Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba nami nianze kuunga mkono hoja hii. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana katika Bunge lako Tukufu ili kuhitimisha hoja ya Mheshimiwa Waziri ambayo aliiwasilisha jana. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kwa nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Waziri wangu, Mheshimiwa Prof. Makame Mnyaa Mbarawa kwa jinsi ambavyo anaiongoza Wizara, nasi wengine kwa kweli tunajivunia kufanya kazi chini yake na kupata uzoefu ambao mwenzetu kwa kweli amebobea katika Wizara hii. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuishukuru familia yangu ambao uwepo wao ndiyo unanifanya niwe na utulivu. Pia nawashukuru wananchi wote wa Jimbo la Ileje ambao wametulia na wanaamini nawawakilisha vyema. Nami nasema kwa kweli ninawakilisha vyema na wananipa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu chini ya Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso; Makamu Mwenyekiti, Mama yangu Mheshimiwa Anne Kilango kwa jinsi ambavyo walichambua bajeti hii ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawashukuru Wabunge wote wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa michango yao. Baadhi ya hoja naamini zitatolewa ufafanuzi na Mheshimiwa Waziri, lakini mimi nitatoa ufafanuzi wa baadhi ya hizo hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitanabahisha kama Rais ambaye amedhamiria kwa dhati kuifungua Tanzania. Anaifunguaje Tanzania hii? Kuna vipaumbele kadhaa ambavyo Mheshimiwa Rais anavifuata. Kwanza ni kuteleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi inaelekeza tufanye nini? Kuunganisha Makao Makuu ya Mikoa kwa lami, kuunganisha nchi na nchi, bandari zetu, barabara za kimkakati, kupunguza misongamano katika majiji na miji na pia kupeleka barabara za lami za ulinzi katika Tanzania. Kinachofuata baada ya kukamilisha huo mkakati, itakuwa ni kuunganisha wilaya zote na makao makuu ya mikoa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba kitu ambacho kinafanyika na Wizara, kwanza nikutengeneza barabara ya mzungunguko wa nchi nzima kuanzia Mtwara, Songea, Nyasa, Kyela, Ileje, Tunduma, Sumbawanga, Mpanda, Uvinza na Kigoma. Ukitoka Kigoma unakwenda Manyovu, unakwenda Kasulu ama unakwenda Nyakanazi unakwenda mpaka Rusumo – Bunazi - Omurushaka – Murongo; unarudi Omugakorongo unakwenda Kyaka, Bukoba; unarudi Lusaunga, unaenda Geita - Busisi kwenye daraja letu kubwa unavuka unaenda Kigongo - Mwanza – Musoma; Musoma - Nata unaingia kwenye Mbuga, unakwenda Arusha; Arusha unazunguka Mlima Kilimanjaro kwa lami, unakuja Himo unaweza ukaamua kwenda Same, ukaenda kwa Mheshimiwa Mama Kilango sasa ama Korogwe, unaenda Tanga; Tanga – Pangani – Makurunge – Bagamoyo - Dar es Salaam – Mkuranga - Lindi, uko Mtwara tayari kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hivyo vipande, kipande ambacho hakina mkandarasi sasa hivi, lakini viko kwenye hatua katika hizo nilizozitaja ni kutoka Kyela kwenda Ileje, lakini soon tutatangaza, alichosema kuanzia Mpanda kwenda Mishamo, mkandarasi yupo na tunategemea kupata fedha kutoka Mishamo kwenda Uvinza hadi Kanyani. Kasulo kwenda Bugene tayari tuna mkandarasi yuko pale, kwa kaka yangu Bilakwate soon Mheshimiwa anakwenda kuandika mkataba. Ukitoka Murongo kuja kwa Omugakorongo tayari tuko kwenye hatua za manunuzi. Mheshimiwa Rais ameamua kuifungua nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema nitatoa mfano mmoja ni namna gani Mheshimiwa Rais anakwenda kupunguza misongamano katika miji na hasa majiji. Nitaongelea Jiji la Mbeya ambalo waliopita kwa kweli ni mtihani kwa sasa. Mheshimiwa Rais kwanza alitoa kilometa 29. Ulikwenda ukasema barabara inaning’inia, inaishia Ifisi, kwa nini isifike airport? Mheshimiwa Rais anaongeza kilomita nne, ziko kwenye manunuzi. Pia ameirudisha kutoka Uyole kuja Mlima Nyoka, badala ya 29 sasa ni 37. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mji wa Mbeya ni mfinyu, wananchi wa Mbeya waelewe kwamba ile barabara ambayo inapitika sasa itakuwa ndiyo diversion. Kwa hiyo, kulia zinajengwa barabara mbili na hiyo barabara ya sasa baadaye ndiyo itatumika kama barabara ya mwendokasi kwa Miji wa Mbeya. Barabara yote sehemu kubwa itawekwa taa pamoja na vivuko na kwa watembea kwa miguu. Huyu ndio Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyotaka kuipanga miji yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sitaki kuongelea Dodoma, wanaotembea wanaona kinachofanyika. Barabara kwa Dodoma tuna mzunguko wa nchi ambao tunajengwa, tuna mzunguko wa kati, tuna mzunguko wa ndani. Huo ndiyo utakuwa Mji wa Dodoma, lakini kwa kaka yangu hapa tutajenga Songea Bypass. Kwa African Development kwa fedha ya World Bank. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tu niseme baadhi ya mambo ambayo yanafanyika. Hapa katikati, barabara za EPC ambazo zinatembea hapa katikati kuanzia Songea kwenda kwa kaka yangu Mgungusi pale Malinyi mpaka Ifakara tunakuja mpaka Mikumi, mpango sasa ni kujenga barabara ya kutoka Mikumi kuja Kilosa kwa kaka yangu Mheshimiwa Profesa Palamagamba ili mtu akitoka Songea anakuja Dodoma anatoka Mikumi anakuja Kilosa anakuja Dodoma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutoka Kongwa – Kibaya - Orkesumet kwa kaka yangu Mheshimiwa Ole-Sendeka mpaka Arusha, lakini tunaanzia Kiberashi tunakuja Kibaya - Chemba – Kwamtoro – Singida, barabara ya Tanga ameishaifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unavyoona magogo yote haya yanatoka Mgololo, EPC + F inaanzia Mafinga kuchukua ambako mpaka sasa hivi ni barabara ya changarawe kuijenga kwa kiwango cha lami kwa kutumia mtindo huu wa EPC + F. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kaka yangu Mheshimiwa Kuchauka alisimama, Mheshimiwa Ungele alisimama, kaka yangu wa Nachingwea alisimama. Barabara kutoka Masasi - Nachingwea hadi Liwale inakwenda kujengwa kwa EPC + F. Tuna barabara ambayo nataka niwahakikishie ndugu zangu wa Mtwara; Mnivata – Tandahimba – Newala – Masasi yenye kilomita 160, lot mbili; Mnivata hadi Mitesa, Mitesa hadi Masasi, saa yeyote mkataba utasainiwa. No objection imeshatolewa, kwa hiyo, tunakwenda kufungua pia huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna Barabara ya Igawa kwenda Tunduma, EPC + F na katika Mkoa wa Mbeya kutakuwa pia na Bypass ambayo itaanzia Uyole hadi Songwe ili magari makubwa hayo yasipite hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi wanataka nitaje barabara zao, lakini naomba nitaje barabara moja ambayo sisi kama Wizara tunaambiwa katika barabara zote zile kubwa hasa trunk road ambayo imebaki ndefu ni barabara ya kutoka Mbalizi – Mkwajuni – Makongorosi – Rungwa. Ukifika Rungwa itaenda Ipole kwa kaka yangu Mheshimiwa Kakunda ama unakuja Itigi. Hii Mheshimiwa Waziri amesema tutaitafutia utaratibu maalum, japo tumeanza kuijenga upande huku na kutoka Itigi kuja huku, Makongorosi kuja huku, lakini hilo ndilo eneo ambalo tukishajenga tutakuwa tumeunganisha sasa kusini kwenda kaskazini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini? Anachokifanya sasa hivi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimezungusha hizo Barabara, lakini ukitoka Nyasa – Mbinga – Songea - Njombe, utaamua ukitoka Njombe uje Iringa, unakuja Dodoma; Dodoma unaweza ukaamua kwenda Kongwa ama ukaenda Babati huko Arusha, unatoka Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo ukitoka Dar es Salaam kwenda Kigoma sehemu pekee ambayo sasa unaweza ukatembea kwa vumbi ni kati ya kaeneo kanaitwa Chagu – Kaizilava, bado kama kilomita 13 na Uvinza – Malagarasi ambapo wakandarasi wako site. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lile eneo ulilosema, sasa hivi tunatoka Mpanda – Luhafwe, Lohafwe – Mishamo. African Development Bank sasa hivi tupo na mpango watukamilishie barabara hiyo kutoka Mishamo hadi Uvinza. Kwa kweli tunakwenda vizuri sana kwenye miundombinu. Wanaotaka ku-google waangalie, kwenye miundombinu Tanzania sasa hivi ni wangapi? Ndiyo maana Mheshimiwa Rais hakupata hiyo tuzo kwa bahati mbaya, ni kwa sababu ya hii kazi. (Makofi)
SPIKA: Nadhani makofi hayo yanaashiria kwamba Waheshimiwa Wabunge hawana swali la nyongeza, wamesikia maelezo ya barabara zote. Kwa hiyo, nadhani wamekusikia kwa kweli. Wamekusikia Mheshimiwa Naibu Waziri, nadhani haya makofi yatakuwa yanaashiria tumekuelewa, huna haja ya kuendelea kuzungumza. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, bandari zote sasa hivi mpango ni kuziunganisha kwa kiwango cha lami. Tuna bandari tumejenga Karema, tumeishatangaza tenda Mpanda – Karema, tuna barabara ya Lyazumbi kwenda Kabwe, ipo kwenye mpango, barabara ya kutoka Sumbawanga – Matayi hadi Kasanga imeshakamilika. Bandari hizi zote tumeshazijenga. Pia tuna barabara ambazo zinaunganisha na nchi ambazo bado. Moja ya barabara hizo ni Likurufusi – Mkenda barabara ambayo muda wowote kuanzia sasa hivi tutaitangaza kilomita 60 kuanzia Likurufusi hadi Mukulu kilomita 60. Mkataba upo tayari kwa ajili ya kusainiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara za kutoka Songea kuja kuunganisha na Mkoa wa Njombe ziko tayari kusainiwa na nyingine wakandarasi wako site. Sasa hivi tunajenga barabara kwa kiwango cha zege kutoka Njombe kwa maana ya Itoni – Lusitu – Mawengi kuja Manda. Barabara ni bora kabisa katika Afrika kwa kiwango cha zege. Tumeshakamilisha kilometa 50, tunaendelea kujenga kilometa 50. Tuna barabara ambazo zinaunganisha Mkoa wa Njombe kupitia Makete kuja Isyonje kuunganisha na Mkoa wa Mbeya, wakandarasi wako site wanafanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuna barabara inatoka Kyela - Katumba Songwe – Ngana – Ikinga – Ibungu – Isongole, mkandarasi muda wowote anakabidhiwa site aanze kujenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, lakini siyo kwa umaana, Mkoa wa Arusha tumepata maelekezo maalum. Baada ya Royal Tour kiwanja cha Lake Manyara kimeshalipiwa fidia, tunaanza kukijenga, lakini kutokea hapo hapo Lake Manyara ambapo ni Karatu, tunajenga EPC kutoka Karatu kuja Mbulu – Haydom – Idarafa – Sibiti – Lalago hadi Maswa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile Barabara ya Mto wa Mbu – Engaruka – Oldonyo Lengai – Sale hadi Waso ambapo unakuwa upo kabisa kwenye Klein’s Gate ya Serengeti tumeshakamilisha kilomita 40 na maelekezo yametolewa maalum kwenye maeneo yote korofi kuna kilomita kama 39 tujenge kwa kiwango la lami.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)