Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Geita Vijijini kwa kazi kubwa aliyotufanyia na nasimama kwa kujiamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaiona hii siti niliyokaa, hata mwaka 2026 niko hapa hapa, kwa sababu ya hii Wizara. Mimi nakaa kilometa 54 tu kutoka ninakotoka jimboni kwangu kwenda Geita Mjini, lakini kilometa kama 105 kutoka jimboni kwangu kwenda Mwanza ambayo ndiyo Geneva yetu kwa Kanda ya Ziwa. Tulikuwa tunatumia saa saba hadi kumi kwenda Mwanza; saa tatu kwenda Geita. Pamoja na kwamba sina lami, lakini nikupongeze sana kaka yangu Mbarawa, Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na Wizara yako unayoendelea kunifanyia kwenye jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli pamoja na kwamba umenipiga kidogo kanzu kwenye kusaini, sijaona kwangu lakini Meneja wangu yuko hapa tusije tukakabana baadae naamini kabla ya mwezi wa saba na mimi nitafanya sherehe kubwa ya kusaini mkataba wa lami kwa mara kwanza toka miaka 60 ya uhuru na tunapata hizo kilometa 20 na nikuombe Mheshimiwa Mbarawa tutakutana kwenye corridor pale, ongeza tano ziwe hata 25 at least sijaona humu, lakini mimi naamini Serikali inafanya kazi kubwa, imetutambua hata sisi watu wa kijijini, wananchi wangu wananiona hapa, nina kila sababu ya kukupongeza na kuipongeza Wizara yako kwa sababu kwa kweli pamoja na kuwa hatuna lami, kwetu kunapitika Mheshimiwa Waziri kunapitika, unatereza hata mimi mwenyewe naenda vizuri tu nalala kijijini kwangu wala sina shida, Mungu akubariki sana wewe pamoja na Wizara yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri wananchi wangu wananisikiliza. Tumehaidi mwaka jana na mzee wa sarakasi tulikuwa batch moja. Umeishasaini kule kwa mzee wa sarakasi, sasa mimi bahati nzuri sana ni bondia ambaye nilitarajiwa kupambana na January akanimbia, sitaki kupambana mimi na wewe maana mimi nakula ugali Mheshimiwa Waziri kisije kikakutokea kitu cha ajabu.

Naomba ukamilishe mchakato uje usaini mkataba kwa wananchi wangu nakuomba na mkataba huo utasainiwa Nkome watu wanasuburi kuona lami. Unajua kwetu ukiona lami Gwajima yuko hapa, ndiyo itakuwa sehemu ya kwenda kuogea hata mizimu Mheshimiwa Mchungaji hata mizimu unaogea maana tunaogea kwenye mawe sasa tukipata ka-lami utakuwa unaogea hata roundabout. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, wananchi wa jimbo langu wanatamani kuona lami na nikuombe nisikilize na njoo uweke mimi na wewe hatuna tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nilindie dakika zangu mimi ni mmoja wa Wabunge nilioenda Dubai kuona uwekezaji ulioko Dubai wala sijifichi nilienda kwenye ziara ya Kamati ya Mheshimiwa Mbarawa na mimi kidogo sijui unaweza ukanunua akili yangu bei gani, maana na mimi ni la saba mwaminifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunachelewa kwenda kwenye maendeleo kwa sababu ya degree. Mimi na twende taratibu degree risk assessment, mchakato; haya mambo yatatuchelesha, upembuzi yakinifu jamani..., tulikuwa humu Bungeni Bunge lililopita. Mimi nilikuwa Mbunge wa kwanza kwenye Wabunge tulioenda kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, risk assessment humu, sijui nini walichelewesha haya mambo na kuna wengine wanapinga humu ndani walikuwa Mawaziri kwenye hizo. Mazingira tutakata miti, kuna vyura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unajengaje reli ya kisasa ya matrilioni kwenda Congo, kwenda Mwanza halafu una bandari inayotoa mabehewa 120 kwa siku. Tunachelewa sana ni lazima ninyi wasomi sasa ikifika mahala tutagawana, unajua gita lina kitu cha kukoleza, Nape ni mtaalam, mimi nitaondoka na kale kakukolezea spika hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachelewa kwa sababu ya watu wachache wajinga ambao kila kitu unataka ushirikishwe, sawa. Tunataka tuletewe mkataba humu kila mtu atachangia dakika kumi lipi ambalo unaweza kupinga kwenye dakika kumi? Twende taratibu ni lipi? Niulize humu lipi? hivi tumefika mahala sasa na watalamu wotee ni wajinga? Mpaka CAG naye anayetugombanisha humu nae ni mjinga? Maana sisi tuna jicho lakini hatuamini, haya mtu anakuja anazungumza miaka kumi, miaka 20 ya TICTS ilitufikisha, ikatupeleka; sawa miaka 20 si tulikuwa darasani au wenzangu hamsomi? Tumefika mahala sasa tunang’amua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dubai DP World ukifika pale mimi nilienda na Wabunge wenzangu tukawa kama 30; kule bandarini mimi sikuona watu, niliona mashine tu zinapishana hivi “kakakaka” kadada kadogo hivi nikakaomba na namba ninayo hapa kakibonyeza hivi kontena linaenda. Tutoke huko tulikobaki hatuwezi kwenda kwenye hiyo mifumo...

MHE. GEOFFREY I. MWAMBE: (Hapa hakutumia kipaza sauti).

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Nasikia sauti Mheshimiwa naongea na kiti.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma, endelea na mchango wako.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Naendelea.

Mheshimiwa Mwambe nakuheshimu sana, usiingie kwenye kumi na nane, mimi hunipigi swagga brother. Tulikupa nafasi na uli-fail, ndiyo maana uko-backbencher, tena nyuma yangu nipige taarifa uone.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiwasikilize watu wa hovyo, hii nchi ni yetu wote, tunajenga meli Mwanza ya mabehewa kwenda Uganda, tunatengeneza reli kwenda Congo halafu unakuwa na watu kama Mwambe huyu, simama huyu. Wewe mchakato, tulikupa nafasi kutoka EPZ mimi mwenyewe umenifelisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Taifa ni letu wote, mliosoma na sisi, niwaombe tena tumechelewa, tumechelewa kila mtu ana uwezo wake humu ndani, kuna mtu ana uwezo wa akili na mtu mwingine anauwezo kama wa kwangu mimi najivuna kwa sababu gani? Sina shule, lakini mimi ni msukuma, najisimamia mwenyewe, hatuwezi kutembeza imprest Bungeni humu. Tusitembezee mawazo ya watu wachache kuja kununua Bunge, pinga haya tusimamishe anayepinga hapa atueleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wanajua tunatoka sasa reli ya ngongongo au labda mwenzangu hajapanda treni, ngongongo tunaenda mshale, halafu una watu 900/1200 bandarini hayo si mawazo potofu kama ya kina Mwambe hawa. Nikuombe sana huyu ni Mbunge mwenzangu, usijichanganye kunipiga swagga, kwa sababu nimemsikia amesema wewe; na yeye ni mpingaji.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma endelea na mchango wako…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nikuombe hii nchi ni ya kwetu wote na nazungumza kwa sababu mimi ninafaida na reli ya mwendokasi, tusisubiri haya mawazo ya kujaribisha, twende mbele, hawa watu wanao tuletea mawazo ya kujaribisha kutegana tegana humu mimi nina miaka 61 leo ya uhai wangu tusije kuchambuliana ma–file humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe na niwashawishi Wabunge wenzangu kwamba kiukweli huwezi kuwa na train ya mwendokasi, unatoka kwenye makontena ya kusahihisha, basi inawezekana wenzangu hawajawahi kupita bandarini. Ukipita pale bandarini usumbufu uliopo unaweza ukalipa TPA, ukaambiwa leo sijui portal, sijui Harris hayupo, mnakaa hata wiki mnasubiria makontena na storage inasoma. Jamani hatuwezi, tunasomesha watoto wenye degree zao watu wa IT halafu tunang’an’gana kukaa analogue. Mimi mwenyewe natoka kwenye analogue sasa hivi ni doctor. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalieni vizuri natoka kwa sababu naendana na wakati ningepewa hii doctor ya heshima miaka kumi iliyopita nisingeelewa lakini leo tu–complete na mimi na mtu anayepinga hapa tukakae kwenye tv watu watusikilize tumwage material, hatuwezi kuwa na degree ambazo hazija..., kizungu mnasemaje?

MBUNGE FULANI: Hazija-qualify.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Hazi–qualify, yaani kwenye maisha halisi, nashukuru kukaa na yaani lazima tutoke huku, unaweza ukajaza Taifa la degree za watu wa hovyo na mkabaki kuwa wa hovyo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Sekunde 30.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja. Ukienda Dubai nakupa mfano mzuri. Mimi nimebahatika kumuona Mfalme wa Dubai, huyu hapa nilikuwa na mtafsiri wangu. Ziara yangu kutoka jimboni na wananchi wangu wananisilkiliza. Nikamuuliza umeijengaje Dubai? akaniambia wakati naanza kutoka kwenye maisha ya Dubai kuwatengeneza watu waione Dubai tunayoiona leo, wakaniambia nilivyoanza kuwaruhusu watu wajenge kutoka mataifa mbalimbali wale wazee maarufu wa Dubai wakaandamana. Walivyoandamana akawaambia njooni tuzungumze Ikulu. Wakaenda kuzungumza akawaambia mna shida gani? Unauza Dubai kila mtu unampa hati; kuna Wanaigeria kuna Watanzania, kuna Wahindi kuna Wazungu; mwisho wa siku sisi tunaondoka Dubai, akasema, sasa mna tatizo na nilichokifanya? ndio. Tufanyeje? akawaambia sasa nyie mmekuja wangapi? 150. Nawagawanya mara mbili 75 mtakaa airport, 75 mtakaa bandarini. Ndio njia ya kutoka Dubai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona mtu amekuja na nyumba anaipakia kwenye meli nakutumia na jeshi mnisaidie kunipigia simu tu. Leo Dubai ukienda pale sijui vizuri kizungu utaona majumba. Nyinyi mnang’ang’ana na vitu vya kijinga. Mtu akitaka kujenga unawaambia huyu ni mzungu, ukimpa ardhi tuta, ndiyo tutabaki na tunalima mazabibu. Haiwezekani. Tuachane na wapingaji tutengeneze Tanzania ya kisasa, tupambane na bandari zinazotuzunguka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.