Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata muda, naomba leo niongee kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kusema ukweli; hakuna awamu ambayo imejenga barabara katika nchi yetu kuzidi awamu ya sita. Hakuna mahali ambapo sasa hivi hapajengwi barabara. Ukienda mijini barabara zinajengwa, ukienda vijjijini TARURA wanafanya kazi ya kujenga barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nichukue nafasi ni kwa mara nyingine niishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Sita, na niipongeze kwa kujenga barabara nchi nzima. Nimalizie kwa kusema kwamba Tanzania iko busy sana sasa hivi kwa miradi ya ujenzi wa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, nirudi kwa Mheshimiwa Waziri Mbarawa. Hii Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, hii ni Wizara pana sana, ni Wizara ambayo ina shughuli nyingi sana. Amesema Mheshimiwa Mbunge jana pale, hii Wizara ina taasisi 22. Tuchukue taasisi moja tu ambayo nashukuru Waheshimiwa Wabunge mmiongea sana; taasisi ya TPA (bandari).

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ni lango kuu la uchumi, na kweli kabisa; mimi niwapongeze Waheshimiwa Wabunge, mko very positive na kupata wawekezaji wa kusaidiana na Serikali upande wa bandari. Iwapo ile bandari tutaitumia vizuri, Serikali itaangalia vizuri na sisi Wabunge tukaridhia tunakwenda kukomboka, kukombolewa nchi yetu na Bandari ya Dar es salaam pamoja na bandari zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi huwa na-google sana na kuangalia, ukienda India tukubali Waheshimiwa Wabunge kwamba Wahindi ni wachumi wazuri; wenzetu India wametengeneza Wizara maalum ya bandari ambayo inaitwa Ministry of Ports Shipping and Water Ways. Wametengeneza Wizara maalum kwa ajili ya bandari kwa sababu wanajua uchumi uko kwenye bandari. Mimi nimesema tu sijasema zaidi ya hapo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudi jimboni kwangu sasa. Mheshimiwa Waziri nakupongeza tena, nimesikiliza hotuba yako vizuri mno niende kwenye kifungu chako cha namba 106 ulipoongelea barabara yangu ya Mkomazi – Kisiwani – Same. Naomba nikushukuru, si mimi wananchi wa Jimbo la Same Mashariki wamenituma, Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana, Waziri Mbarawa tunakushukuru sana. Tunakupongeza kwa sababu hii Serikali ya awamu ya sita imesikiliza kilio cha wananchi wa Jimbo la Same Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Same Mashariki silisemei kwa ukubwa, kwa ukorofi, tarafa mbili zote ziko milimani, narudia zinalima Tangawizi asilimia 72 ya tangawizi ya nchi nzima. Tarafa ya chini, Tarafa ya Ndungu inalima Mpunga, inalima inalisha Kilimanjaro inalisha Tanga. Lakini tulikuwa tunaponzwa na barabara ya Mkomazi – Kisiwani – Same Mheshimiwa Waziri tunakushukuru wananchi wamenituma nikushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fungu la 116 limeniambai kwamba barabara ya Mkomazi - Kisiwani - Same sasa imepata wakandarasi wawili na inajengwa kwa kiwango cha lami kilometa zote 97. Mkandarasi wa kwanza anaanza Same – Kisiwani – Mroyo kilometa 56.83 Mheshimiwa Waziri tunakushukuru sana, mkandarasi wa pili anaanzia Ndungu – Mkomazi kilometa 36. Mikataba hii itasainiwa mwezi wa sita, ambao ni mwezi ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie kabisa Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wameshona nguo, wanaume wameshona suti, wanawake wameshona vitenge; tutakuwepo kwa wingi sana mwezi wa sita utakapo kuja kwa ajili ya kusaini mikataba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi wananchi wa Same mashariki huu ni ukombozi mkubwa. Jimbo hili lilizaliwa mwaka 1995, Mbunge wa kwanza alikuwa ni Daniel Yona, alizungumza akiwa Waziri, huku akiwa Waziri alifanya kazi kuhusu barabara hii. Nikaingia mimi kwa kipindi cha miaka kumi kila wakati nazungumzia barabara hii. Akaingia mdada pale alipoingia naye akazungumza, na mimi nikaingia saa hiyohiyo nikawa Mbunge wa kuteuliwa nikasimama imara nikizungumzia barabara hii, nimerudi sasa nazungumzia barabara hii; lakini awamu ya sita tunaishukuru imetusikia imetupa barabara hii, ahsante sana, ninaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza kwa uchungu sana kuhusu Dar es salaam. Nazungumza kwa uchungu kuhusu Dar es salaam na ninaomba Serikali mnisikilize vizuri. Dar es salaam yalikuwa ndiyo makao makuu ya nchi yetu tangu tumeitwa nchi. Awamu ya tano ndiyo imekuwenda kufanya kimatendo kuhamisha makao makuu kutoka Dar es salaam kuja Dodoma tunashukuru sana. Lakini, Dar es salaam inajengwa barabara nzuri, lakini Dar es salaam inatatizo kubwa mvua zinaponyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali inisikilize, siitumi, inisikilize. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aandike historia, aandike historia ya kuitoa Dar es salaam kwenye matatizo ya maji wakati wa mvua. Kwa nini nasema hivyo? Sisi tuna ma- engineer wengi sana. Ukienda TANROADS yenyewe ina ma- engineer 306 walioko kwenye ajira za kudumu. TANROADS hiyo ina Ma-engineer 238 walioko kwenye ajira za mikataba. Hivi wananshindwaje hawa Ma-engineer kukaa chini wakatumia Elimu yao wakaondoa lile tatizo lililopo Mkoa wa Dar es salaam?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Dodoma ni makao makuu, lakini hata kama Dodoma ni makao makuu, Dar es salaam itaendelea kuwa mji mkuu wa kibiashara na Tanzania tukubaliane kwamba Dar es salaam bado itaendelea kuwa ni jiji ambalo linavuta watu na linapendeza mpaka mwisho wa maisha ya kuishi huku duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naiomba Serikali kipindi hiki cha Mama Samia Suluhu Hassan asimalize kipindi chake hiki cha kwanza kabla hajatatua tatizo la maji yanayotuama, yanayojaa na kukosa njia kiasi kwamba wananchi wanashindwa kuendesha magari mimi juzi alipokuja Makamu wa Rais nilishtuka nikasema atashindwa kupita akitoka airport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona nimegongewa kengele lakini naiomba Serikali itumie Ma-engineer wote tulionao kipindi hiki hiki cha Mama Samia cha kwanza iondoe matatizo ya Mkoa wa Dar es Salaam. Ma-engineer tumieni elimu yenu Mheshimiwa Mbarawa una ma-engineer wengi kaeni muangalie hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.