Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii adhimu ya kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya na ya kupigiwa mfano ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa taasisi hii ambao wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba sekta hii ya ardhi inapata mapato ya kutosha na kuweza kuwatatulia wananchi kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze katika makusanyo ya maduhuli. Wizara katika kipindi cha mwaka 2022/2023 ilijipangia kukusanya shilingi bilioni 250 kutokana na vyanzo vyake vya mapato. Uhalisia wa mapato hayo waliweza kukusanya asilimia 42.55 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki cha mwaka 2023/2024, Wizara pia imeweza kujipangia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 300. Naomba niulize Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na watendaji; changamoto ambazo hazikuweza kushughulikiwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023, je, tutaweza kuzishughulikia changamoto hizo katika kipindi hiki cha 2023/2024?

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni nyingi, moja ikiwa ni migogoro mikubwa ya ardhi inayolikumba Taifa letu. Nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kuweka nia ya dhati kabisa ya kuwasaidia wananchi wa nchi hii kupitia migogoro hii ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Mradi wa KKK, Wizara imeweza kutoa fedha za mikopo katika halmashauri mbalimbali, lakini kuna halmashauri ambazo zimeweza kufanya vizuri na kuweza kukusanya mapato na kurudisha mikopo hiyo. Hata hivyo, zipo halmashauri kadhaa ambazo zimeweza kuchukua mikopo lakini hazikuweza kurejesha mikopo hadi hivi sasa, lakini pia wanaendelea kutekeleza miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zile zinatakiwa zirejeshwe ili baadaye halmashauri nyingine ziweze kutumia fedha hizo ambazo zinasubiri. Hiyo ni changamoto kubwa ambayo Wizara wanatakiwa kutuhakikishia kwamba fedha hizi zinarejeshwa haraka ili ziweze kuwasaidia halmashauri nyingine ambazo zinasubiri fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la migogoro ya ardhi; migogoro hii kama walivyosema Waheshimiwa wenzangu, ni mikubwa na ni mingi sana. Kwanza, niipongeze Wizara kwa kuweza kupata Shilingi Bilioni 350 ambazo ni sawa na Dola za Kimarekani milioni 150 ambazo zitaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kuondoshwa migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kusikitisha ni kwamba Wizara katika mradi huu imeweza kujielekeza katika halmashauri 41 tu katika kutatua na kutekeleza miradi hii ambayo ni pamoja na kupanga na kupima katika maeneo ya halmashauri hizo. Migogoro ya ardhi iko nchi nzima, kwa nini Wizara ijielekeze katika halmashauri 41 tu? Katika halmashauri hizo 41 katika fedha hizi imejipangia kutatua migogoro ya ardhi, kwa kushughulikia vijiji 500 tu ambavyo kila mwaka watakuwa wanashughulikia vijiji 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini, kwa vile tunayo Tume yetu ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi na ina ukwasi mkubwa katika kupata fedha za kuendeleza miradi ya maendeleo ambao ni ule Mradi wa Kupanga na Kupima Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Wizara isitenge bilioni 62 tukafuata maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu ambayo imeelekeza mpaka ifikapo mwaka 2025 vijiji vipya 4,131 viwe tayari vimeshapimwa. Kwa nini Wizara kupitia fedha hizi tusitenge shilingi bilioni 62, tukazielekeza katika tume hii na kuanza kutekeleza Mradi huu wa KKK katika vijiji vyote na tukahakikisha kwamba mwaka 2025 vijiji vyote viwe tayari vimeshapimwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, 2025 haiko mbali, Chama Cha Mapinduzi kiliingia mkataba na wananchi na kikawahakikishia kwamba ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote vitakuwa vimepimwa. Kwa nini tusitenge fedha, shilingi bilioni 62, tukaenda tukatatua migogoro ya ardhi kwa kuangalia suala la kupanga na tukaweza kupata mapato makubwa kupitia mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote tukae tuupitie tena mradi, tuangalie namna ya kutenga shilingi bilioni 62 ili tuzielekeze katika mradi huu wa kupanga ili kuhakikisha kwamba tumekwenda na maelekezo ya Ilani, ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote 4,131 viwe tayari vimeshapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna jumla ya vijiji 12,318, lakini vijiji vilivyopimwa ni 2,818 tu ambayo ni sawa na asilimia 23. Tutakapoingia katika mradi huo na kuweza kutenga fedha ya kutosha tutaweza kupima vijiji 826 kila mwaka. Tutaweza kuondosha migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuhusu asilimia 30 ya mapato ya halmashauri ambayo fedha hizi zilikuwa zinabaki ndani ya halmashauri na kuweza kuwanufaisha na kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, karibuni tu tutakuwa na bajeti hapa na kupitia sheria mbalimbali, naomba sana Serikali tuweze kurekebisha sheria hii na kuelekea kwenye kanuni na miongozo mbalimbali ili fedha hizi asilimia 30 ziendelee kubaki halmashauri ili ziendelee kuzisaidia halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niunge mkono taarifa ya Kamati, lakini pia niendelee kuunga mkono hoja ya Wizara lakini kwa kuona kwamba changamoto zote ambazo tumezieleza, ziweza kufanyiwa kazi, ahsante.. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, (Makofi)