Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, kwanza nawapongeza Waziri na timu yake kwa bajeti ambayo imefafanuliwa vema sana. Nina mawazo ambayo naomba kuyawasilisha kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, nianze na EPC+F; napongeza hatua hii ambayo kwa mujibu wa hotuba ya Waziri mikataba itasainiwa kabla ya mwezi Juni. Jambo hili linaonekana kama ndoto na wananchi wamekuwa bado gizani, nadhani wataamini pale watakapoona kweli mkataba unasainiwa. Hizi ndio feelings za wananchi wanaosubiri kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Mafinga - Mgololo.

Mheshimiwa Spika, tunachokifanya ni maendeleo lakini pia ni kujenga na kuimarisha siasa na uelewa wa wananchi. Wananchi wakiwa na mashaka ni muhimu Serikali kuwaondolea mashaka, tunaita political management kwamba hiki kilichoandikwa ndicho kitakachotendeka. Nasema hivi kwa sababu kwa uelewa wa wananchi kutokana na Bajeti ya Ujenzi hii tunayoendelea nayo kwa maana ya mwaka 2022/2023, matarajio yao ni kwamba ujenzi ulikuwa unaanza mwaka huu, kwa hiyo wanaposikia kwamba mkataba wa EPC+F utasainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, wanatuambia mbona kila mwaka mnaitaja tu hii barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo na kwa kuwa siasa ni perception, nashauri shughuli ya kusaini mikataba na wakandarasi iwe shughuli nzito ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao. Barabara hii imesubiriwa miaka mingi, ni ukombozi kwa uchumi wa Mufindi, Iringa na Taifa kwa ujumla hasa kutokana na umuhimu wa mazao ya misitu na zao la parachichi.

Mheshimiwa Spika, nashauri shughuli iwe shirikishi kwa maana ya Chama, Serikali na Halmashauri (Madiwani) washiriki katika signing ceremonies.

Mheshimiwa Spika suala la pili ni ufafanuzi, wananchi wanafuatilia sana hizi hotuba katika mitandao, wanauliza kuwa hii barabara Kasma 4037 imeandikwa kilometa 78 na imetengewa shilingi 50.00? (ukurasa wa 248), na kwamba chanzo cha fedha ni GoT kwa maana Serikali ya Tanzania, na mbona kwenye hotuba Waziri ametaja hiyo EPC+F, je, kipi ni kipi, nami nauliza kwa lugha ya wananchi.

Mheshimiwa Spika ushauri wangu, kwa kuwa jambo hili ni geni na ili kuwapa wananchi comfort na uelewa Mheshimiwa Waziri anapojumuisha atolee ufafanuzi ni nini hii EPC+F. Ni muhimu sana wananchi kuelewa na sehemu sahihi ya kueleweshwa ni wakati Mheshimiwa Waziri anahitimisha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ATCL; napongeza jitihada za Serikali kununua ndege na hasa ya mizigo. Hata hivyo nina ushauri kuhusu ATCL hasa katika suala la delays na kukosekana kwa connections. Ilivyo kama unatoka Dodoma kwenda Mbeya lazima ukate tiketi mbili, yaani Dodoma-Dar, kisha Dar-Mbeya. Nimeshauri suala hili mara kadhaa, sasa sijui ni masuala ya kitaalam au ni kitu gani. Kwa nini tusiwe na connecting routes?

Mheshimiwa Spika, nimeshauri pia mara kadhaa kwamba pawepo na routes za kuanzia Dodoma kwenda pande kuu za nchi hata kama itakuwa kupitia Dar. Kwa mfano kwa nini tusiwe na routes Dodoma to KIA, Dodoma to Mbeya, Dodoma to Mtwara via Dar. Dodoma to Mwanza na Dodoma to Kigoma via Tabora. Ikiwa juzi tumezindua Ikulu yetu maana yake ni kwamba sasa Dodoma ni real capital city ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nashauri pia ili kuendana na kasi ya kupokea watalii kama matokeo ya Royal Tour, tufikirie kuwa na ndege ambazo zitakuwa zinabeba abiria kwenda kwenye mbuga za wanyama. Tukiwa na ndege za kubeba abiria kati ya nane hadi 14, zitabeba watalii kutoka KIA to Manyara, Serengeti, Mikumi, Ruaha na kadhalika. Tukiwa na ndege za aina hiyo zitasaidia kupunguza gharama za kufikisha watalii mbugani lakini pia watafika kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, taa za barabara katika Mji wa Mafinga; naomba kukumbusha uwekaji wa taa za barabarani kando ya barabara ya TANZAM eneo la Mafinga Mjini hasa Kinyanambo hadi Hospitali ya Mafinga. Suala hili linakumbushwa sana na wananchi kwa kuwa hata wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais lilizungumzwa na Mheshimiwa Waziri mbele ya wananchi na mbele ya Mheshimiwa Rais alieleza umma wa Wana-Mafinga kwamba kutawekwa taa za barabarani umbali wa kilometa mbili, naona mwaka wa fedha uko mwishoni na taa hizi bado hatujaanza kujenga. Ni ombi langu kwa niaba ya wananachi wa Mafinga kutekeleza ahadi hii.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara Iringa-Msembe; barabara hii ambayo ni kiungo muhimu katika biashara ya utalii, katika bajeti hii ya mwaka 2022/2023 kwa uelewa wa wananchi na sisi Wana-Iringa ni kwamba inaanza kujengwa mwaka huu, hata hivyo nimeona kwamba huenda ikatangazwa mwezi Juni, kwa wananchi wanashindwa kuelewa na hata mimi nilitarajia kwamba tutakuwa tumeanza kujenga au walau mkataba kuwa umeshasainiwa. Kwa hiyo, rai yangu ufafanuzi ufanyike, kwa sababu uelewa ni kwamba hata hii kutangaza mwaka huu pengine ujenzi hautaanza mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuboresha utendaji wa bandari kupitia mwekezaji; kwanza nawapongeza sana bandari kwa ubunifu, lakini zaidi kwa ushirikishwaji. Sisi Wabunge tumepata semina kuhusu nini kinakusudiwa kufanyika na kitakuwa na manufaa gani kwa nchi yetu. Yapo mashaka na maoni tofauti, tuyapokee lakini kama Taifa lazima tuamue kwenda mbele, haiwezekani tuendelee kuchekwa na nchi majirani kwamba tumekalia uchumi. Tuamue sasa, twende mbele.

Mheshimiwa Spika, mimi kwa bahati nzuri nimetembea duniani nikiwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje, mfano mdogo nchi ndogo kwa eneo kama Singapore, bandari yao inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na ni chanzo cha mapato kwa nchi yao. Katika kufanya maamuzi tukishajiridhisha ni kwa manufaa ya Taifa letu, basi mengineyo tuweke pamba masikio, tufanye maamuzi sasa, tusirudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.