Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, kupitia njia ya maandishi naomba kuchangia bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Sekta hii ni sekta wezeshi katika ujenzi na maendeleo ya nchi yetu ikichangia takribani asilimia 26 katika kuleta fedha za kigeni. Hii ni sekta inayoongoza katika sekta zinazounda tasnia ya huduma (service industry). Unapoangalia mafanikio na mchango wa utalii katika kuingiza fedha za kigeni ni vigumu kutenganisha usafiri na usafirishaji na utalii. Pamoja na umuhimu huu hii ni sekta ambayo tofauti na rasilimali zinazokwisha kama madini, sekta hii ni ya kudumu na huleta manufaa kadri inavyoboreshwa.
Mheshimiwa Spika, ninapoandika na kuchangia sekta hii nitambue mafanikio makubwa katika Taifa letu katika mwezi huu, hatua ya kufikia makubaliano kati ya Serikali na wawekezaji katika mradi wa kutengeneza gasi kimiminika (LNG) na matumizi ya gesi asilia katika magari yaendayo kasi jijini Dar es Salaam (CNG) ni jambo lenye tija kubwa kwa sekta hii na Taifa kwa ujumla. Mafanikio haya yanahitaji nguvu na ushiriki mkubwa wa Wizara ili tufikie malengo tunayotarajia.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuishukuru Wizara kwa kuboresha uwanja wa ndege wa Bukoba hasa eneo la uongozaji ndege. Nilipongeze Bunge letu tukufu kupitia Kamati inayosimamia Wizara hii kwa kuishauri Serikali ijenge uwanja wa ndege mpya mkoani Kagera. Eneo la mkoa wa Kagera ukizingatia na nchi zinazotuzunguka (location advantage) kuna umuhimu na haja ya kujenga uwanja wa ndege mkubwa maeneo ya Omukajunguti au Kashaba ili kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji kwa maeneo haya. Wananchi wa Rwanda, Uganda na DR Congo katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii wanategemea eneo hili.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za uwanja wa Bukoba uliopo sasa, uwanja huu ni miongoni mwa viwanja saba vyenye abiria wengi nchini bila kuhesabu abiria wanaoshuka Mwanza kwa kuogopa kutua Bukoba. Tunaiomba sana, Serikali ijenge uwanja wa ndege mkubwa Kagera.
Mheshimiwa Spika, shirika la ndege la ATCL linaelekea kuanza biashara ya kusafirisha mizigo kwa ndege maalum za mizigo. Naomba na kushauri katika kutekeleza mpango huu ni muhimu kuanzia sasa kuwashirikisha wadau wa kuuza na kuagiza bidhaa toka nje ya nchi kwa lengo la kubaini wingi wa mizigo inayohitaji huduma ya ndege. Tuwe na uhakika sasa kabla ya ndege ya kwanza kuwasili, wazalishaji wa nchini na nchi jirani wahamasishwe kutafuta masoko ya moja kwa moja na maalum.
Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza sana kwa kujenga vivuko katika Ziwa Victoria upande wa Mashariki na Kusini, niombe na kushauri sasa ombi la kujenga vivuko katika Ziwa Victoria upande wa Mkoa wa Kagera litekelezwe.
Mheshimiwa Spika, napongeza mpango na uboreshaji na ujenzi wa maegesho Kisiwa cha Ikuza. Tunaomba na kushauri vivuko kwa kutoa huduma kati ya Magarini na Kyamkwikwi na visiwa vya Ikuza, Mazinga, Bumbiile na Kelebe ipangwe na kutekelezwa. Upo mpango wa siku nyingi wa kujenga na kuweka kivuko Kabango Bay kilometa 42 Kaskazini mwa Mji wa Bukoba. Kivuko hiki ni muhimu katika kuunganisha nchi yetu na Uganda katika dhana hii ya biashara huru katika Bara la Afrika lakini na mahusiano mema na nchi jjrani.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuishukuru Serikali na hususani Wizara kwa mipango ya kuboresha usafiri katika Visiwa vya Wilaya ya Muleba. Uwepo wa meli ya Clarias na meli/boat maalum ziendazo kasi utasaidia kuboresha maisha ya Visiwa vya Goziba, Kelebe, Bumbiile, Ikuza na Mazinga na bandari ndogo za Kyamkwikwi na Magarini nchi kavu. Tunashukuru kwa nia ya kupeleka barge Bandari ya Goziba ili kuwezesha meli tunaposubiri gati yetu kuboreshwa. Nashukuru kwa mipango na utekelezaji wa uboreshaji wa Bandari za Bukoba na Kemondo Bay, tunapoendelea na uboreshaji nishauri Bandari ya Bukoba iwekewe mazingira ya kuwezesha meli zaidi kuegesha hasa Songoro Marine. Tunaomba meli za Songoro ziwezeshwe kutoa huduma katika bandari na visiwa vya Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Spika, nipongeze na kushukuru kwa ujenzi wa barabara kiwango cha lami kutoka Muhutwe, Kamachumu, Buganguzi, Nshamba mpaka Muleba. Ujenzi umebakiza kilometa 7.4 kukamilika, tunaomba na kushukuru kazi iendelee kwa kumalizia eneo lililobaki. Tunaomba mchepuko wa kilometa tatu kuelekea Hospitali ya Ndolage ufikiriwe kwa kuendeleza kilometa moja iliyojengwa katikati ya Mji Mdogo wa Kamachumu.
Mheshimiwa Spika, napongeza mpango wa ujenzi wa barabara ya Mutukula, Bukoba mpaka Kagoma, ombi na ushauri ni kuwa maegesho ya magari wakati wa kushusha a kupakia abiria yaboreshwe. Sasa hivi barabara tajwa ina mabasi ya abiria mengi sana, tena mengi yakipita maeneo haya usiku na alfajiri, uboreshaji uzingatie eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu niombe kufungiwa taa za barabarani katika Mji Mdogo wa Kamachumu. Pamoja na eneo hili maboresho ya barabara ya Mutukula mpaka Kagoma yahusishwe kuweka taa Mji Mdogo wa Muhutwe, Kakindo, Izigo, Kagoma na Kikuku.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.