Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na uzima kusimama mbele ya Bunge lako tukufu. Vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa usomaji wake mzuri pamoja na Mheshimiwa Zahor pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Ulinzi na viongozi waliokuja wastaafu wa ulinzi na viongozi wanaoendelea na majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sina budi kwanza kuishukuru Wizara na SUMA - JKT kwa ujenzi wa Ikulu yetu nzuri, ya kileo ya kufahari, kwa pesa za kodi za Watanzania. Jengo linapendeza na wamelijenga kizalendo, lazima tuwapongeze. Mtu akifanya kitu kizuri ana haki ya kupongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitazungumzia ujenzi wa hanga la kuegesha ndege za jeshi. Kwa kweli walipewa Shilingi bilioni 11 na walitakiwa wajenge Dar es Salaam, Dodoma, pamoja na Chato Mkoa wa Geita. Wamejitahidi na kampuni iliyopewa M/S Simba Limited imefanya kazi nzuri. Tumekwenda kulitembelea la Dodoma liko katika hali nzuri na hata Kamati imeeleza hapo mbele kwamba wamejitahidi na lazima na wao pia kampuni ipongezwe na Wizara tuipongeze kwa kusimamia. Ingawa walianza mwaka 2021 wakatakiwa kumaliza mwanzoni mwa 2023, lakini hawajachelewa, kazi imekamilika, hongereni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakuja kwenye suala la ukusanyaji wa maduhuli. Ukusanyaji wa maduhuli kwa kweli kidogo wameshuka, lakini siyo sana na ilikuwa Ngome - Fungu 38, JKT - Fungu 39 pamoja na Wizara - Fungu 57 kwa pamoja zipatikane Shilingi bilioni 87.6, lakini kwa kweli hawakufikia lengo. Wamefikia Shilingi bilioni 85.1. Siyo mbaya, lakini hawakufika lengo.
Mheshimiwa Spika, kimsingi labda tuangalie pesa walizokuwa wakilipwa na Wizara ya Fedha zilikuwa chache tuseme ikawa ndiyo sababu, kwa sababu na Wizara ya Fedha safari hii imewabinya. Maombi ya fedha walizokuwa wakiwapa siyo waliyoomba. Wanasahau kama hiki ni chombo cha ulinzi, kinahitaji pesa. Usalama wetu na ulinzi wa mipaka yetu iko chini ya dhamana yao, na mtu hawezi kufanya kazi kama hana pesa. Sasa Waziri wa Fedha hili awe analiangalia. Makisio ya ulinzi yawe hayapungui, yanapelekwa kama wanavyoomba na matokeo yake tunayaona kwa sababu wanajeshi wetu ni wazalendo, wanafanya kazi zinavyopangwa kwa mujibu wa taarifa wanazozileta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu sera ya ulinzi wa Taifa (defense policy). Hii sera bado haijafanya kazi kwa sababu hatuoni hizo missions na visions zao walizozipanga na wanashindwa kutokana na kwamba hii sera haijatolewa tukajua. Unajua tu kwamba wameambiwa wafanye siku nyingi toka Bunge la Tisa. Wanasema hivi, Serikali ya Zanzibar bado haijatoa maoni yake, wadau; lakini Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari ilishatoa maoni na wadau tayari walishatoa maoni. Sasa kinachochelewesha nini hii sera haifanyi kazi? Bila ya sera huwezi kufanya kazi. Sera ndiyo itakayokupa mwongozo ukaweza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atuambie amekwama wapi? Kuna tatizo gani? Hii sera hadi hii leo mambo yote umeshapata, majukumu itakuwa yote umeshapata, kwa nini mpaka hii leo haijafanya kazi? Tunaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja utuambie umekwama wapi? Kama utataka upate msaada kwenye Kamati au kwenye Serikali tutajua vipi tunakuisaidia Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nazungumzia kwamba Wizara iongeze kasi ya utekelezaji wa mkakati na kupata hatimiliki za maeneo. Unajua maeneo ya jeshi kwa sasa na tunakoelekea siyo makubwa ya hivyo, yanahitaji kuongezwa, na nafasi hamna kwa sababu mshabanwa na wananchi wamejenga mpaka karibu na kambi. Mliambiwa mkae na Wizara ya ardhi ili mweze kuelewana, vipi mtaondoa, vipi mtapima, kwa sababu kuna kambi nyingine mpaka hii leo hazina hatimiliki.
Mheshimiwa Spika, ingawa leo wamezungumza hapa kwamba Kambi ya Chukwani tumeshalipwa, lakini ziko nyingi tu. Kuna Mtoni, kuna Ubago, zipo nyingi tu ambapo bado nina hakika hazina hatimiliki. Hiyo ni kwa upande wa Zanzibar. Sikwambii kwa upande wa Pemba, sikwambii kwa upande wa Mikoani. Naomba hili Mheshimiwa Waziri mliangalie mweze kujua kwamba ni vipi mtaweza kuvuka ili tusigombane na wananchi, tusigombane na Taifa na mweze kuwa na makambi yenu ambayo mnayamiliki na yawe hayana matatizo.
Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja. (Makofi)