Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa nichangie katika bajeti hii. Nianze kwa kumpongeza Waziri, kwa kweli nampa pongezi kubwa kwa sababu ya usikivu na uvumilivu na utendaji kazi katika Wizara hiyo, hongera sana. Pia nampongeza Katibu Mkuu Doctor Faraji Mnyepe kwa kazi kubwa anayofanya pamoja na watendaji wote katika Wizara hii. Watendaji hawa wanafanya kazi kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na Jeshi la Wananchi Tanzania, napenda kuwapongeza pia nao kwa utendaji mkubwa wa kazi zao uliotukuka na kwa gharama ya uhai wao. Hapa tulipo tunapumua na tuna starehe kabisa, lakini wenzetu wapo kazini wanafanya kazi bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye Amir Jeshi Mkuu kwa kutufanya tuwe na amani hii katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo na utendaji wote wa Jeshi wanaoufanya, lakini kwa kweli fedha wanayopata ya maendeleo ni kidogo. Laiti wangepata fedha nyingi za maendeleo wangefanya vitu vikubwa sana. Tumetembelea maeneo mengi ambayo wanafanyia kazi, wanafanya kazi kubwa, kwa weledi mkubwa na kazi zao zinaonekana ukilinganisha na maeneo mengine ambayo tunakwenda. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kutoa fedha wamepata asilimia 30.11 tu ya fedha za maendeleo. Kwa hiyo wangepata asilimia mia moja wangeweza kufanya kazi kubwa Hivyo, niombe Serikali itoe fedha kwa asilimia mia moja bila kuleta mzaha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jeshi letu ili liendane na ubora hasa kama ubora wa kimataifa, lazima bajeti yao inayotengwa, iliyoidhinishwa itolewe kwa wakati na itolewe kikamilifu. Ikitolewa hivyo, wanajeshi wetu watafanya kazi kwa uhakika, lakini pia Serikali ihakikishe kwamba maslahi ya wanajeshi wetu wanapata bila changamoto zozote.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano tunaona kuna wanajeshi ambao wanaenda kwenye kozi mbalimbali sasa wanakwenda kule wanatoa fedha zao mfukoni za mshahara, ningependa kama ingekuwa Jeshi linapata asilimia mia moja fedha za maendeleo, hawa wangeweza kulipiwa kwa sababu kuna kozi ambazo ni za kuongeza teknolojia na mambo mengine ambayo ni ya kiubunifu ambayo wanatakiwa waweze kulipiwa. Kwa hiyo Serikali isifanye masihara katika kutoa fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, niende katika mashirika yetu ya kimkakati, Nyumbu pamoja na Mzinga. Mashirika haya ni mashirika ya kimkakati yapo. Tumeona Nyumbu juzi tu hapa yametengeneza magari ya zimamoto na magari haya yamekuwa ni magari mazuri kabisa. Dunia yenyewe inatuona tumetengeneza magari ya zimamoto kwa fedha zetu hapa ndani. Sasa hawa Nyumbu wakiweza kupewa fedha za kutosha, wakiweza kupewa teknolojia za kisasa, wanaweza wakatengeneza vitu vingi vikiwemo vipuri mbalimbali wakauza ndani ya nchi na hata nje ya nchi. Wanaweza wakashirikiana na shirika la reli, wakasaidiana kuona wanatengeneza vipuri mbalimbali vikasaidia katika kupunguza mapato ambayo tunakwenda kununua katika nchi nyingine, tunatumia fedha za nje badala ya kutumia fedha zetu.

Mheshimiwa Spika, Nyumbu ilitoa mafunzo katika Nchi ya Uganda na Rwanda, lakini wenzetu wameshatupita,wako mbali kwa sababu ya kutekeleza azma ambayo Baba wa Taifa alikuwa anaitaka, kwa hiyo tuombe Serikali mweze kuchukulia kwa uzito, shirika hili linaweza likatutoa likatupeleka mbali sana kwa kutengeneza vifaa mbalimbali vya kisasa na hii itatusaidia kuweza ku-serve fedha za ndani badala ya kutumia fedha za nje kwenda kununua labda chuma nje, tunaweza tukasaidia Jeshi letu likapata Mchuchuma na Liganga wakaweza kuona kuna kitengo gani wawape ili waweze kuvuna chuma kile kikatumika kwenye Shirika la Nyumbu ambalo litasaidia katika kuleta masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna changamoto ya ikama ya watumishi. Kuna watumishi wapo lakini kuna wale ambao ni hitaji katika shirika hilo ambao wana sifa ambazo zinatakiwa katika shirika hilo. Nimwombe Mheshimiwa Waziri na niiombe Serikali waweze kupeleka watumishi wa kutosha katika shirika hilo ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, kwa sababu wanafanya kazi kwa weledi mkubwa. Ukifika pale unashangaa ni Tanzania ama sio Tanzania, ni kweli kabisa kwa kweli wenzetu wanajitoa, wanafanya kazi kwa weledi lakini tuwape fedha, Serikali wapeleke fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda katika suala la JKT; Jeshi la Kujenga Taifa ni jeshi ambalo linaweza likatusaidia sana kututoa katika hali ya kiuchumi hasa tukishirikiana na vijana. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa mawazo ya kuona kwamba vijana wanatakiwa kusimamiwa kimaadili na mambo mengine yoyote, lakini bila fedha bado ni changamoto. JKT wametengewa asilimia sita tu ya fedha za maendeleo, itafanya nini? Tumeona wanajenga majengo mazuri. Tumeona wanashindwa hata kupeleka vijana JKT wengi kwa kukosa fedha za kuwahifadhi pale. Kuna vijana wengi wanatamani kwenda Jeshi la Kujenga Taifa hapa Wabunge wengi tunapigiwa simu kutoka huko, tunaomba vijana waende, lakini Mkuu wa Jeshi anashindwa awaweke wapi, hakuna hata sehemu ya kuwaweka. Kwa hiyo fedha zikienda, fedha nyingi za maendeleo tunaweza tuka-accommodate vijana wengi kwenda katika Jeshi hilo lakini wakafanya kazi nyingi za kilimo, za kiuchumi na za kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri aangalie kabisa kwamba target kubwa katika fedha ya Wizara JKT inachangia asilimia 73.3, hizo ndio fedha zinazochangiwa na JKT. Pale ambapo wanachangia fedha nyingi na Serikali ione namna ya kuwekeza zaidi ili kuweza kuongeza fedha nyingi Zaidi, kama tutawekeza kwa Jeshi la kujenga Taifa. Nimwombe Mheshimiwa Waziri aweze kufanya hivyo kwa Jeshi letu la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwamba katika Jeshi la Kujenga Taifa kuna miradi ya kilimo ambayo inafanywa, lakini wanashindwa kuitekeleza kwa ukosefu wa fedha. Changamoto kubwa ni hiyo ya ukosefu wa fedha. Kwa hiyo niombe Serikali, Wizara ya Fedha wapeleke fedha kwa Wizara hii, hatuwezi kuwa salama bila ulinzi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. (Makofi)