Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ussi Salum Pondeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chumbuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nitumie nafasi hii kwanza kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii kuchangia leo hii katika Bajeti yetu hii ya Ulinzi.

Mheshimiwa Spika, vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi letu hili la Wananchi wa Tanzania, mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Vilevile nitumie nafasi hii kumpongeza pia Rais wetu wa Zanzibar kwa majukumu yake na ushirikiano ambao anautoa katika kuhakikisha amani inaendelea kutawala katika nchi yetu, lakini katika kushauriana na Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni mama yetu Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza yale majukumu ya amani na ulinzi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii sasa kukupongeza wewe Waziri kwa jinsi ambavyo unafanya kazi katika nafasi hii muda mchache lakini jinsi gani umetufikisha hapa na umelifikisha hapa Jeshi letu hili katika kuongoza. Nakushukuru sana na tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, mimi leo hapa nataka nitoe ushauri ambao nahisi ukiuchukua ikikupendeza itatusaidia sana katika Jeshi letu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa kwanza ni katika kuhakikisha nafasi zile za ajira zinapotokea uliendeshe Jeshi kama ilivyo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani nafasi za ajira zinapotoka, umesema katika hotuba yako, nimekusikia, lakini unavyosema wewe na inavyochukuliwa haiko hivyo. Nina ushahidi, ukihitaji nitakupa, jinsi gani ambavyo hata mgawanyo wa ajira unapotoka katika Serikali yetu hi ya Muungano, tuna asilimia 79 kwa 21, lakini mgawanyo hauko hivyo, kama ambavyo washauri wako au watendaji wako labda wanakuelezea unakwenda sawa, lakini hauko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nimekuwa nikisimama mara nyingi nikiuliza maswali yangu kuhusu Wizara yako, ni jambo la mipaka ya makambi ya Jeshi. Hili umelizungumza kuwa mmeanza, umetuonesha mpaka picha kuwa mnapima. Lakini kiuhalisia mipaka bado ni jambo moja ambalo linasumbua sana baina ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na wananchi siyo kama Jeshi hawalipendi, Jeshi wanalipenda kwa sababu ni Jeshi lao na linafanya kazi vizuri, lakini sasa inapofika mipaka wakijenga tokea asili yao ilivyokuwa Jeshi wanasema sisi mpaka hapa, lakini hakuna mwenye hati. Jeshi tatizo kubwa ambalo lipo, lina makambi mengi hayana hati miliki, lakini wananchi wapo ambao wana hati lakini Jeshi kwa heshima yake au kwa nguvu zake ambazo ipo na tumeipa sisi, na ndivyo tunavyopenda Jeshi letu liwe lina nguvu, basi huwa linafanya mpaka mwisho wanavyotaka wao.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine ambalo nataka pia nikushauri. Kiwanda chetu cha Nyumbu kinafanya mambo mengi, lakini yote kwa yote, fedha hakipati kwa muda, lakini na Serikali haitoi fedha kukiimarisha Kiwanda chetu cha Nyumbu kuhusu vifaa vyetu vinavyoweza kutengenezwa pale.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nishauri, leo hapa sina haja ya kushika shilingi ya Mheshimiwa Waziri, kazi yangu kubwa ni kumshauri yale ambayo nahisi ana mapungufu katika Wizara yake ila na ni kuboresha ili jeshi letu liendelee kuwa bora. SUMA JKT wamefanya kazi nzuri na wamefanya kazi kubwa katika nchi yetu hii lakini tatizo lao nalo kama Kiwanda cha Nyumbu bajeti wanaomba na pesa wanazoomba hawazipati kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri, tukiziimarisha taasisi zetu mbili hizi Nyumbu na SUMA JKT tukiwapa fedha ambazo wanataka na kwa wakati basi zita-create hata ajira ambazo tumesema zipo rasmi na ambazo sio rasmi, basi wana uwezo wa ku- create, kwa sababu wamefanya mambo mengine ambayo sitaki niyarudie wachangiaji wengine wamesema hapa, mpaka Ikulu yetu ambayo tunajisifia sasa hivi kubwa, nzuri, lakini imefanywa chini ya usimamizi wa SUMA JKT na ni vitu ambavyo vinawezekana, lakini wakiwezeshwa ndio itaonekana. Sasa ni jukumu la Waziri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka labda nimshauri Waziri na ushauri wangu sio jambo kubwa sana, jinsi ambavyo zinavyotoka nafasi zile za vyeo, majengo, basi yatoke kwa uwiano na yatoke kwa wakati, lakini sana vyeo. Kuna maafisa ambao wanatoka kwenye JWT lakini wanafanya kazi katika SMZ ambao wamechukuliwa kwa ajili na wao ni Watanzania kama sisi, lakini unapofika wakati wa kuwa na wao wafikiriwe kwenye vyeo, kidogo wanasahaulika. Ningependa hili nalo Mheshimiwa Waziri alichukue kwa sababu yote hii inatokana na nini? Jeshi letu hili la Muungano linafanya kazi huku na huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu wa mwisho, ikimpendeza Mheshimiwa Waziri, Jeshi lina hospitali ya Bububu kule Zanzibar ambayo ndio hospitali kubwa na hospitali ya viongozi wa ngazi ya juu na ya mwisho ikitokea wamepata matatizo au wana shida yoyote hata Mawaziri kama huyu akija, basi hospitali yao ya mwanzo huwa ni ya Bububu ambayo ni ya Jeshi, lakini ukiingalia hali yake sio nzuri kabisa, ina hali mbaya inahitaji ukarabati mkubwa na vifaatiba, vile vile na hata yale majengo yake hayako sawa, yaani ukiangalia hadhi yake na ya Jeshi letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hospitali ile haviko sawa. Kwa hiyo, ushauri wangu nafikiri nitakuwa nimechangia pale ambapo Waziri anahitaji mchango wa sisi kama Wabunge, naomba leo mchango wangu uwe huu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono asilimia mia moja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)