Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, kwa hiyo, kwa kuwa, ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu, la kwanza kabisa niunge mkono hoja ya Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipita nje hapo unaona limeandikwa Bunge la Tanzania, kwa hiyo, Wabunge kutoka majimbo mbalimbali tukiingia humu tunakuwa Wabunge wa Taifa. Serikali inaposhauriwa na Waheshimiwa Wabunge ichukulie kwamba, Bunge linaishauri Serikali ili kuweza kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, michango mingi imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge hapa, wamezungumza kwa kishindo sana kuhusu barabara, lakini kwa kuwa na mimi ni mmoja wa Wabunge wa Taifa, nataka nianze na wastaafu wa ATCL. Kuna watu wameshafariki hawajalipwa pesa zao, kuna watu wako kitandani hawajalipwa pesa zao, kuna watu wana mazingira magumu, Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa atupatie majibu hawa wastaafu watalipwa lini? Maana deni lao lilishafanyiwa uhakiki, upembuzi yakinifu ulishafanyika kwa hiyo, tupate majibu kwamba, lini watalipwa pesa zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, nataka nizungumzie Barabara ya Ntyuka Junction - Mvumi Makulu - Mvumi Mission - Handali kwenda Kikombo. Barabara hii ina wakandarasi wawili, kuna mkandarasi ameanzia mjini na mwingine ameanzia Kikombo. Nataka Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba, hawa wakandarasi wanakwenda kutuacha sisi kama kisiwa au wanaenda kumaliza kazi ya kutuunganisha Makao Makuu ya Jimbo la Mvumi pamoja na Mji wa Dodoma na Mji wa Chamwino wa Kiserikali? Majibu hayo yatakuwa majibu mujarabu sana kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Mvumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia hapa, kwa suala la kipande maana hatuzungumzi kubinafsisha bandari yote, tunazungumza kipande ambacho walikuwa wanafanya kazi TICTS. Mimi huwa nafananisha na mtu amenunua lori lake, amenunua semi, matairi yameisha, propeller imekatika, huna uwezo umeli-park nje, sasa kazi yako ni kuonesha wajukuu gari la kwangu hili, lakini wajukuu hawana chakula, wamefukuzwa ada, wewe kazi yako kuonesha lile gari bovu, gari hili langu bwana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachofanya hapa, tunaiomba Serikali itafute mwekezaji wa kuja kutia matairi mapya, kununua propeller jipya, ili mtoto wetu sisi awe tingo, wakusanye pesa, maisha yaendelee. Kwa hiyo, eneo hilo tunaomba Serikali ikatafute mwekezaji mwenye uwezo mkubwa, lakini wakati wakitafuta mwekezaji mwenye uwezo wahakikishe jambo la kwanza wanalinda ajira za Watanzania walioko katika eneo lile. Tusije tukaanza tena kuathirika, watoto wetu wakafukuzwa kazi, hapana, tunataka mwendo mkubwa zaidi kutoka pale walipoishia TICTS kwenda mbele, ili tuweze kujiletea maendeleo ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukishabinafsisha bandari katika kipande hicho kidogo tutapata tija kutoka makusanyo tunayokusanya sasa yataongezeka zaidi, lakini na uharaka. Juzi tumeona wafanyabiashara namna ambavyo wamelalamikia suala la uharaka, tunaambiwa meli moja kila siku moja tunayoichelewesha tunalazimika kuilipa Dola 25,000. Sasa hebu niambie na pale kuna meli kibao zinasubiri ziko foleni, tuweke mwekezaji ambaye atatuondoa kwenye deni lile, tuweke mwekezaji ambaye speed yake ya kutoa ma-container itakuwa kubwa ili kuondosha ile gharama ambayo tunaipata pale.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Lusinde, Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Songe.

TAARIFA

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Taarifa Mchangiaji kwamba, zile gharama ambazo anazisema za ucheleweshaji kwa siku dola 25,000, mwisho wa siku analipa mlaji wa mwisho. Kwa hiyo, tunaongeza gharama kwa vitu vyetu bila sababu ya msingi.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, Taarifa unaipokea?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea maana inatoka kwa Mbunge kijana kabisa, mtu smart, nawezaje kuikataa Taarifa ya kijana wangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake ni njema, yote hayo ndio tunayoyazungumza sisi kama Wabunge, kuishauri Serikali kwamba, itupunguzie hizo gharama kwa sababu, gharama mwisho wa siku zinakuja kwa anayetumia. Unaweza kuona hata bidhaa hizo ambazo zilitakiwa ziuzwe hapa kwa bei ya chini zaidi zinauzwa bei ya chini Zambia, zinauzwa bei ya chini Kongo, halafu zinaturudia tena sisi hapa. Kwa hiyo, soko letu linakuwa gumu, lakini tukiweza kuboresha hiyo, bidhaa zetu zitakuwa za bei ya chini na hapo wageni wengi watakuja kununua hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nilizungumze. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais ametupatia pesa milioni 500 kujenga Daraja la Mloa Barabarani kuunganisha na Makang’wa na ile ni barabara ya lami ambayo baadaye inakuja kujengwa kuja tena kuunganisha Mvumi. Vilevile connection ya watalii tunapata uwanja mkubwa wa ndege hapa Dodoma Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu uwanja utakuwa na faida kama tutafungua barabara mpya kutoka hapa Dodoma Mjini, kupitia Nagwelo, kwenda Huzi, kwenda Manda, kwenda Ilangali, iingie ndani ya hifadhi kwa njia ya mkato. Badala ya watalii kuzunguka kupita Iringa watakuwa wanakatiza hapa tu taratibu wameshaingia kwenye Ruaha Game Reserve na baadaye wanaingia kwenye National Park ya Ruaha kwa ajili ya kuona wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya barabara yamezungumzwa kwa umakini. Kuna barabara ambazo zinajengwa Dodoma za mzunguko, lakini barabara nyingine za mzunguko ambazo Wizara izifikirie ni Barabara ya Mpwapwa inayotokea Kibakwe kwa Mheshimiwa Simbachawene. Hii barabara ni ya muhimu sana, badala ya mtu akitoka Iringa kuja moja kwa moja anaweza kuingilia pale Kibakwe akaja kuunganisha Kongwa kwa Mheshimiwa Mzee Ndugai, tayari tumepata barabara nyingine ya lami inayotokea Kiteto, moja kwa moja anakwenda Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana ujenzi wa Dodoma ukatuondolea adha ambazo wanapata sasa hivi Dar-es-Salaam. Tunapozungumza jiji tusiseme tu Dar-es-Salaam maji yakijaa kuna shida, hata Dodoma mvua ikinyesha kuna shida. Nje ya Bunge hapa kunakuwa na foleni kubwa kabisa. Kwa hiyo, tuangalie majiji yote, modal ya Dar-es-Salaam ya kuondoa matatizo ya mvua hiyo hiyo itumike kwa Dar-es-Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dodoma, tusiseme leo tunazungumzia Dar-es-Salaam halafu kesho Dodoma inapata shida, tunaanza kusema, aah, na Dodoma, hapana. Wasomi wetu lazima waiangalie sasa nchi namna inavyokuwa na namna ya kuondoa misongamano ya magari pamoja na maji mvua ikinyesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kama nilivyosema. Sina shida na Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. Sina shida na watendaji wote wa taasisi zake wamejipanga vizuri, ni matarajio yetu kwamba, watakwenda kwa kasi zaidi kuweza kuondoa matatizo yanayolikabili Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)