, nawaomba kwenye bajeti hii, hii reli iende ikajengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile asubuhi hapa Mheshimiwa Mhata ameuliza swali muhimu sana. Kuna barabara inaunganisha wilaya nne, barabara hii inatoka Mangaka – Nachingwea mpaka Liwale, barabara hii inatoka Tunduru inaunganisha Wilaya ya Tunduru, Wilaya ya Nanyumbu, Wilaya ya Nachingwea mpaka Wilaya ya Liwale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye randama hapa au kwenye bajeti wameandika kuna upembuzi yakinifu wa barabara inayotoka Liwale kuelekea Mahenge. Barabara hii kiunganisho chake kikubwa ni barabara inayotoka hapa Tunduru, Nanyumbu. Barabara hii mpaka sasa hivi bado ina hudumiwa na TARURA. Niwaombe sana, sisi kwenye RCC yetu Mkoa wa Lindi tulishaiombea hii barabara iingie TANROADS, muda mrefu sana. Sasa umefika wakati naomba hii barabara itoke TARURA iende TANROADS ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee hapo hapo kwenye TAZARA imezungumzwa hapa tunaenda kuboresha TAZARA. Sambamba na TAZARA na hizo meli za uvuvi nilizozungumza, ni lazima tuhakikishe narudia tena wasaidizi wanaomsaidia Mheshimiwa Rais, Rais ameamua kuifungua nchi hii kiuchumi, hizi ni fursa ambazo tunataka kuzitumia, naomba tumsaidie kikweli kweli kwa kuiboresha Bandari yetu ya Dar es salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo tu machache, yanatosha kwa leo. Nashukuru sana. (Makofi)