Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ya kuchangia fungu 48 - Wizara ya yetu hii ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi. Kwa nafasi hii naweza kuchangia maeneo kama mawili na nikipata muda zaidi nitakuwa na eneo la tatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze hapa ambapo ameishia Mheshimiwa Halima kwenye eneo la mgogoro. Kwanza, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi anavyoendelea kuwaaminisha Watanzania kwamba gurudumu linaendelea bila kusimama, wazi kabisa. Nitatoa uthibitisho katika maeneo mengi haya ambayo nitachangia. Pia nawapongeza sana Wizara; Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mabula na kaka yangu Mheshimiwa Pinda, pamoja na Katibu Mkuu na timu yake ya watendaji, wananendelea kufanya kazi vizuri sana.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza hapa alivyosimama Mheshimiwa Halima juu ya mgogoro wa kule Dar es Salaam, eneo ambalo linaingiliana katika majimbo mawili. Hili linaitwa Shamba la Malolo (Malolo Farm). Kwenye historia, ni kweli shamba hili lilikuwa linamilikiwa na Shirika la Maendeleo Dar es Salaam (DDC) kwa hati Na. 30 (163) iliyotolewa Tarehe 01 mwezi wa Nne mwaka 1983 ya miaka 99 na eneo hilo lilikuwa kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa hekta au ekari 4,743.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza tukubaliane, ni kweli shamba lilikuwa la DDC, hilo lazima tukubali, lakini kwa kupumzika na wakawa wamelala, hili Shirika la Maendeleo Dar es Salaam, wananchi wakaingia. Sasa wananchi hawa ni takribani zaidi ya 70,000. Upande mmoja wa Kinondoni zaidi ya 39,000, maana wengi wapo Kibamba katika maeneo aliyoyasema Tegeta A, Goba maeneo ya Msumi yote, lakini na maeneo ya upande wa Kibesa Mabwepande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa upande mmoja watu wana uelewa kidogo hili jambo lililotembea upande wa Kinondoni. Nitumie nafasi hii sana kumpongeza Mkuu wa Mkoa aliyeondoka, Cyprian Amos Makala na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu yangu Abas Zuberi Mwishehe Mwanga Mtemvu. Nisiache kumpongeza sana Mkuu ya Wilaya ya Kinondoni, wamefanya vikao zaidi ya vitatu juu ya hii sintofahamu. Mheshimiwa Waziri umesema, moja ya njia zako za kutatua migogoro ni viongozi kutembelea maeneo yale. Ulitamka kabisa, na hii ndipo ilipopatikana. Maana Mkuu wa Mkoa alipoenda kutembelea kule, ndiyo akaliona hili jambo na akatoa maelekezo ya vikao vianze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa upande wa Kinondoni kwenye watu 35,000 Mheshimiwa Gwajima angekuwepo angesema, na ndiyo maana nampongeza sana. Amekaa vikao vitatu, wamefikia kwenye solution, kwamba walipe fidia kuanzia shilingi 8,000 wakakatana, shilingi 6,500 wakakatana, wamefikia shilingi 4,000 kwa kiako cha juzi. Hiyo ni hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu mimi niseme, kwa sababu engagement haionekani wameingia watu wa Ubungo na wakati fulani niliwahi kumwuliza Mheshimiwa Kheri Denis James, Comrade, Mkuu wangu wa Wilaya akaenda Mbulu. Vipi hili jambo? Akasema anaendelea nalo, lakini nilipofuatilia hakuna vikao vya Ubungo ambavyo vimeingia kwenye ile engagement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana, wamefikia 4,000 sawa, lakini kama mtu namiliki kipande cha square meter 500 akalipwa shilingi 4,000 ni shilingi 2,000,000 kule kuna watu wana nyumba za udongo, anatoa wapi shilingi 2,000,000? Kwa hiyo, mimi kama Mbunge wa upande mmoja mwenye watu wengi, hapo mlipofikia kama Serikali ni jambo zuri, mmeangalia consideration ya wananchi wako pale, lakini shamba hilo, hili ni Shirika la Serikali tu. Kwanini isiwe bure?

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani kwa nini shilingi 4,000? Anaenda kupewa nani? DDC aliyekaa miaka 40 na kuliacha! Hebu mwende mkaone, engagement ya Wilaya ya Ubungo; na hapa nitumie nafasi hii kumwomba sana Comrade Hashim Abdalla Komba, DC bora kabisa, yaani ni DC sijawahi kuona. DC bora kabisa aingie kwenye jambo hili vizuri, tuweze kuona wananchi wa Jimbo la Kibamba upande wa Tegeta A, Goba, upande wa Msumi nzima na upande wa Kibesa, nusu ya Mabwepande. Kwa hiyo, kwa sisi shilingi 4,000 bado ni kubwa, tupunguze au twende na bure kabisa. Hayo ni maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nafikiri hapo utakuwa umenielewa, kazi mmeinza, mmefanya vizuri. Siyo tu ya kulaumiwa, kweli wananchi waliingilia eneo hilo la ekari 4,700.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuhusu urasimishaji. Kila nikisimama hapa, lazima niseme hili, na huwa nasema kidogo kwa ukali, lakini leo nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. Tumekaa vikao vingi Dar es Salaam. Sana. Tumekaa vikao vingi Jimboni, umekuwa ukitafuta jinsi ya kutatua jambo la urasimishaji. Urasimishaji limefeli Dar es Salaam. Kweli, lakini nilisikia sehemu tunazungumza, kama huyu, mpeni mpango mmoja wa miaka 10. Kama umefika mwisho, Desemba mwaka huu wa 2023, twende kwenye masterplan. Nikakwambia, hapana, masterplan ina gharama kubwa na ni ngumu kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ile tuliyokuwa ya kuwapatia hati kwa gharama nafuu, tuendelee kuwa nayo. Leo umeniambia kwenye page 59, unao mradi wa uboreshaji wa miliki za ardhi (LTIP), Dola 150,000,000 takribani Shilingi bilioni 345, hongera sana, lakini moja na vipaumbele vyako vingi vya kujenga maofisi na kadhalika, namba moja ni kutatua changamoto ya urasimishaji katika maeneo mengi nchini na hasa Dar es Salaam. Nakupongeza sana. Umeenda mbali, unatatuaje? Unasema utaenda kuanza na mitaa 559. Mimi nina mitaa 42 tu. Naamini ndani ya mitaa yako 559, mitaa 42 yote, najua mmeambiana sample na Benki ya Dunia, lakini mpeleke yote 42 ili tutatue tatizo la wananchi wa Jimbo la Kibamba kwenye urasimishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wangu naomba niwaambie, utafiti umepatikana, Mheshimiwa Waziri anaenda nalo vizuri na timu yake ya Wizara, na anawaondoa hofu wananchi wa Kibamba, yale mambo yangu matatu makubwa; maji, barabara na urasimishaji, yote yanapata majibu mwaka huu. Mambo yanaenda vizuri bambam, mambo yanakwenda vizuri Kibamba. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Jambo lingine ni uboreshaji wa makazi, ndiyo jambo la tatu nilisema kama muda upo. Naona upo. Nimekuwa nikisema hapa pia kuhusu uboreshaji wa makazi. Nimeangalia taarifa za mapato na maduhuli, bado yako chini, 42% ni chini sana. Waheshimiwa Wabunge wengi waliotangulia kusema, wanne au watano mbele yangu, wameendelea kusisitiza kwamba Mheshimiwa Waziri ongeza mikakati ya kukusanya mapato. Pia ongeza ubunifu wa kuona vyanzo vipya vya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema na juzi kwenye semina yako nilisema lakini nilipata majibu kwa wataalamu ambayo yanaleta moyo. Nitumie nafasi hii tena kumpongeza Mheshimiwa Rais na nilikuwa nasema, nitaendelea kusema, nampongeza kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mradi wa Samia Housing Scheme, nyumba 5,000 ni jambo kubwa sana, kwa sababu dhamira au dhima ya mpango wetu wa maendeleo wa miaka mitano, ulikuwa ni kuona tunaboresha makazi ya wananchi wetu ili wajiinue kiuchumi. Mama ameionesha wazi, tunabishana wapi hapo? Nyumba 5,000, asilimia 50 zinakaa Dar es Salaam, asilimia 20 zinaenda Dodoma, asilimia 30 katika mikoa mingine. Ndivyo tulivyoambiwa. Jambo la kupongeza sana hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba, hilo mmepeleka pale Kawe, kwenye eneo moja tu, makazi mapya na wananchi wengi watapata, lakini vipi yale makazi holela, makazi ya chini sana ya wakazi wa Tandale? Nimeendelea kusema, mwaka wa tatu nasema hapa; Manzese ni wachache. Ndugu zangu Wakinga pale akina Sanga wanachukua chukua tu pale wanajenga magorofa Manzese. Kuna Vingunguti na majiji mengine, maeneo ambayo kwa kweli yana hali mbaya, kwa nini tusiende tukatengeneza engagement pale ya kutengeneza MoU, mkubaliane na wananchi wanaomiliki vile vinyumba vya urithi, mkachukua mkawaachia chini ya floor ya kwanza ya pili, Serikali ikachukua ya tatu mpaka ya kumi mkaingiza wananchi wengine? Maana yake wananchi sasa watakuwa wanalipa kodi ya majengo, wananchi watakuwa wanalipa mambo mengine, na maisha yao na afya zao zitakuwa zimeboreka na pia miundombinu ya miji itakuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo la msingi. Nilisema juzi, mfano kule Lang’ata constituency, Jiji la Nairobi; hili ni Jimbo ambalo alikuwa anaongonza Mheshimiwa Raila Odinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli kulikuwa kuna eneo linaitwa Kibera, nyie wengine mnajua, lilikuwa lina mabati-mabati, hivyo kuliko hata Tandale, leo liko vizuri, twende tuige hivyo. Misri kule, South Africa haya mambo yapo ni gharama ni kweli. Juzi nilijibu, hebu endeleeni ingieni tufanye uchumi wa hewani, nyumba ina miaka 30/40 ndiko kwetu sisi, Magomeni, Manzese, Kariakoo, ndiko kwetu, ndiko kwa wazee wetu. Tuko tayari, njooni mtupe uchumi wa chini wa maduka na floor ya kwanza ya pili, chukueni ya tatu hadi ya kumi, mbona tayari hapo utaongeza mapato Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niliona mwaka huu wa tatu nimesema na ninashauri anza kufanya...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umeisha Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu.

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naunga mkono hoja ya Wizara hii. Ahsante. (Makofi)