Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, maboresho yanayohitajika katika mfumo wetu wa udhibiti wa Sekta ya Uchukuzi; kama ilivyo katika nchi zote duniani, mfumo wetu wa udhibiti wa nchi, kiuchumi, kiusalama na kiulinzi umegawanyika gawanyika vipande vipande vilivyo chini ya utitiri wa mamlaka za udhibiti zilizo chini ya Wizara mbalimbali kuendana na eneo lake la udhibiti zenye majukumu yanayoingiliana, kutegemeana, na wakati mwingine hata kusigana/kukinzana na kutengeneza ombwe la udhibiti katika maeneo fulani fulani. Hali hii imepelekea kuwepo kwa changamoto ya namna sahihi, rahisi na fanisi ya kuzipanga mamlaka hizo ili kuziwezesha sio tu kuifanya kazi ya udhibiti iliyokasimiwa kwanza, bali pia kuyafikia malengo yaliyokusudiwa kwa ufanisi uliokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, sekta ya uchukuzi wa abiria na mizigo ni miongoni mwa sekta za uchumi wa nchi yetu zinazoathiriwa sana na changamoto hiyo. Kwa vile sekta hii ni sekta mwezeshaji wa sekta zingine za uchumi wa nchi athari zinazoikabili haziishii kudumaza mafanikio katika sekta hii pekee, bali kupelekea/kuchangia kudumaza mafanikio katika sekta zingine za uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na kuathirika sana na changamoto ya ufanisi katika udhibiti ni udhibiti wa usafirishaji mizigo hatari; usafirishaji mizigo hatari unasimamiwa na mamlaka lukuki kufuatana na ama aina ya bidhaa au aina ya hatari iliyomo katika bidhaa husika. Mfano rahisi wa kuielezea hali hii ni usafirishaji wa petroli kwa njia ya barabarani unaoangukia katika mamlaka za udhibiti zisizopungua nne.

Mheshimiwa Spika, kwa vile petroli ni nishati, na usafirishaji petroli ni sehemu ya mchakato wa usambazaji petroli, EWURA ina jukumu la kisheria la udhiniti wa usafirishaji petroli. Aidha, kwa vile petroli ni kemikali hatari (tena sana), GCLA ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji petroli. Kwa vile petroli huagizwa kutoka nje ya nchi kupitia usafiri wa majini, TASAC ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji petroli mpaka inaposhushwa bandarini; na kwa vile petroli husambazwa nchini kwa kupitia usafiri wa barabarani na relini, LATRA ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji petroli mara inapoondolewa bandarini.

Mheshimiwa Spika, mfano mwingine wa kuielezea hali hii ni usafirishaji wa vifurushi na vipeto kwa njia ya barabarani unaoangukia katika mamlaka za udhibiti zisizopungua nne: -

a) Kwa mujibu wa Sheria iliyoianzisha TCRA, udhibiti wa usafirishaji vifurushi na vipeto ni jukumu la TCRA.

b) Kwa vifurushi na vipeto vilivyofungasha kemikali hatari, GCLA ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji vifurushi na vipeto hivyo.

c) Kwa vifurushi na vipeto vilivyofungasha vimelea hatari, Wizara ya Afya ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji vifurushi na vipeto hivyo.

d) Kwa vile vifurushi na vipeto hivyo vinasasafirishwa kwa njia ya barabarani (mara kwa mara kwa njia ya mabasi), LATRA ina jukumu la kisheria la udhibiti wa usafirishaji vifurushi na vipeto hivyo.

Mheshimiwa Spika, uwepo wa mamlaka zaidi ya moja, sio tu unaleta mkanganiko unaozorotesha shughuli ya udhibiti, bali pia unachangia sana katika kuzalisha urasimu na gharama kwa wasafirishaji zisizo za lazima. Hivyo basi, ningependa kupendekeza maboresho yafuatayo katika mfumo wetu wa udhibiti wa usafirishaji mizigo hatari: -

Kwanza tutunge sheria moja ya udhibiti wa usafirishaji mizigo hatari itakayosimamiwa na mamlaka moja ya udhibiti itakayozijumuisha kwa pamoja sheria-ndogo, kanuni, na taratibu za udhibiti za hizo mamlaka mbalimbali za udhibiti. Tunaweza tukawaiga wenzetu Wamarekani ambao pamoja na kuwa na utitiri wa mamlaka za udhibiti kama tulizonazo sisi, jukumu la udhibiti wa usafirishaji mizigo hatari unaangukia katika idara ya usafirishaji (department of transport), na unasimamiwa na sheria moja; 49CFR (49th Code of Federal Regulations).

Pili, Kitengo cha Udhibiti wa Usafirishaji Vifurushi na Vipeto kwa njia ya barabarani kilichopo TCRA kwa sasa kihamishiwe LATRA kwani kwa muktadha wa lugha ya usafirishaji/usambazaji, vifurushi’ na vipeto ni majina-rasmi tu ya mizigo midogo. Taratibu zake za udhibiti hazitofautiani sana na zile za mizigo mikubwa.