Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ila na mimi nichangie hotuba ya Mtukufu Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Hotuba ya Rais kwanza kutoa muda wa kuchangia ni kama vile tunapoteza muda, ile hotuba haina matatizo. Mwelekeo wake ni mia kwa mia hakuna mtu anaweza kuipinga. Ya kukazia ni yale mambo aliyoyaeleza mwenyewe tuyafuate na yatekelezwe haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuunda Mahakama ya Mafisadi ifanywe kwa haraka sana. Pili, wakati wa bajeti hapa Bungeni wanakuja Wakurugenzi, Wakuu wa Mikoa, Ma-RAS
wanakuja kufanya nini? Hilo nalo liondoke. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kufuta Sherehe za Uhuru na ikiwezekana afute na Sherehe za Mwenge iwe hata mara baada ya miaka mitano. Tunabana matumizi, Mwenge kila mwaka unapita na tunapoteza pesa. Nimezungumza mimi Mwenge ukipita Wilayani
kwangu siku tatu kazi hakuna. Siku ya kwanza wanalaki Mwenge, Ofisi za Halmashauri zinafungwa. Siku ya pili wanapokea Mwenge kwa hiyo wanakesha kwenye Mwenge. Siku ya tatu Mwenge ulipopita wanalala wamechoka. Sasa ndugu zangu ni uharibifu, ni lazima twende
kama anavyosema kazi tu, hiyo ndiyo kazi tu. Hatuwezi kufanya sherehe wakati watoto wanalia, hawana madawati, dawa, viatu na chakula, tupunguze sherehe za ajabu ajabu.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilishangaa sherehe za Mapinduzi Zanzibar wanapakia watu elfu moja kutoka Pemba. Sasa kulisha chakula watu elfu moja ni gharama wakati wananchi hawana hela? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tupunguze Majimbo yamekuwa mengi, Wabunge wamekuwa wengi gharama za kuendesha Bunge ni kubwa Rais alizungumza hapa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Bunge linatumia gharama kubwa. Mabunge mengine ni watu ishirini na tano au watu kumi na tano. Ndugu zangu hatuendi namna hiyo. Twende na Bunge la kisasa, tumekalia kusema ma-DC wapungue, Wakuu wa Mikoa wapungue na Wabunge
tupungue kutokana na idadi ya ukubwa wa Majimbo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta Jimbo kama la Kwela kwa Mheshimiwa Malocha ukubwa wake ni sawa na Rwanda, anapewa pesa za kuendesha Jimbo sawa na Mbunge mwenye watu elfu mbili. Hapa uhalali uko wapi? Lazima twende na sera ya „Hapa Kazi Tu‟ na kazi ianzie kwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wanaunda mpaka vikosi vya michezo wanakwenda na ndege ya Rais na kurudi na ndege ya Rais, huu ni ubadhirifu wa hali ya juu.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani wakati wa bajeti wanatoka wataalam wa Nkansi wanakuja Dar es Salaam wanakaa wiki mbili, wao na madereva wao, gari sita, zinakuja Dar es Salaam eti bajeti. Karne ya 21, Namanyere ije ifanyiwe bajeti Dar es Salaam! Mkurugenzi na kundi lake atoke Bukoba aje Dar es Salaam, atoke Tarime aje Dar es Salaam, ndugu zangu hii haiwezekani, kuanzia sasa bajeti zifanyike Wilayani itumike mitandao tu. Haiwezekani Madereva na Wakurugenzi wa kila Wilaya kuja Dar es Salaam
kuchezea hela za Serikali wakati wananchi hawana maji, dawa wala barabara. Tunafanya sherehe kubwa kama nchi za Kiarabu, haiwezekani lazima tubanane, tule kwa jasho letu, hatuwezi kwenda kienyejienyeji. (Makofi/Kicheko)
Kisa kingine kuhusu madereva wa Serikali, madereva hawa wanapunjwa, madereva wa Mashirika ya Umma wanakuwa kama wako peponi madereva wa Serikali hawapati chochote. Hata akistaafu anapewa shilingi milioni mbili, itamtosha nini shilingi milioni mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wa marine service wa Lake Tanganyika, Lake Victoria, Lake Nyasa, hawaajiriwi, ni vibarua miaka yote. Hawana likizo, hawana insurance yaani wamekaakaa tu, wanaona bora wagongeshe meli watu wafe kwa sababu hawathaminiwi
kabisa. Kwanza hii marine service ni shirika la nani, ni la umma kweli? Lazima anayehusika alichunguze hili shirika la marine service. Nimekutana na wafanyakazi wa Liemba wanasema Mzee hatuna hata likizo, insurance, mishahara duni, wakistaafu hawapewi chochote wakati TRA, Shirika la Nyumba wao ni kama wako peponi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu NASACO amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja, turudishe NASACO i-control mali bandari. Leo kuanzia Bagamoyo mpaka Dar es Salaam bandari bubu nyingi. Wazanzibar ndiyo wamefanya pa kupitishia mali na kufanya huku Bara ndiyo soko. Tunaibiwa mchana mchana! Mali yote inatoka Zanzibar inapitia vichochoroni hawalipi ushuru. Zinaletwa mali za ajabu ajabu, sukari, mafuta na kila kitu. Wanastarehe kuinyonya Bara hawalipi ushuru, hiyo haikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuweke mikakati anayekamatwa mara moja mali yake itaifishwe hamna kwenda Mahakamani. Pia chombo kinachopakia mali ambayo hailipii ushuru kitaifishwe, watashika adabu. Wote ambao wanahisiwa kwamba wanashirikiana na
wafanyabiashara kutuibia, cha kwanza kabisa mali zao zinyang‟anywe kabla ya kupelekwa mahakamani. Apewe form aulizwe hii mali umeipataje, akishindwa kujieleza anyang‟anywe kabla hajaenda Mahakamani. Akienda Mahakamani, Mzee mlango chini anapita anafungwa
miezi sita, anabakia anachezea ile mali. Kwanza mali yake inyanganywe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mambo ya kuendelea kuleana yaishe sasa.
Nimezungumza sana habari ya Namanyere, miradi ya maji wanahamishwa Wakurugenzi, Maafisa Ugavi na Wahandisi wa Maji, naomba majibu yakatumbuliwe Wilayani Namanyere kuna watu wameiba pesa. Kule kwa vile tuko karibu na DRC-Congo wafanya kama hamna
Serikali, wanafanya mambo wanavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimezungumza hapa Bungeni, mtu anaandika gharama ya gari Namanyere Dar es Salaam gari tani kumi shilingi milioni kumi na mbili badala ya shilingi milioni tatu. Anaandika mabomba yameingia ndani gari tisini na nane milioni wakati bomba
hakuna yaani gari hewa, mabomba hakuna, Serikali imelala usingizi. Tunataka tutumbue majipu tupeni idhini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya mbolea haya, mbolea hazifiki kwa wakulima wanaandika hewa tupu mpaka majina ya marehemu wanaandika. Hatuwezi kukubali safari hii, namwambia Waziri wa Kilimo, Kamanda wangu Mwigulu, anipe kibali nitembee kijiji kwa kijiji,
nikague mimi mwenyewe simwamini DC, simwamini OCD, siiamini TAKUKURU maana ndiyo wamefanya njia za miradi yao. Nitatembea mwenyewe, Mheshimiwa Mwigulu nipe kibali nikakague kijiji kwa kijiji, nyumba kwa nyumba kama mbolea au mbegu imefika. Serikali ya CCM inatukanwa ni kwa sababu ya Watendaji hawa, wamefanya miradi yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo, kuanzia sasa bajeti ijayo hakuna kuja cha Mkuu wa Mkoa, hakuna kuja cha RAS, hakuna bajeti za Wilaya kupangiwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)