Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumbawanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea. Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na Watanzania wote wanajua na wanaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu Ndugu yangu, Kaka yangu Mheshimiwa Prof. Mbarawa kwa kazi kubwa anayoifanya, ama kweli Wizara hii ni ngumu lakini amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba maendeleo yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii tena kwa niaba ya Wanarukwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. Nimekuwa Bungeni nikapambana sana kuhusiana na Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga Mjini. Mwaka jana nilisimama hapa nikasema endapo hatutaweza kufanikiwa kujenga uwanja wa ndege kwa mwaka huu nilitaka niiombe Serikali na niliombe Bunge lako litoe hiyo bajeti kwa sababu tumekuwa tukiipigania mwaka wa saba leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tu Mheshimiwa Waziri alinipigia simu na hatimaye ombi letu limekubaliwa tukaenda kusaini mkataba na wananchi wakaona na wakafurahi sana na mwezi ujao Mkandarasi atakuwa site anaanza kazi. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana Kaka yangu kwa kazi kubwa uliyoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba niongelee maeneo matatu au manne hivi. Barabara zetu za Mkoa wa Rukwa, tumetembelea barabara mbili ya kutoka Matai kwenda Kasesha na ya kutoka Ntendo kwenda Muzi. Mheshimiwa Waziri nikuombe, Rukwa tunajivunia sana kilimo lakini Rukwa tuko pembezoni mwa Lake Tanganyika, tunapakana na Congo, Burundi na Zambia. Tumejenga bandari nzuri sana, tumejenga bandari ya Kipili, tumejenga bandari ya Kasanga, tumejenga bandari ya Karema na maeneo mengine kwenye Mikoa mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya barabara tukuombe sana, kuna barabara ya kutoka Namanyere kwenda Kirando inaelekea Kipili. Mheshimiwa Waziri tumewekeza vya kutosha lakini tusipojenga barabara zile bandari zitakuwa tumewekeza kama kwa kazi bure. Sasa nikuombe sana kwenye bajeti ya mwaka huu barabara ya kutoka Namanyere kwenda Kipili kwa kweli tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Lyazumbi kwenda Kabwe ambako na kwenyewe tumejenga bandari kubwa sana na yenyewe tujenge barabara kwa kiwango cha lami ili kuwe na tija ya zile bandari tulizozijenga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana lengo la kujenga zile bandari ni kusafirisha mizigo kwenda Congo, Burundi na kwenda Zambia, tusipojenga barabara za lami, bandari zile zitakuwa ni kazi bure. Kwa hiyo, tukuombe sana barabara zipitike na bahati nzuri Kamati tulikwenda kutembelea tukaona kwa kweli kuna kila haja ya kujenga barabara zile. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kwenye barabara naomba niishauri Wizara kwamba tumekuwa na barabara nyingi, tumekuwa na Wakandarasi wengi lakini wazawa hawa ambao tunao hawanufaiki mara nyingi na hii miradi ya barabara za kiwango cha lami kutokana na masharti magumu ambayo Mkandarasi wa kawaida kuweza kujenga hizi barabara kwa kweli wameshindwa. Nikuombe Mheshimiwa Waziri rekebisheni masharti ni makubwa mno na mazito. Unapomwambia mkandarasi wa kawaida au mzawa awe na turnover ya shilingi bilioni tano anaitoa wapi? Kwa mradi upi alioupata? Kwa hiyo, nikuombe barabara hizi tukipata wazawa wetu wakijenga, maendeleo yatabaki ndani ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi wa nje wengi wakipata barabara hizi mara nyingi sana wanakwenda kuwekeza huko kwao. Kwa hiyo tuangalie sana na uzawa, tupunguze masharti kidogo angalu hata wa kilometa 10, 15 basi wakandarasi wa hapa nchini wapewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta Mheshimiwa Waziri barabara ya kilometa 15 ama 20 masharti yanayowekwa hakuna mzawa ambaye ameweza kupata kujenga barabara. Kwa hiyo, nikuombe sana katika hili unapokuja utusaidie na wazawa wakandarasi waweze kupata kazi ili waweze kunufaika na wakinufaika maendeleo yanabaki nchini kwetu, wakinufaika watajenga kama ni hoteli zitabaki kwetu, wakinufaika kama watajenga maeneo mengine ya maendeleo lakini yote yatabaki kwetu. Kwa hiyo, kwenye hizi kazi ndogo ndogo, kilometa 10, 15 basi at least Watanzania waweze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza unakuta kuna kampuni inajenga barabara zaidi ya kilometa 100, kilometa 200 bado ukitangaza tender ya kilometa tano unamuona na huyu bwana naye anakuja kuiomba hiyo tano. Kwa hiyo, ni vigumu sana kwa Mkandarasi wa Kitanzania kupata kazi. Kwa hiyo nikuombe sana katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kumekuwa na kilio Lake Tanganyika tumejenga kweli bandari lakini cha kushangaza hatuna hata meli moja inayotembea, hakuna! Ukienda kwenye Shirika la Meli wakakutembeza kule Kigoma utakuta kuna meli moja wanaisifia sana tumeikarabati, meli yenyewe ya MV Sangara, meli ya mafuta! Leo hii tumeona bora mafuta kuliko wananchi waweze kupata huduma ya usafiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanakufa sana, maboti yanazama sana, mizigo inazama. Kwa hiyo nikuombe, Meli ile ya MV Liemba nimekuwa nikipambana sana ndani ya Bunge kuhakikisha kwamba ile meli inafufuliwa lakini mpaka leo. Mwaka jana tumepitisha bajeti, mwaka juzi tumepitisha bajeti na mwaka huu tunaipitisha tena bajeti. Sasa Mheshimiwa Waziri mimi nakuamini sana, tuangalie sana wananchi tunaoishi pembezoni mwa Lake Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja ya kujenga meli ya tani 2,000, hoja ni nzuri lakini inawezekana tunaifikiria hii tani 2,000 labda kwa miaka mingine 50 ijayo. Kwa miaka hii ya sasa hivi tuhakikishe kwamba meli hii ya tani 2,000 tuigawe iwe meli ya tani elfu moja moja ziwe zinapishana. Ukijenga meli moja ukawa unasubiria mzigo wa kwenda Congo, kuna watu hapa wanafikiria Kalemi ni Mji mkubwa kama Dar es Salaam siyo kweli! Kwa hiyo tunajikuta meli ya tani 2,000 itakaa inasubiria watu wapate mzigo, wajichange, wajichangae waende kuusafirisha. Hiyo inakuwa ni ngumu zaidi. Kwa hiyo, ninakuomba sana tani 2,000 mimi siungi mkono lakini nimekuwa nikikushauri mara nyingi na umekuwa ukikubali ushauri wangu naomba katika hili tujenge meli za tani elfu moja moja ili ziwe zinaenda kwa wakati na kwa muda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho naomba nikupongezeni sana Wizara ya Ujenzi.
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Hilaly kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa.
TAARIFA
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa taarifa mzungumzaji anayezungumza kwamba, ni kweli hii meli ya tani 2,000 ni nia njema ya Serikali kweli lakini tani elfu moja moja ni nzuri hasa kwa wafanyabiashara ambao utaratibu wakati mwingine kukodi meli ni ngumu kukodi meli ya tani 2,000 lakini tani 1,000 ni rahisi. Kwa hiyo nampa taarifa mzungumzaji.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Aeshi taarifa unaipokea?
MHE. AESHI K. HILALY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa na kwa kuongezea tu tuna mfano Congo wamejenga meli ya tani 2,000 inaitwa MV Amani, ile meli haisafiri! Kwa hiyo tuige tuone kule Congo ile meli waliyoiunda inatembea? Leo hii ina mwaka wa pili au wa tatu nafikiri imeenda trip tatu au nne. Sasa kama wenzetu wamejenga meli ya tani 2,000 sisi tujenge meli za tani elfu moja moja ambazo zitakuwa zinabeba mzigo kirahisi na zinaweza kufikisha mzigo na wafanyabiashara wakafanye biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze sana Wizara ya Ujenzi lakini niipongeze TRC kwa kazi kubwa wanayoifanya. Tumeenda kutembelea miradi, tumetembelea SGR kwa kweli inajengwa kwa kiwango kinachotakiwa. Naomba niwe mkweli nisiwe mnafiki katika hili. Tumetembelea lot namba moja na namba mbili, kwa kweli kuna watu ambao hawajawahi kufika kwenda kuangalia. Tunaweza kuwa tunafikiria kuna jambo linajengwa siyo la uhalisia lakini kimsingi kwa kweli Serikali imefanya kazi kubwa. Nikuombe sasa Mheshimiwa Waziri mabehewa ambayo tumeambiwa yapo njiani basi yafike ili na wananchi waweze kuona sasa kile ambacho tulikuwa tumekusudia.
Ninaamini wananchi watajenga imani na mimi niseme nisiwe mchoyo wa fadhila, nawapongezeni wote Wizara ya Ujenzi na taasisi zote. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya, lakini nimuombee kila la kheri awe na afya njema aweze kutuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)