Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Kwanza nianze na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuipa msukumo mkubwa Wizara hii ya Ardhi. Kusema kweli ardhi ndiyo maisha ya wanadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamesema kuanzia asubuhi tulipoanza kuchangia, wamezungumza suala la kumilikisha ardhi kwa wananchi wetu wa Tanzania. Napenda nimpongeze sana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa Dkt. Mabula na Naibu Waziri, ndugu yangu, Mheshimiwa Pinda, wanafanya kazi nzuri katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni kati ya Wizara chache zenye changamoto nyingi. Interest kubwa ya wananchi iko kwenye ardhi na ndiyo maana kila anayesimama anazungumza habari ya wananchi kumilikishwa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu umuhimu wa kupima ardhi katika maeneo yote ya nchi yetu. Umuhimu wake uko hapa, mwananchi akipimiwa ardhi yake anaweza kupata hati, akipata hati ya kumiliki eneo lake anaweza kuitumia kupata mikopo katika vyombo vyetu vya fedha na hivyo kumwondolea umaskini. Wananchi wetu wengi ni maskini lakini wana maeneo ambayo hawana uhakika kwamba kesho wataishi pale au wataondolewa lini. Hiki ndicho kitu ambacho Wabunge wengi wamezungumza leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana wananchi wetu wakawa na uhakika na eneo wanapoishi. Kwamba akiwa na hati, eneo lake limepimwa, hata kama Serikali itataka kutwaa eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya umma, lazima fidia itakuwa nzuri, kutakuwa na utaratibu wa kisheria ambao utamsaidia yule anayeondoka eneo lile atakwenda kule anakokwenda akiwa amepata fidia nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ilivyo, mtu amekaa anaambiwa apishe labda bomba la mafuta au apishe nini, anaondoka hakuna cha fidia wala nini, anaendelea kuwa maskini kuliko aliokuwa nao wakati ule. Kwa hiyo nashauri sana Wizara hii ipime. Migogoro hii ya ardhi mnayoiona Waheshimiwa ni kwa sababu ardhi yetu haijapimwa, kwa hiyo wananchi kila siku wananyang’anyana ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika ofisi ya Mheshimiwa Waziri, bado katika idara nyingi, hasa kwenye halmashauri, kuna wafanyakazi wachache wasio waaminifu. Wanamilikisha ardhi kwa mtu zaidi ya mmoja, matokeo yake mtu anakaa anajua ana kiwanja mahali Fulani, kumbe kile kiwanja kina wamiliki zaidi ya mmoja au watatu. Matokeo yake kila siku wako mahakamani kwa ajili ya kesi ya kutafuta nani mwenye umiliki halali. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hili alichukulie kwa uzito sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale wafanyakazi wanaofanya ubadhirifu wa namna hii wachukuliwe hatua kali, hata ikiwezekana waachishwe kazi. Huwezi kumilikisha ardhi watu wawili, watatu, ukatarajia kutakuwa na amani katika eneo hilo, haiwezekani kabisa. Kwa hiyo, hili jambo ni muhimu kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mpwapwa tuna maeneo, tuna kata ambazo tayari zina sifa za kupimiwa ardhi. Katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa 34, amezungumzia habari ya Sheria ya Mipango Miji, Sura ya 355, akatoa hata sifa za eneo kutangazwa kwamba linaweza kupimwa. Waziri amesema anaangalia uchumi wa eneo hilo, maendeleo ya eneo hilo, hata mazingira yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mpwapwa tuna maeneo mengi ambayo yanakidhi hizi sifa alizokuwa amezisema Mheshimiwa Waziri. Kwa mfano, kuna Kata za Chitemo, Chunyu, Mlembule, Lupeta, Godegode, Berege, Miima; haya ni maeneo ambayo yangepaswa kupimwa kwa sababu yana sifa zote. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo ili eneo letu lipimwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpwapwa Mjini pia hatujapima, yaani zoezi la kupima linasuasua sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri a-push maeneo haya yapimwe ili wananchi wetu waweze kuyatumia kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ambayo pia inaweza kufanyika vizuri ni kwamba Waziri akipima maeneo, Serikali itakusanya kodi kwa sababu wale wote watakaokuwa wamepimiwa maeneo na kupata hati, watapaswa kulipa kodi ya kila mwaka ya pango la ardhi. Ingawa utaratibu wa sasa Mheshimiwa Waziri, bado hauleti matumaini ya kukusanya fedha za kutosha, bado wananchi wetu hawajawa na hamasa ya kulipa kodi, walio wengi hawalipi kodi, lakini ni kwa sababu ya utaratibu ulioko sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ulioko sasa unamsubiri mlipakodi aende mwenyewe kulipa kwenye mamlaka inayohusika, lakini tungetumia utaratibu mwingine, hata wa kulipa kupitia simu, ili mtu apate unafuu wa kulipa. Leo tunakusanya kodi chache sana za pango la ardhi kwa sababu ya utaratibu ulioko sasa. Kwa hiyo naomba pia Mheshimiwa Waziri waliangalie sana hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuchangia leo ni juu ya utoaji wa hati. Hili nalo ni tatizo lingine katika Wizara hii. Mtu akishapimiwa na kulipa kila kitu, hati inachukua muda mrefu sana kupatikana. Hii ndiyo inasababisha hata viwanja vinavamiwa, kwa sababu mtu amelipa anakaa mwaka au miaka miwili hajapewa hati yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kuna tatizo gani, kwa nini hati hazitoki? Kama mtu amekamilisha kila kitu kinachotakiwa kwa nini hapewi hati yake haraka ili aweze kufanya maendeleo, aweze kuendeleza, aweze kupata mikopo katika mabenki ili aendeleze maisha yake? Hati zinachelewa sana, naomba sana suala la hati waliangalie kwa ukaribu ili wananchi wetu waweze kujikwamua katika maisha haya ya sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya ule mradi wa upimaji. Wamesema sana wenzangu, nami naomba sana fedha hizi nyingi zitumike kwenye mambo ya upimaji wa ardhi. Tumeona katika ripoti ya Waziri, fedha kidogo sana ndiyo inakwenda kwenye ile mamlaka ya kupima, lakini fedha nyingi zinatumika katika kazi ambazo kwa kweli hazina tija kwa wananchi wetu. Kwa hiyo kwa kauli za Wabunge wengi waliosema, naamini Mheshimiwa Waziri atakwenda kuangalia upya, fedha zile zifanye kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini akitumia fedha hizo kwa ajili ya kupima, kwanza kasi ya upimaji itakuwa kubwa, lakini mwakani hatakuja akasema tuna asilimia 25 ya upimaji mpaka sasa hivi. Ndiyo maana migogoro ni mingi, asilimia 25 ni sehemu ndogo sana iliyopimwa. Migogoro hii haitaisha ndugu zangu kama hatutapima maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninakushauri sana Mheshimiwa Waziri, fedha hizi zitumike vizuri, zipime maeneo mengi katika nchi yetu ili mwakani anaporudi hapa atuambie tumepima asilimia 75 na hiyo 75 itatuonesha kwa sababu tutaona migogoro ya ardhi imepungua, hasa ndilo lengo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasemaji wamesema hata nchi za wenzetu majirani migogoro yao ya ardhi siyo mingi kama ya kwetu, lakini ni kwa sababu hatujapima. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi nzuri sana katika Wizara yake, nampongeza sana, lakini kwenye eneo hili la kupima, naomba sana alichukue kwa uzito wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, basi naomba niunge mkono hoja; ahsante sana. (Makofi)