Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza naomba nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, kubwa kwa kuendelea kuiunga mkono Wizara hii pamoja na vyombo vyetu vyote kwa sababu yeye ndiye kiongozi wa majeshi haya na ndio mkuu wa ulinzi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake yote kwa sababu mara zote wamekuwa wakishirikiana vizuri na Kamati yetu ili kuhakikisha kwamba Kamati zinafanya majukumu yake kwa mujibu wa Kanuni zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi naomba kuchangia mambo machache sana, nikiamini kwamba Serikali itaweza kutusikia, kutusikiliza na kutekeleza. Kwanza naomba niwashukuru kwa sababu Serikali imeamua kuongeza asilimia kama moja nukta kitu hivi kwa ajili ya shughuli za Wizara yetu hii. Lakini ninaomba kuomba zaidi, tena kwa heshima kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, huko nyuma niliwahi kusema kwamba Jeshi ni chombo cha utafiti, Jeshi ni chombo cha ulinzi. Chombo hiki kinatulinda angani, kinatulinda ardhini, kinatulinda baharini na mipakani. Sasa pamoja na kwamba Serikali yetu inafanya jitihada kubwa za kuwaongezea uwezo, bado naiomba Serikali iendelee kutafakari kwa kina sana, kwa sababu kazi kubwa ya Jeshi letu ni kulinda mipaka yetu, period. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba sana, pamoja na kwamba Serikali imefanya kazi ya kuongeza lakini bado kwa sababu Jeshi hili halina pa kulia, Jeshi hili sehemu ambayo itaomba ipatiwe nyenzo za kufanyia kazi ikiwemo utafiti ni Bunge lako hili. Kwa hiyo ninaomba sana, kwa niaba ya Kamati yangu, lakini kwa niaba ya Bunge hili, tuombe sana Serikali itusikie na ituelewe kwamba tunahitaji Jeshi la kisasa, ambalo tutaliwezesha ili kazi yake iwe moja tu, ya kulinda mipaka yetu ili kuhakikisha kwamba Tanzania inaendelea kubaki kuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wakati tunasoma taarifa yetu pale, tulizungumzia hoja ya kuliwezesha Bunge. Moja miongoni mwa kuliwezesha Bunge Jeshi letu hili ni kuhakikisha kwamba linapata vitendea kazi lakini vilevile na sisi tunaendelea kusaidia kuhakikisha kwamba halitumii fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jeshi letu linapata gharama kubwa kwenye kulipa kodi. Sasa mimi naomba niliombe Bunge lako, na naomba niiombe Wizara, kwamba sasa wakati umefika wa kuhakikisha kwamba Jeshi letu linapatiwa msamaha wa asilimia 100 kwa vifaa vyake vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kama sikosei tunatafsiri vifaa vya Jeshi kwamba ni silaha, kwa maana ya risasi na mizinga; hapana, tunakosea. Huko nyuma Jeshi letu lilikuwa na msamaha fully kwa vifaa vyake vyote inavyotumia. Inawezekana yalitokea mapungufu kwa watu wachache, lakini tumeliadhibu Jeshi kwa kutokuona kwamba hata uzi wa askari ni silaha. Sasa ombi langu, naiomba Serikali, hasa Wizara ya Fedha, ituletee mabadiliko ya sheria ili kuhakikisha kwamba Jeshi tunalipa msamaha kwa vifaa vyake vyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kuitoza kodi Wizara ya Ulinzi ni sawasawa na kutoa pesa mfuko wa kushoto ukaweka kulia ukitegemea tija; haipo. Lakini pili, Jeshi hili ndilo linalotulinda, mimi sioni sababu ya kuwa na wasiwasi na chombo chetu halafu ukawapa nafasi baadhi ya watu pale bandarini wanakwenda kuchungulia Jeshi wameleta nini. Siyo kazi yetu vifaa vyetu kuchunguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama vifaa vyetu vimeletwa kama Jeshi, ombi langu, kwa sababu ndio wanaotulinda, tumewaruhusu na tumewapa fedha ya kununua vifaa hivyo, hatuna sababu ya kuendelea kuwatoza kodi Jeshi. Ombi langu, watuletee sheria tuibadilishe, tena iletwe kwa hati ya dharura ili tuipitishe hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuendelea kwenye pointi yangu nyingine, kwamba pamoja na Serikali kuendelea kujitahidi bado naomba tuendelee kwa sababu sisi ndio tunaosimamia Wizara hii pamoja na nyingine mbili; bado tunahitajika kuhakikisha kwamba Jeshi letu hili, hasa kwenye suala la kuewezesha makazi yao na vifaa vyao, bado. Kwa sababu wenzetu hawa wanafanya kazi kubwa, ninaomba sana Serikali iendelee kuona namna gani tutaliongezea Bunge Jeshi letu hili ili makazi yao na vifaa vyao viendelee kuwa vya kisasa kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, sisi sote hapa ni wastaafu watarajiwa. Sote hapa kwa njia moja au nyingine ama tutastaafu kwa muda ukifika au tutastaafishwa na Mungu kwa sababu hatma ya kufa pia ipo. Sasa ninaomba basi, wale wenzetu wote ambao wamestaafu au wale ambao wametangulia mbele ya haki lakini wao wenyewe au wale warithi wao bado hawajapatiwa yale mafao yao, ninaomba sana, kwa sababu umepoteza mzazi au mlezi halafu yale mafao unapata usumbufu. Si kwa sababu Jeshi hawapati, hapana, ni kwa sababu bado Wizara ya Fedha haijatekeleza hoja ya kuwapa fedha ili waweze kuwalipa waliostaafu na waliofiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba wenzetu hawa, hasa Wizara ya Fedha, wajue kwamba Jeshi ni chombo cha kujitolea. Sisi kama Serikali, kama Taifa, hatuna cha kuwalipa Jeshi ambao wametoa roho zao na nafasi zao kwa ajili yetu. Ninaomba sana tuwathamini, tuwalinde, kuwalinda wao ni pamoja na kulinda haki zao na waliowaacha ili waweze kujenga Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)