Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon Ally Juma Makoa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili kuchangia Wizara hii ya Ardhi. Awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake nzuri juu ya Wizara hii. Kwanza kwa kuona umuhimu wa Wizara hii, Mheshimiwa Rais ameridhia kuunda Kamati kwa ajili ya kushughulika migogoro ya ardhi. Hili ni jambo kubwa ambalo kwa kweli likikamilika litaleta tija kwenye nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, utaona amefanya mabadiliko kwenye Wizara hivi karibuni na ametuletea Naibu Waziri huyo hapo, tunamwona lakini na Katibu Mkuu mpya. Yote hii ni kutaka kuendelea kuimarisha hii Wizara, lakini Mheshimiwa Waziri yuko pale dada yetu Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula anaimudu hii kazi na ndio maana Mheshimiwa Rais kaendelea kumwamini. Kwa maana hiyo tunajua kwa safu hii iliyopangwa sasa hivi, tunawapa muda ili kuweza kushughulikia haya majadiliano na michango ya Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha angalau tunakwenda kupunguza hii migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru, leo utaona asilimia kubwa ya Waheshimiwa Wabunge wanachangia kuhusiana na migogoro, itafikia mpaka kipindi tutashindwa kuona kazi nyingine ambazo zinafanywa kwenye Wizara hii. Mheshimiwa Rais amemtoa Engineer Sanga kule Wizara ya Maji akamleta huku na sisi tulikuwa na mawazo kwamba tunataka sasa Wizara ya Ardhi tuanze kulipa kodi ya ardhi kupitia simu. Tunawapongeza Wizara sasa hivi tunaona tukiwa majumbani tunapata meseji na zenye control number na tunaanza kulipa kwa urahisi. Kwa maana hiyo tunaona mwendelezo mzuri na tunawatia moyo waendelee kushughulika na jambo hili ili na hii Wizara ionyeshe mchango wake mkubwa kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia huu mkopo umekuwa ukizungumzwa hapa na Wabunge, of course mkopo una mambo mengi mazuri ambayo tukiyafanya italeta tija kwenye Taifa, michango ya Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na matumizi hasa ya fedha hizo, lakini tunaamini viko vitu. Wakinunua mashine, mitambo wakatujengea ofisi hizo na vitu kama hivyo, vitaleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wanaona ni nanma gani kunakuwa na migogoro mingi na ndio maana wote tunatamani ardhi yetu yote ingepangiwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro. Sasa hapa Mheshimiwa Waziri aendelee kuchukua ushauri wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na aendelee kuufanyia kazi. Nakumbuka mwanzo walikuja na vijiji 250, baada ya ushauri wa Kamati, leo wamekuja na vijiji 500, bado Kamati inaona ipo room ya kuendelea kuongeza idadi ya kuvipima vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hotuba ya Kamati ni nzuri na waendelee kuichukua kama Wizara na waendelee kuifanyia kazi. Waone namna bora ya kuweza kuongeza idadi ya vijiji. Katika ule mkopo nilikuwa naona fedha zile zilipangiwa Kamati nyingine tofauti ya kuendelea kushughulika na zile fedha. Nadhani tunaongelea Tume ya Mipango ya Ardhi kwa sababu tunaamini wale ukiwapa fedha leo, leo hii wanaingia site kwa haraka na kwa kutumia vifaa vyao hivyo hivyo wataendelea kuvipima vile vijiji hata kama hiyo Kamati nyingine itakuwa haipo. Kwa hiyo, waendelee kuuchukua ushauri wa Kamati, ushauri wa Wabunge, waone namna gani wanaweza kuboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi jimboni kwangu; tuna migogoro ya ardhi kama ilivyo katika majimbo mengine, lakini sasa kwangu kuna migogoro miwili, mgogoro kati ya wananchi wa Mongoroma na Pori la Swagaswaga ambalo Mheshimiwa Rais alilitolea maelekezo. Sasa Mheshimiwa Rais anatoa maelekezo, lakini kule kazi nyingine zinaendelea za kuweka vigingi. Sasa kabla Wizara ya Ardhi haijakwenda kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kazi nyingine zinaendelea. Hapa inaonekana sisi kama Wizara ya Ardhi tunakuwa nyuma, tunachelewa kwenda kufanya maamuzi ambayo yangesaidia kuondoa hii migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wito wangu bado Mheshimiwa Waziri kuna maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba kufika kule ambapo Kamati ambayo yeye ndiye Mwenyekiti walielekezwa kufika, hawakufika kama Kamati, lakini hali iliyopo kule kwa kweli sio nzuri, wananchi wanashindwa kuendeleza maeneo yao. Kwa hiyo, ni lazima kwenda kuutatua ule mgogoro ili kuwaweka wananchi wetu vizuri, waweze kufanya kazi zao za maendeleo wakiwa na amani kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la King’ang’a na Wananchi wa Kingale, jambo hili wamelishughulikia vizuri, tunawashukuru sana na mgogoro ule umekwisha. Wizara ilikwenda, Waziri alimtuma Mpimaji na ramani Mkurugenzi, amefika kule kafanya kazi yake vizuri. Kachukua mapendekezo yamefika mpaka kwa Mheshimiwa Rais, kwa ukarimu wa Mheshimiwa Rais ameridhia yale mapendekezo na ni mapendekezo ya wananchi. Cha ajabu juzi anakwenda Mkuu wa Gereza anakamata ng’ombe wa wananchi anawapiga faini. Najiuliza hivi kila idara, kila mtu anaamua tu kukamata ng’ombe wa watu na kuwatoza faini, hawa wananchi fedha hizo wanatoa wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Bwana anaitwa Juma Kanene ametozwa faini ya 150,000; kuna Bwana anaitwa Hamis Mwiguu ametozwa 400,000; na kuna Bwana anaitwa Kiteto Kiteto ametozwa 200,000; Bwana John ng’ombe wake wawili wamezuiliwa gerezani na huyu Bwana Samweli ng’ombe amezuiliwa gerezani. Sasa tunajiuliza kila mmoja akijipa jukumu la kukamata ng’ombe wa wananchi na hali ya kuwa eneo hilo tayari limeshakwishatatuliwa mgogoro wake, imebaki Wizara ya Ardhi kwenda kutuonesha tu mipaka tuliokubaliana, hii inakuwa sio sawa na inakuwa ni uonevu kwa wananchi. Kwa hiyo, naomba mamlaka iliyopo hapa ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani amwelekeze Mkuu wa Gereza awarudishie wananchi fedha alizochukua kwa sababu si halali yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara sasa iende ikakamilishe jambo hili, lililobaki ni kuwaonyesha tu wananchi kwamba Mheshimiwa Rais katupa maelekezo kwamba ninyi mpaka wenu unaishia hapa na gereza unaishia hapa. Tuwasaidie kuweka vigingi ili kila mmoja aweze kujua mpaka wake ili wananchi wetu hawa waweze kufanya kazi zao kwa amani bila kutishiwatishiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipata nafasi ya kuja kuchangia kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani nitashauri juu ya uendeshaji wa lile gereza kwa sababu tunaona halina tija kwa safari hii, inabidi tulifanyie mapinduzi ili liweze kuleta tija katika nchi na wananchi wa eneo lile waweze kunufaika na gereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)