Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pia kuchangia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwanza naunga mkono hoja ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, lakini pia naunga mkono Taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Spika, duniani kote unapopima uwezo wa taasisi kwa maana ya uthabiti na uimara, basi kuna uhusiano wa moja kwa moja na uimara na uthabiti wa mkuu wa taasisi husika. Kwa mantiki hii nichukue nafasi hii kumpongeza Amir Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maboresho mbalimbali ambayo anayafanya kwenye Jeshi letu pamoja na vyombo vya ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kiwango kikubwa ili vyombo vya Ulinzi na Majeshi yaweze kufanya vizuri unahitajika uwekezaji mkubwa sana katika teknolojia, katika rasilimali watu lakini pia na rasilimali fedha. Mheshimiwa Rais amechukua jitihada mbalimbali katika kuhakikisha Majeshi yetu yanafanya kazi vizuri na ndio maana tunaona Taifa letu liko imara na liko salama. Asubuhi nilikuwa namtania kaka yangu Lusinde, namwambia kuna mataifa Wabunge hawatembei mtaani wanazurura tu bila ulinzi au bastola kiunoni, lakini sisi Tanzania tuko imara kwa sababu ya ulinzi na usalama. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri na Wataalam wake wote Wizarani, nampongeza Afande CDF Mkuu wa Majeshi, Majenerali na Makamanda na watumishi wote wa Jeshi pamoja na Wizara. Kazi nzuri wanayoifanya lakini pia na Makamanda wetu walioko maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya kuhakikisha wanaweka usalama mbalimbali kwa maana ya peace keeping mission na peace building mission. Wanajitolea unapoingia katika viwanja vya mapambano maana yake umeweka rehani usalama na uhai wako. Tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie baadhi ya maeneo asubuhi hii katika hotuba hii ya Waziri kuhusu Wizara ya Ulinzi. Eneo la kwanza ningependa kuchangia ushiriki wa Jeshi letu kwenye usanifu na usimamizi wa miradi ya kitaifa na miradi ya kimkakati. Tunaamini kabisa Jeshini ni sehemu ya kwanza katika suala la strategy, mikakati na ulinzi. Serikali ningewashauri waongeze wigo wa ushiriki wa Jeshi letu katika usanifu wa miradi hii hususan miradi mikubwa ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Nishati hivi karibuni niliwaona wamekaa wakijadiliana kuhusu suala la kuimarisha ulinzi kwenye Mradi wa Bwawa letu la Umeme. Hii ni hatua nzuri wakati mwingine wawe wanashirikishana kwenye miradi mikubwa kama Serikali ya kimkakati. Miradi kama Liganga na Mchuchuma ambayo kwa sasa ndio move ya Taifa letu, wahakikishe wanashirikisha Jeshi letu kuanzia hatua za awali na Jeshi letu limejaliwa wataalam wengi, lina ma-engineer wa kila aina, lakini lina watu wazalendo ambao watafanya kazi kwa maslahi ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ambayo ningependa kuchangia mchana huu ni suala la Kamandi ya Jeshi la Akiba. Hili ni kama vile limesahaulika kidogo, naomba Wizara na Serikali waongeze nguvu katika kamandi hii. Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa askari mgambo, lakini baada ya mafunzo tunajikuta tunawaacha mtaani kwa maana ya notion kwamba ni Jeshi la Akiba. Hawa watu waingizwe kwenye mfumo rasmi wa kiserikali, waweze kuwa-monitor kwa ukaribu, lakini pia waangalie namna ya kuweza kuwasaidia kwa namna yoyote, mbeleni wawe na mipango hata ya kuimarisha bima za afya ili waweze kuwa tayari gado, wakiwa fit, hata inapotokea dharura yoyote watakapowahitaji basi wanaungana na Majeshi yetu katika operation mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi, Military Act ukijaribu kuangalia hawa watu kunapotokea tafrani, hadhi yao ni sawa na askari wetu ambao wako kazini. Kwa hiyo na wenyewe katika kipindi ambacho ni cha amani na utulivu, basi tujaribu kuangalia namna ambavyo tunaweza tuka wa-accommodate na waka-feel kwamba ni sehemu ya Jeshi letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia mchana huu ni ujenzi wa anga za ndege za Jeshi ambalo Mheshimiwa Fakharia aliliongelea, niwasisitize tu na kuwaomba Serikali wakamilishe ni anga za kisasa na kubwa ambazo zinaweza zika-accommodate ndege zetu hususan hii ya Dodoma ambapo kwa sasa ni makao makuu, tungependa kuona hivi karibuni imeanza kufanya kazi ili tuweze kuimarisha ulinzi wa Taifa letu na Makao Makuu ya Nchi yetu. Kama tunavyojua tumezindua Ikulu yetu kwa sasa ya Chamwino, basi na Jeshi liwe kamili kamili kabisa kwa lolote ambalo litakuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana nalo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni Mradi wa Nyumbu TATC-Tanzania Automotive Technology Centre ni kituo cha Jeshi kwenye teknolojia, tunaomba Serikali na Wizara waongeze fedha. Kamati tulipita pale tukaona maendeleo yaliyokuwepo mwaka jana na mwaka huu kuna improvement kubwa, tuwatie moyo, waendelee kupambana. Naamini kwamba Jeshini ukiwekeza teknolojia Zaidi, basi tutasonga mbele, utafiti utafanyika kwa kiwango kikubwa, lakini tutabuni mambo makubwa ambayo yatakuwa yanatusaidia katika ulinzi na usalama wa Taifa letu na kupiga hatua mbele katika level ya teknolojia.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ningependa kulichangia na kulisisitiza ambalo baadhi ya Waheshimiwa wamelichangia ni kuhusu msamaha wa kodi kwenye vifaa vya Jeshi. Mheshimiwa Waziri ajaribu kukaa na Waziri wa Fedha hili jambo walione ili itakapokuja Sheria ya Fedha tuliangalie kwa mapana. Haiwezekani tukawa na Jeshi ambalo tumeliamini kulinda mipaka ya nchi, tumeweka usalama wetu mikononi mwa Jeshi letu, lakini inapokuja kwenye clearance ya vifaa tunaanza kuwa na kigugumizi. Ni aibu sana, tulifanyie kazi, sisi tumeamua kulisemea Jeshi kwa kuwa linafanya uzalendo wa Taifa letu, linatulinda usiku na mchana na sisi kama Taifa tumebaki imara.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)