Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SILYVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Wizara yetu muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wake wote kuanzia Wizara hadi Mikoa, hakika ni kazi kubwa inafanyika kwa miradi mikubwa mbalimbali inayofanyika kuanzia viwanja vya ndege, reli, barabara na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada za kutaka kujenga barabara ya express way inayoanzia Kibaha kuja Morogoro na hatimaye Dodoma ambayo itajengwa kwa ubia, hakika hii inakwenda kuwa ni mkombozi wa usafiri kutoka Dar es salaam – Kibaha hadi Dodoma ambayo leo hii unachukua muda mrefu sana na kupoteza muda wa kufanya kazi zenye tija kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, lakini tunazo changamoto mbalimbali katika maeneo yetu na hususani katika Jimbo la Kibaha. Mimi niseme kwamba kazi inayofanywa na TARURA ni kazi inayoleta siasa lakini ni kazi ambayo ina mhudumia mwananchi mpaka eneo lake ikiwa ni pamoja na mitaa katika maeneo mbalimbali na hususani Kibaha Mjini. Pamoja na ujenzi mkubwa wa hizi barabara kubwa, lakini bado wananchi wetu wanapata adha kubwa sana kwa kukosa barabara zinazoingia katika mitaa yao na wakati mvua zikinyesha wanakuwa na changamoto kubwa sana ya kufanya shughuli za kiuchumi na ukizingatia Kibaha ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara inayotoka Sheli - Maili Moja - Shule hadi Muheza; barabara hii mvua zikinyesha haipitiki ingawa iko katikati ya Mji wa Kibaha ambao ni Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani; lakini tunayo barabara ya Tumbi – Boko Timiza, tunayo barabara ya Kwa Mathias hadi Mikongeni ambako kuna Makao Makuu ya Chuo Kikuu Huria, lakini vilevile tunayo barabara ya Kongowe – Forestry mpaka Yombo ambayo inaunganisha Kibaha na Bagamoyo, lakini Kongowe - Soga na Visiga - Madafu hadi Mbwawa; hizi ni barabara ambazo ziko ndani ya Mji wa Kibaha na ni barabara muhimu ambazo ningeomba ziko katika network ya TARURA. Sasa TARURA wapewe fedha waweze kuhudumia barabara hizi ili ziweze kutengeneza uchumi katika miji wetu wa Kibaha na ili ziweze kuleta tija kwa wananchi ambao wanataabika sana hasa mvua zinaponyesha, wanashindwa kufanya kazi zao za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa TANROADS kazi zinaendelea kuwa nzuri, lakini bado kuna maeneo mbalimbali ambayo tunaendelea kusuasua. Barabara ya TAMCO - Mapinga kweli ujenzi unaendelea lakini unakwenda kwa kasi ndogo sana, lakini tunayo barabara ya Makofia – Mlandizi kupitia Mbwawa hiyo barabara iko katika Ilani toka mwaka 2015 na kila mwaka inasemekana fedha zinatengwa, lakini utekelezaji haufanyiki. Mwaka huu tunaona kwamba zimetengwa fedha kidogo sana takribani shilingi milioni 600; sasa fedha hii itafanya nini? Italipa fidia, itaanza ujenzi au itafanya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe kwamba sasa tunapokwenda katika miradi mikubwa na ya kimsingi kama hii ya kuunganisha mikoa basi fedha itoke ya kutosha ili ifanye jambo ambalo litaleta tija na kuonekana machoni mwa watumiaji ikiwa ni pamoja na wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunayo Kisarawe road, barabara ambayo inatakiwa itoke pale Kibaha Mkoani ambayo itatuunganisha na Kisarawe na yenyewe hii imekuwa katika upembuzi yakinifu, bado haijaweza kuanza ujenzi. Naomba barabara hii ijengwe ili iweze kuunganisha Wilaya ya Kisarawe pamoja na Makao Makuu ya Mkoa wa Pwani ambayo ni Kibaha Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo tunayo barabara ya zamani kwa jina maarufu barabara ya Zamani. Barabara hii inaanzia pale Picha ya Ndege hadi Mlandizi; hii ni barabara ambayo naweza nikasema ni barabara muhimu na ambayo inasaidia sana hasa tunapokuwa na matatizo katika hiyo barabara kuu ya Morogoro. Ninyi ni mashahidi kunapokuwa na ajali katika barabara hii magari hayawezi kupita na ucheleweshwaji unakuwa ni mkubwa sana, hata kama kuna majeruhi kuwakimbiza hospitalini Tumbi inakuwa ni changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo barabara ni mkombozi katika katika jambo hilo kwamba ni barabara iliyokuwepo toka zamani na inahitaji tu ukarabati wa kawaida, sasa ukarabati umeanza kidogo, kidogo na kwa mafungu. Mimi nilikuwa naomba kwamba basi TANROADS ikarabati barabara hii ambayo itakuwa ni mbadala na kupunguza vilevile msongamano katika hiyo barabara kubwa ya Morogoro. Mtu anayetoka Kibaha kwa mfano anatoka pale Picha ya Ndege anataka kwenda Kongowe hana sababu ya kuja kwenye barabara kubwa na kuongeza foleni, anaweza tu akapita kwenye barabara hii na ikawa inaleta tija kusaidia kupunguza foleni katika barabara kubwa ambayo kwa sasa hivi ndiyo barabara kubwa ya kiuchumi inayopitisha zaidi ya asilimia 85 ya magari yote yanayoingia na kutoka Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nataka nitoe ushauri wa Wizara, kwamba TARURA ambayo inakwenda kutoa huduma kwa wananchi na ndiyo inayotengeneza siasa ya miundombinu kwa wananchi wetu, hakika bado hawajapata fedha za kutosha. Barabara nyingi ziko katika network yao, lakini fedha ya kuhudumia barabara hizi hata katika kiwango cha changarawe zipitike muda wote bado hawanazo jambo ambalo linaifanya azma hii njema ya kumpelekea mwananchi maendeleo kwa karibu ishindwe kufanyika.
Mimi ombi langu kwa Wizara, waangalie ni namna gani TARURA itapewa fedha zaidi ili barabara hizi zote ambazo ziko katika network angalau zifike katika kiwango cha changarawe kama hazitaweza kwenda katika kiwango cha lami ili azma ya kumuhudumia mwananchi kwa karibu iweze kuwepo na waweze kunufaika sasa na hizi barabara kubwa za highway. (Makofi)
Mheshiwa Mwenyekiti, ya kwangu ni hayo machache na ninaunga mkono hoja, tuko pamoja na Wizara yetu ya Miundombinu. (Makofi)