Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia Wizara yetu hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri fupi ambayo imejaa mambo yote ambayo yanahusu masuala ya kijeshi. Kipekee nawapongeza watendaji wake ambao wameandaa hotuba hii kwa kweli wamefanya kazi nzuri na wameisoma na tumeifahamu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa upande wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kwa kuwashukuru sana kwa kuwapatia eneo wananchi wa Kimbini Kengeja, eneo ambalo linamilikiwa na Jeshi lakini kuwaruhusu wananchi kufanya shughuli zao pale kwa masharti ambayo wananchi wanayatimiza ya kutojenga, kutouza ili wafanye shughuli za kilimo na za kijamii tu, na wananchi kweli hakuna mgogoro na jeshi wanafanya shughuli zao kama kawaida, na yale masharti na matakwa ambayo wamepewa na jeshi wanayafuata.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikwambie kwamba wananchi wa Kengeja Mwambe wanashukuru sana jeshi la wananchi kwa kuwapatia eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar tuna school mbili ambazo zinamilikiwa na jeshi. Kuna School ya Nyuki iliyopo kisiwa cha Unguja na na School ya Ally Khamis Camp iliyopo Vitongoji Chakechake Pemba. School hii ya Ally Khamis Camp ni miongoni mwa school zinazofanya vizuri sana kwa upande wa Pemba na hata kwa Zanzibar. Inafanya vizuri kwa upande wa msingi, na pia inafanya vizuri kwa upande wa sekondari. Nilikuwa naomba tu hata Mheshimiwa Waziri, najua hana muda mrefu katika Wizara hii, lakini afanye jitihada za makusudi za kufika Kisiwani Pemba na kwenda kuikagua school hii aone jinsi watoto wanavyofanya vizuri katika masomo yao na ukakamavu ambao wanao, na matokeo bora ambayo wanayapata katika kila mwaka kwenye mitihani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri atambue kwamba, skuli hii ina changamoto ya mabweni ya wanafunzi wa kike na wa kiume, ili wanafunzi wafanye vizuri lazima wapate mahali pazuri pa kusomea. Ningeomba Mheshimiwa Waziri atenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika skuli ile ili watoto waendelee kufanya vizuri na kulijengea heshima Jeshi la Wananchi, lakini pia na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, katika Kambi ya Jeshi la Wananchi katika eneo la Uwanja wa Ndege, makazi yao kwa kweli siyo mazuri. Wanajeshi wale wanafanya kazi kwa uzalendo mkubwa sana kama lilivyo Jeshi lenyewe, na yale maadili yao ambayo wanayo, lakini kwa kweli yale majengo yaliyoko katika eneo lile la uwanja wa ndege hayaridhishi kabisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe kwamba, katika bajeti yako siyo kambi kubwa sana lakini ni ulinzi mkuba kwa uwanja wetu wa ndege hasa kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar sasa hivi miongoni mwa miradi yake mikubwa ni kuutanua uwanja wetu wa ndege wa Pemba ili ndege kubwa ziweze kutua. Sasa kwa style ile ya nyumba zile au ofisi zile au kambi ile ya jeshi kwa kweli, haileti picha nzuri.
Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri utakapofanya safari yako upite huko uone. Najua kwamba, Jeshi lina maadili, hawawezi kila taarifa wakazitoa, lakini hili kwa sababu wanatulinda nasi tulioko humu tunawatetea, ni vema ile kambi nayo ikafanyiwa ukarabati mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo alilieleza katika ukurasa wa 14 la kuendelea kutoa huduma za afya kwa Maafisa, wapiganaji na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Ninakiri kwamba, katika kisiwa chetu cha Pemba kuna hospitali kubwa ya Jeshi ambayo inatuhudumia wananchi wengi, lakini hospitali hii ina upungufu wa vifaatiba. Ameeleza hapa kwamba, wanao mpango wa kununua vifaatiba, kaviorodhesha, ukiangalia katika ukurasa wa 14 utavikuta. Nimuombe Mheshimiwa Waziri na ile Hospitali ya Jeshi ya Vitongoji tunaomba na wao wapelekewe vifaa hivi ili huduma zile za tiba tuweze kuzipata vizuri pale Jeshini na kwa nidhamu nzuri ambayo tunaipata kutoka Jeshini.
Mheshimiwa Spika, kuna jambo jingine ambalo Jeshi la Wananchi Tanzania kwa upande wa Zanzibar limefanya ni jambo kubwa sana na ni jambo la kushukuru sana. Jeshi hili wamefanya uwekezaji mkubwa katika eneo la Migombani, miongoni mwa uwekezaji ambao wameufanya ni ujenzi wa kituo cha mafuta pale maeneo ya Migombani, kituo ambacho kinatoa huduma masaa 24 pamoja na huduma za kifedha ambapo wananchi wa Zanzibar wanaamini kwamba, time yoyote ambayo unahitaji kupata huduma pale Jeshini unazipata. Kwa hiyo, tuwashukuru na tunawapongeza sana kwa kazi hii kubwa ambayo wameifanya, ni uwekezaji mkubwa na wanaendelea kujenga maduka mengi na makubwa ya kisasa kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kengele tayari ya kwanza imeniashiria huko na umeshanionesha, hata niombe dakika moja nizungumzie kidogo tu kwa upande wa JKT. Kwa upande wa JKT nao wanafanya vizuri na wanachukua vijana wetu hawa wa kujitolea, wanawajengea uzalendo na ujasiriamali. Ninaomba sana kwamba, katika kuwajengea ujasiriamali huu basi lazima kule JKT wajipange kwa vifaa ili watoto wetu wanapotoka kule, mbali ya kutegemea ajira hizi kupitia vyombo vya ulinzi na usalama na wao wakitoka waweze kujiajiri na wasikae tu mitaani na kusubiri kazi hizi za ulinzi. Vinginevyo hawa watu wamefundishwa uzalendo, wanaweza kutumia silaha vizuri, ndiyo sasa mara tunakuja kukuta hawa watu wanatumia silaha mitaani vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)