Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata fursa ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya mwaka 2023/2024. Namshukuru Mungu kwa uwezo huu wa kuwasilisha mchango wangu nikiwa na afya njema.
Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Rais Samia kwa juhudi zake za kuhimiza kukamilisha miradi mikubwa ikiwemo SGR, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari na vivuko. Aidha, nawapongeza Waziri na timu yake ya watendaji kwa bidii yao katika kufanikisha malengo ya Wizara pamoja na changamoto zinazojitokeza.
Mheshimiwa Spika, tunatumbua bahati tuliyonayo kwa nchi yetu kuwa na bandari kadha zilizomilki yetu, lakini zinakosa kuleta matunda tarajiwa na uwezo upo wa kutumika sawasawa kwa tija.
Mheshimiwa Spika, nikubaliane na wazo la ubia kwa bandari ya Dar es Salaam ina uwezekano wa kunyanyua uchumi wetu kwa kiwango kikubwa. Bandari ya Dar es Salaam katika sehemu yake ilipo ina uwezo wa kuhudumia nchi kadhaa ikiwemo DRC, Rwanda, Zambia, Malawi na Uganda.
Mheshimiwa Spika, kwa bandari ya Dar es Salaam kinachotakiwa ni mabadiliko ya uendeshaji na usimamizi mzuri, ni muhimu kwa kuongeza tija.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupigiwa mfano kwenye ujenzi barabara mimi mwenyewe ni shahidi nimeona. Nilibahatika kusafiri kwa barabara kwenda Kakonko - Kayla barabara haijajengwa na juzi nimetoka Nyakanazi mpaka Kakonko lami safi sana, barabara imenyoooka kama mgongo wa ngisi, kusema kweli wanastahili pongezi sana.
Mheshimiwa Spika, mpango mzuri wa barabara ya express way Kibaha mpaka Morogoro ni ukombozi mkubwa na kichochea muhimu sana kwa uchumi na maendeleo, inakwenda kuondoa udhia mkubwa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi huu wa express way ya Kibaha - Morogoro sijui kwa nini Wizara bado haikamilishi kujenga Daraja la Morogoro kwenye eneo la Jangwani Dar es Salaam ambao ndio kiungo muhimu sana, eneo hili ni shida sana wakati wa mvua. Ni muda mrefu tunaambiwa kwamba ujenzi utaaanza, lakini ujenzi huo hauanzi.