Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nina maeneo mawili ya kuchangia katika hoja hii kama ifuatavyo: -
Kwanza, Serikali imalize mgogoro kati ya wananchi wa Mtaa wa Baruti na TANROADS.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu kumekuwepo na mgogoro kati ya wananchi wa Mtaa wa Baruti na TANROADS kufuatia uamuzi wa TANROADS kuwataka wananchi wapishe eneo la makazi yao kwa ajili ya upanuzi wa barabara husika. Madai ya muda mrefu ya TANROADS ni kuwa wengi wa wananchi hawa walishalipwa fidia. Hata hivyo wananchi wanapinga madai haya. Historia fupi ya mgogoro huu ni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, miaka ya 1990 barabara hii ilikuwa na lanes mbili, moja ikiingia na moja ikitoka. Baadaye Serikali iliona haja ya kupanua barabara hii. Hivyo wananchi waliofuatwa na barabara walilipwa fidia na kupewa maeneo ya kujenga katika maeneo ya Mbweni na Mabwepande. Hii ndio asili ya Mtaa wa Ubungo kule Mbweni na Mtaa wa Manzese kule Mabwepande.
Mheshimiwa Spika, mgogoro uliopo kwa sasa ni pale Serikali ilipoamua kupanua tena barabara kuwa njia nne kwa kila upande. Katika hatua hii ndipo ilipowakuta wananchi. Hawa ni wananchi ambao wamekutwa na barabara inayopanuliwa na baadhi yao wameisha katika maeneo husika kwa zaidi ya miongo mitatu.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 (hususani kifungu cha 3b) ipo wazi kwamba; katika hatua zozote za kuendeleza ardhi ni muhimu “kuhakikisha kuwa haki za wakazi waliokaa muda mrefu zinalindwa….”
Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali imalize mgogoro huu ili wananchi waishi kwa amani na kufanya shughuli za maendeleo na wakazi wa maeneo husika wapewe haki zao kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali itekeleze ahadi ya muda mrefu ya kujenga barabara ya Kimara – Mavurunza – Kinyerezi.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana wakati wa mjadala wa Wizara hii mimi na Mbunge mwenzangu wa Jimbo la Segerea, Mheshimiwa Bonnah Kamoli, tulizungumza kwa sauti kubwa sana kuhusu umuhimu wa barabara ya Kimara -Mavurunza - Kinyerezi yenye urefu wa kilometa saba na ambayo ipo chini ya TANROADS, niliamini Waziri alituelewa, na tangu mwaka jana na mwaka huu tumezunguka ofisi zote husika, zikiwemo kwa CEO wa TANROADS na Katibu Mkuu wa Ujenzi, Engineer Aisha Salim. Aidha, tumezungumza na Waziri na Naibu Mawaziri mara nyingi. Wote hawa walituahidi kwamba mwaka huu barabara hii ingeingia katika bajeti na ingeanza kujengwa. Na kweli tumeona barabara katika randama. Lakini sasa ndio imetengewe shilingi bilioni moja kwa kilometa tatu?
Mheshimiwa Spika, tangu lini bilioni moja ikajenga kilometa tatu za lami? Halafu Waziri amezungumzia kufanya feasibility study. Hili ni jambo ambalo tuliambiwa lilishafanyika tayari, hatuwezi kueleweka kwa wananchi. Naomba Waziri atakapohitimisha hoja yake atueleze ni lini barabara hii itaanza kujengwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. Nitasubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri kabla sijaamua kuunga mkono hoja.