Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hii Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu, ambaye ndiye kiongozi wetu Mkuu.

Mheshimiwa Spika, lakini nampongeza na Mheshimiwa Waziri, CDF wetu pamoja na vikosi vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa na nzuri ambayo mnaifanya kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa tulivu na inaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, mimi ninayo maombi mawili na ushauri mmoja tu kwa ufupi. Ombi la kwanza linahusiana na wananchi wangu wa Kata ya Buhare kwenye Mtaa wa Mgalanjago. Wale wananchi kwenye hili eneo vilevile kuna eneo la Jeshi; lakini mnamo mwaka 2008 Jeshi liliweza kuongeza eneo ambalo walimega kwenye maeneo ambayo wananchi wangu walikuwa wanjipatia riziki, pale walikuwa wanafanya shughuli zao, na wakawa wameahidi kwamba watalipwa fidia. Sasa mchakato huo umeendelea kusema kweli mpaka sasa hawajapata fidia.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, hawa watu wako kama 26 na barua yao ninayo hapa, naomba mhudumu aje aichukue akupatie hapo ili tuweze kuhakikisha kwamba basi hawa ndugu zetu wa Buhare ambao wanahitaji wapate hiyo fidia yao waweze kupata fidia ili waweze kuendelea na maisha yao kama kawaida.

Mheshimiwa Spika, la pili vilevile ni ombi ambalo bahati nzuri nilishakufikishia Mheshimiwa Waziri. Sasa nikuombe basi, kwamba kule eneo la Bukanga mnamo mwaka 1979 tulipata bahati ya kuwa na ulinzi pale, Jeshi lilichukua maeneo pale kwa hiyo wakahamia pale. Lakini katika yale maeneo waliyokuwa wamehamia, kumbe wakati wanapewa walipewa maeneo ambayo ni makubwa na mengine hawakuyafahamu.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba wao kwa sababu hawakuyafahamu, wale wananchi waliishi katika baadhi ya maeneo. Sasa miaka imekwenda, Jeshi hawajui kama ni ya wale lakini na wale wananchi wanajua ni maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kilichokuja kutokea miaka mitatu iliyopita watu wa MUWASA wakaja kuomba eneo la kujenga tenki la maji, sasa sisi kama wahusika wa eneo hilo tukawapa ili wajenge tenki la maji. Wakati wanaendelea ku-demarcate maeneo haya ndiyo wakagundua kwamba lile ni eneo la Jeshi. Tayari kuna familia au kaya zaidi ya 60 zimeshakaa pale; nadhani hilo linahitaji sana busara ya Serikali ili iweze kwenda na kuona kwamba wale watu tunawafanyaje, kwa sababu Jeshi hawakufahamu na wale wananchi nao hawakufahamu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, ombi langu, nadhani hilo nilishakufikishia, kwamba hebu twende wote pale Musoma uende ukaangalie hali halisi halafu tushauriane tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuwasaidia wale wananchi ambao wamekaa kwenye hilo eneo ambalo ni pamoja na huruma ya Serikali kuwapatia ili waendelee kuishi basi maisha yao yaweze kuendelea salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya hiyo, mengine mawili madogo, ninapenda tu kufahamu lile Shirika letu la Nyumbu ambalo ndiyo lilikuwa shirika lililoanza kuwa linatengeneza magari, siku hizi hatulisikii kabisa. Kwa hiyo ninapenda kupata tu maelezo kwamba hivi lile shirika letu limekufa au bado linaendelea.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, niseme la mwisho ambalo ni ushauri wangu, kwamba tunatambua na huwa tunaona hata kule kwetu wakitangaza tu kwamba sasa kuna nafasi za Jeshi, JKT, wako vijana zaidi ya 1,000 wanakwenda pale kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya kuanza kujiandikisha na kuhakikisha kwamba wanapambana ili wapate nafasi ile.

Mheshimiwa Spika, kinachotokea ni kwamba wale vijana watakaochukuliwa hata katika nchi nzima unakuta wanakaa mwaka au miaka miwili baadaye baadhi yao ndio wanapata nafasi ya kwenda katika vyombo vingine au katika majeshi mengine. Lakini vijana wengi baada ya miaka miwili tafsiri yake ni kwamba wanarudi nyumbani.

Mheshimiwa Spika, sasa wakirudi nyumbani, wale vijana bahati nzuri walishajifunza ukakamavu, walishajifunza ulinzi na mambo mengi ya kuwafanya waendeleze maisha yao, lakini kwa bahati mbaya sana sasa wanarudi kule hawana kazi ya kufanya. Kwa hiyo mimi nilidhani kwamba kuna haja kubwa ya Serikali kuangalia kwamba vijana hawa ni rasilimali kubwa ambao wakitumiwa vizuri kwanza wanaweza kusaidia sana kuendelea kuijenga nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nilidhani sasa hata kwenye mpango kama huu wa BBT, huu wa kilimo, ni kwa nini Serikali isitoe fedha za kutosha ikawapa JKT ili wale vijana watakapomaliza yale mafunzo badala ya kuwatupa nyumbani wapewe maeneo ya kujiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tena bahati nzuri kwa sababu wao walishafanya mazoezi, ni vijana wakakamavu, wanaweza wakapewa kama mkopo hata kama ni kilimo hicho, wakapata fedha na baadaye wakarudisha ili wale wengine wanaokuja, intake inayofuata, nao waweze kusaidika na mpango huo.

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo tunadhani kwamba kwanza itasaidia sana kupunguza tatizo la ajira, lakini vilevile itasaidia sana kujenga uchumi wa nchi kwa sababu nchi nyingi zinazotuzunguka, majirani zetu, ukienda Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi, wote wana mahitaji makubwa ya chakula. Sasa kwa sababu maeneo tunayo, vijana tunao, ardhi tunayo, kumbe tunaweza kuleta ajira kwa vijana wetu lakini vilevile tukawa tumesaidia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani hili ni vizuri Wizara lakini na Serikali ingelipa kipaumbele, kwa sababu moja wapo ya majukumu makubwa ya Serikali yoyote ile ni kuhakikisha kwamba watu wake wanapata ajira. Kwa hiyo hiyo nayo ni avenue nyingine ambayo tunadhani tunaweza tukawasaidia vijana wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)