Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuiongoza nchi yetu lakini kipekee kwa nia yake ya dhati kabisa ya kuifungua nchi yetu kwa miradi mikubwa ya barabara, reli, ndege wote tunaona jinsi gani nchi yetu inakwenda kufunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Waziri Profesa Mbarawa na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Watendaji wote wa mashirika yote, Bandari, TASAC, Shirika la Ndege wote vijana wanachapa kazi, wanafanya vizuri tunaona jinsi gani wanaweza kuyaendesha hayo mashirika na tunaona jinsi gani Tanzania inakwenda kubadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mchoyo wa fadhila, nimshukuru Kaka yetu Engineer Choma, Engineer wa TANROADS Mkoa wa Kigoma anachapa kazi vizuri katika Mkoa wetu wa Kigoma, anatupatia ushirikiano wa kutosha, tunaona jinsi miradi ya Mkoa wa Kigoma inavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Muhambwe nasimama hapa leo kutoa shukurani nyingi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo miradi ya barabara inaendelea katika Jimbo la Muhambwe. Tunao mradi wa Barabara wa Mvugwe – Nduta Junction kilometa 59 ambao mwaka huu umefikia asilimia 66, mwaka jana ulikuwa asilimia 25, tunaipongeza Serikali inafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo barabara ya Nduta Junction - Kibondo Mjini kilometa 25.9 mwaka jana ilikuwa asilimia 44 na mwaka huu sasa hivi wako asilimia 58. Tumesaini mkataba wa ujenzi wa barabara kutoka Kibondo Mjini kwenda Mabamba kilometa 47.9 kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 69. Hizi ni jitihada za dhati kabisa za Serikali za kuendelea kuwaunganisha wananchi wake kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee tunaenda kufaidika kabisa maana barabara hii inakwenda kuboresha soko la ujirani mwema pale katika Kijiji cha Mkarazi ambacho tunafanya biashara na ujirani mwema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo ya miradi hii inayoendelea katika Jimbo la Muhambwe, bado ziko changamoto ndogondogo. Kwanza kabisa barabara hizi zitategemewa kuisha mwaka huu Desemba na kama tuko kwenye asilimia 66 ni ukweli usiopingika kwamba tunatakiwa kuongeza kasi. Wananchi wa Muhambwe wamenituma wanaomba kasi ya ujenzi wa hizi barabara ili tuweze ku-meet target. Ziishe kwa wakati kwa sababu hili ni Jimbo ambalo lilikuwa halijaunganishwa kwa lami bado. Kwa hiyo, nawaomba watendaji kwa nia ya dhati kabisa Mheshimiwa Rais ya kutuunganisha na lami basi kazi ifanyike kweli kweli ili barabara hizi ziweze kuisha kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hizi pia zina miradi ya CSR ambayo miradi hii ilitegemewa kujengwa Kibondo, Kasulu na Buhigwe. Barabara zimefikia asilimia 66 lakini miradi hii bado haijaanza. Ninajua michakato inaendelea, niiombe Serikali miradi hii ya CSR ambayo inategemewa kujengwa katika Majimbo haya matatu Kibondo, Kasulu na Buhigwe basi nayo iende kwa kasi ili barabara zitatakapoisha na miradi hii pia iwe imekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kipande cha barabara ambacho Wabunge wa Mkoa wa Kigoma tumekuwa tukikisemea sana, Uvinza – Malagarasi kilometa 51. Ukipita kwenye ile barabara ni changamoto yaani ukimaliza pale lazima upeleke gari yako service. Kipande kile ni kibaya sana na kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri kipo asilimia 26 kwa hiyo ni ukweli usiopingika kwamba bado kiko nyuma sana. Tunaomba Serikali itusaidie sisi Wabunge wa Mkoa wa Kigoma barabara hiyo inatupa changamoto siyo nzuri, haipitiki tunaomba kasi iongezeke. Kama kuna changamoto kwenye kile kipande basi zifanyiwe kazi ili kipande kile nacho kiweze kuisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi hii ya lami bado ziko barabara za TANROADS ambazo tunahitaji ziwe kwenye kiwango cha lami ambapo kwa sababu ya mvua hizi zinazonyesha barabara hizi hazipitiki. Hii ni barabara ya Kitaha na Nyange ni mbaya sana haipitiki, iko chini ya TANROADS, hii ni Barabara ya Kifura – Nyange haipitiki, Barabara ya Bunyambwe – Nyange haipitiki. Nimuombe Engineer Kaka yangu Engineer Choma ninamuamini sana anaweza. Tunamuomba kule Kibondo atusaidie kutengeneza hizi barabara kwa kiwango cha changarawe na kipekee niombe kusisitiza kwamba barabara hizi zinavyotengenezwa basi ziwekwe mifereji kwa sababu mvua imekuwa chanzo kubwa cha kufanya ziharibike sana. Naamini zitatekelezeka kwa sababu TANROADS wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wote wamesema Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, Rukwa na Katavi kwa kweli tunaipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo wamejenga MT Sangara na tumeona ipo asilimia 90 meli ambayo itaenda kubeba mafuta. Hii Serikali imelenga kufanya biashara lakini Serikali kama Serikali mbali na biashara lengo kuu la Serikali kwanza ni kuwahudumia wananchi, ustawi wa wananchi wake. Jamani wananchi wa Mkoa wa Kigoma, Wananchi wa Rukwa na Katavi tunaomba meli ya abiria na mizigo midogo midogo ili wananchi wetu waweze kusafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona imepita bajeti hapa ya kutengeneza MV Liemba, MV Mwongozo, tunaomba kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameweka commitment kwamba itaanza mwezi wa sita na mwezi wa nane itakuwa imeisha. Tunaomba mchakato huu uende haraka sana. Kwa nini? Mwenzangu amesema tumejenga bandari, Kigoma tumejenga, tumejenga Karema, tumejenga Kabwe, Kipili, Kasanga. Kama hatuna meli tulitaka ku-achieve nini kwa ajili ya hizi bandari? Tunajenga SGR inakwenda kupeleka watu kule, bila kuwa na meli tunaenda ku-achieve nini? Tunaiomba Serikali ituangalie Wananchi wa Mkoa wa Kigoma, Katavi na Rukwa ili tuweze kufunguka kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema sana kuhusu Shirika la Ndege. Ni ukweli usiopingika kwamba shirika hili linafanya kazi sana. Tumeona lilikotoka na lilipo sasa, ninampongeza sana Mkurugenzi na watumishi wote. CAG amesema pamoja na jinsi ambavyo shirika linafanya, bado hili shirika ukisema mashirika ambayo yanajiendesha kwa hasara kwa miaka mitano mfululizo basi unataja shirika hili. Ukisema shirika ambalo lina mitaji hasi unataja shirika hili na tumeona kinachochangia kikubwa ni uendeshaji wa hili shirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Kamati imeshauri, CAG ameshauri. Nafikiri ni muda muafaka sasa Serikali kurudi nyuma na kuangalia jinsi gani ya uendeshaji na kipekee kuwapunguzia hii gharama ya kukodi ndege, kwa sababu tumeona CAG amesema mikataba mibovu katika kukodi ndege imesababishia shilingi bilioni 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya ndege ya Tanzania, wakala wa ndege wa Tanzania mikataba inakuwaje mibovu kiasi kwamba shirika linapata hasara? Basi tuwape nafasi tuwapatie hizi ndege ili waweze kuendesha wenyewe. CAG anasema, Serikali ilitoa ruzuku, shilingi bilioni 30, lakini shirika likapata hasara ya shilingi bilioni 35. Ina maana bila ruzuku, shirika lingepata hasara ya shilingi bilioni 65. Sasa kama tunapeleka ruzuku na tunataka wafanye vizuri, tuwasaidie kwa sababu wanafanya vizuri ili waweze kujiendesha. Wapewe ndege na pia walipiwe madeni yao ili waweze kuendelea kujiendesha kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo inaendelea kutuangalia Mkoa wa Kigoma na inaendelea kutaka kutufungua kwa uhakika. Bajeti ya Uwanja wa Ndege wa Kigoma ilitengwa mwaka 2021, hakikufanyika kitu; 2022 imetengwa, hakikufanyika kitu; 2023 imetengwa tena shilingi bilioni tisa. Wananchi wa Kigoma wamechoka kuambiwa kwamba bajeti imetengwa, wanataka kuona utekelezaji. Running way tumesaini mkataba pale, tunaamini mkandarasi atafika site kwa wakati.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Florence, muda wako umeisha.

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)