Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nichukue nafasi hii kwa mara nyingine tena kuendelea kuwashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Muhambwe kwa kunipa kura za kutosha kuweza kuja kuwahudumia kama Mbunge wa jimbo lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia maeneo mawili; Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utawala Bora na nitaanza na Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna mamlaka ambayo inaruhusu kuanzishwa kwa vijiji vipya. Katika Jimbo langu kuna Vijiji vipya vimeanzishwa kama vitano lakini bahati mbaya vimeanzishwa bila kuwepo miundombinu ambayo inawezesha wananchi wa sehemu hiyo kuweza kuishi kwa amani sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vilivyoanzishwa vyote vitano havina shule, havina zahanati lakini vilevile havina miundombinu ya barabara wala maji. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri anayehusika ili nisishikilie mshahara wake ahakikishe kwamba, vijiji vilianzishwa kwa ridhaa yake anaviangalia kwa jicho la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala la afya ya mama na mtoto, tunayo changamoto kubwa sana na hata kwenye mapendekezo ya Bajeti ya Serikali ilionyesha kwamba, kweli bado tuna tatizo la vifo vya mama na mtoto. Hilo suala katika majimbo binafsi linatugusa sana lakini zaidi tunaguswa sana na suala la michango ya Bima ya Afya ile CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejitahidi sana kwa kadiri tunavyoweza tumehamasisha wananchi wanachangia Bima za Afya lakini wanakata tamaa wanapokwenda hospitali halafu tena wanaandikiwa wakanunue dawa. Wananchi wanakata tamaa na wanachoka kweli kweli. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ijizatiti katika eneo hilo, mwananchi anapolipa Bima ya Afya yaani CHF akienda hospitali amkute Daktari halafu apewe dawa asilazimike kwenda kununua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaingia kidogo kwenye suala la elimu; tuendelee kuishukuru Serikali kwa mpango wake wa kuanzisha maabara katika sekondari zote za Kata. Maabara zimejengwa kwa mfano, katika Jimbo langu maabara zimejengwa karibu kata zote 19 zinakaribia kumalizika, tumeshajenga kwa asilimia 70, asilimia 30 bado kumalizia finishing.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini changamoto tuliyonayo ni suala la umeme; hakuna maabara yeyote duniani inayoweza kuendeshwa bila umeme. Naomba sana Serikali iliangalie hilo ili hizo maabara tunazozijenga watoto wetu waweze kuzitumia kwa maana ya kufanya practicles ambazo zitawaletea tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la makusanyo ya ushuru au vyanzo vya mapato vya Halmashauri zetu; najua kwamba, kila Halmashauri ina mbinu zake za kuandaa na kutekeleza vyanzo vyake vya mapato kwa ajili ya kuongeza mapato. Katika Jimbo langu bahati nzuri tunapakana na nchi jirani ya Burundi kwa sehemu kubwa sana, tumeweka masoko kama mawili yamepakana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tuna changamoto, soko moja ambalo lipo sehemu ya Kibuye, kipindi kama hiki cha mvua halifanyi kazi yoyote kwa sababu linahitaji daraja na daraja hakuna. Kwa hiyo, hata wale ndugu zetu wa nchi jirani wanashindwa kuvuka kuja kufanya biashara na kile kilikuwa ni chanzo kizuri sana cha mapato. Hawa watu wa nchi jirani wanategemea sana Tanzania katika kufanya matumizi mbalimbali; kwa hiyo wanatuletea sana pesa. Tunaomba sana Serikali iangalie suala la daraja katika soko la ujirani mwema la Kibuye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa vilevile kuongelea hizi pesa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji, tunaomba sana hizi pesa Serikali itupe mwongozo. Kiukweli ni kwamba, kila wakati ninapokwenda jimboni, kila ukienda kusalimia wananchi wanakuuliza swali hilo hilo. Mheshimiwa pesa ile milioni 50 imeshafika? Kila kijiji unachokwenda kusalimia wanakuuliza hilo swali. Tunajua kwamba, hazijafika lakini sasa kumbe tunahitaji mwongozo wa namna ya kuzigawa na mwongozo uwe wazi kweli kweli, vinginevyo itatuletea sana shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la Ofisi ya Rais, Utawala Bora; Ofisi ya Rais, Utawala Bora wameanzisha Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma. Nakiri kwamba, hicho ni kitu kizuri sana kwa sababu kimeanzishwa muda kidogo lakini ukweli ni kwamba, bado maslahi na mishahara ya watumishi wengi bado ni duni. Wakati mwingine ndiyo inasababisha hata watumishi washindwe kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuingia hata kwenye tamaa za kudai rushwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana hii Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma iwezeshwe sana ili iweze kufanya kazi zake za kuhudumia watumishi ili waepukane na tamaa ambazo zinaweza zikawaingiza katika matatizo, lakini vilevile wajiepushe na tamaa ambazo zitaliingiza Taifa katika hasara kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora vilevile tunapata shida sana na TASAF. Nikiri ukweli kabisa kwamba, wakati wa kampeni mimi nilipata shida sana, wiki mbili za mwisho zile pesa zilitoka kwa wananchi. Wakati fulani wa kampeni kuna mwananchi amekuja amelewa anasifia kweli Serikali kwa kugawa hizo pesa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kabla hata sijamaliza hizo kampeni akatokea mwananchi unamwona kabisa hali yake ni duni amefika pale analalamika kwamba, yeye hajapewa pesa, ilikuwa ni mtihani mkubwa sana lakini nashukuru Mungu kwamba, yale yalipita. Tunaomba sana TASAF watusaidie sana kurekebisha hilo suala. Wanaostahili kupewa kaya zile maskini ndiyo zipewe hiyo pesa ya kuwawezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niongelee suala lile la TAKUKURU, hii ni taasisi ambayo katika hali ya kawaida inatakiwa iwe rafiki sana na wananchi ili iweze kutekeleza majukumu yake. Inapotekeleza majukumu yake sio rahisi kwamba, itafurahisha watu wote, kuna wakati mwingine hawawafurahishi watu wote, kwa hiyo wanajenga urafiki lakini wakati huo huo wanajenga uadui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufanyike utaratibu hawa Maofisa wa TAKUKURU kila baada ya miaka mitatu basi wawe wanabadilishwa vituo ili wasichukiwe sana na wananchi wakatengeneza uadui lakini vilevile wasizoeane sana na wananchi wakashindwa kufanya kazi yao ya kupambana na rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.