Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie na ninachangia jioni ya leo huku Kaimu Waziri Mkuu Kapteni George Mkuchika akinisikiliza, Waziri Senior kabisa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwa kuwa yeye ni Waziri Senior anajua migogoro ya ardhi katika nchi yetu ilivyokithiri, kwa hiyo naamini Kaimu Waziri Mkuu atamshauri Waziri husika na Naibu wake na hasa ukizingatia michango tangu asubuhi hii ya leo imeonesha ni namna gani migogoro ya ardhi katika nchi yetu bado haijapatiwa ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Nyatwali tu leo hii. Suala la Nyatwali lilikuwepo tangu enzi ya Rais Awamu ya Nne Baba yangu Jakaya Mrisho Kikwete, akalisitisha kwa sababu hakutaka kuingia kwenye historia ya dhuluma ya wananchi wa Nyatwali. Suala la Nyatwali, Mungu amlaze mahali pema Hayati John Pombe Magufuli alilisitisha. Mmekuja Mheshimiwa Waziri mnataka kumuingiza Rais Awamu ya Sita aingie kwenye mgogoro na wananchi kwa sababu mnataka kumshauri vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili haliwezekani, wananchi wa Nyatwali waligoma kuhama kabisa, kabisa kwa sababu ya wasiwasi wa kudhulumiwa. Mkatumia nguvu kwenda kuwatisha, kipindi changu mimi niligoma na nikawaambia kuhama siyo issue, issue mnawahamisha kwa fidia ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkumbuke eneo la Nyatwali ni lao wako pale zaidi ya miaka 700, leo kwa dhamira yao mnawatisha, mnawashurutisha, tena mpaka Viongozi wa CCM, viongozi wa vijiji, Diwani mnawaita Polisi kuwashurutisha wananchi wanyonge wale na ninyi mnasema ni Serikali sikivu. Kwa nini hamtaki kuwasikiliza wananchi wa Nyatwali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnawalazimisha kuhama, sawa wamekubali, kweli nchi hii eneo la Nyatwali, eneo la lango kuu la kuingilia Mbuga ya Serengeti, eneo very prime, muende mkawalipe fidia ya shilingi 400 kwa square meter? Yaani mnataka kutuambia thamani ya ardhi kwenye Mbuga ya Serengeti, Nyatwali thamani yake ni ndogo kwa square meter kuliko Coca- cola, Coca-cola shilingi 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnataka kutuambia wananchi wa Bunda Mjini, thamani ya ardhi kwenye lango kuu la kuingia Mbuga ya Serengeti, Mbuga namba moja inachukua tuzo kila siku, thamani yake kwa square meter ni shilingi 400, Coca-Cola shilingi 500, chipsi kavu buku (shilingi 1,000)? Hatuelewi watu wa Mara. Watu wa Mara hatutawaelewa na mnatujua. Hatuhitaji migogoro na ninyi, tunahitaji haki yetu. Hivi leo unampa shilingi 400 kwa square meter, jirani Kata ya Bariri viwanja vinapimwa square meter ni shilingi 3,000. Mnataka kuwatoa watu 13,000 mkawafukarishe siyo sawa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namsikia Mbunge anayetoka kwenye makaa ya mawe kule anashukuru watu wake wanalipwa, nataka nijue, hivi kule nako mnawalipa shilingi 400? Watu wa Mara tumewakosea nini? Shilingi 400! Pale Nyatwali kuna ng’ombe 42,000, kaya 1,300, kwa square meter shilingi 400 ataenda kununua ardhi wapi? Leo mtu ana ekari tano unamwambia umpe shilingi milioni mbili? Tuvaeni viatu vya hawa wananchi! Tuvaeni viatu vya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mabula Dada yangu nakuheshimu, kama kuna watumishi wanakuongopea, usiingie kwenye historia ya kwenda kuwadhulumu. Kuna wamama pale wanalima, wana imani na Rais mwanamke mwenzao, msiende kumuingiza kwenye migogoro. Haiwezekani ng’ombe 42,000, wafugaji 1,000 zaidi ya 300, wataenda kununua hekari ngapi? Mtawaweka wapi? Kwa nini mnaamua kuwahamisha watu kabla hamjajipanga? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumbe macho, mtumie Jeshi la Polisi, mtishe watu kwenda kuwadhulumu watu, kwenda kuwatisha, muwaondoe huku wakiwa wana kinyongo? Taifa letu haliwezi likabarikiwa. Taifa letu haliwezi kuingia katika historia ya kuwadhulumu wananchi maskini. Kuwadhulumu wafugaji, kuwadhulumu wamama wa Nyatwali. Mimi binti yao siko tayari. Mimi binti yao niliyetoka familia maskini ya Manyamanyama, niliyelelewa na wafugaji wale sitokubali! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Nyatwali wanasema walikubali kuhama, walikuwa wana imani na Serikali yao, leo mnataka kuwalipa shilingi 400 kwa square meter siyo sawa.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Taarifa

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Patrobass Katambi, Mheshimiwa Naibu Waziri.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto za migogoro ya ardhi na ndiyo maana kukaamriwa kuundwa timu ya Mawaziri wale wa Wizara Nane kwenda kushughulikia changamoto hizi, katika procedure za Sheria ya Ardhi zinavyoelekeza, lazima mfanye vikao vya consultation na wananchi husika. Vikao hivyo vilifanyika, Mawaziri hawa nane walikaa na wananchi na waliwasikiliza na katika utwaaji wa ardhi hao wanajua, tusipotoshe. Sheria ya Ardhi inaelekeza procedure za acquisition of land, kwenye Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mwananchi unapotaka kuchukua ardhi kwa matumizi ya Serikali lazima ulipe fair and adequate compensation. Hizo procedure zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo taarifa ya mwisho katika utaratibu ule ule hakuna mwananchi ambaye alionewa na bado katika uthamini mwananchi anayo haki ya kukubali malipo au kukataa malipo kabla ya kwenda kwa Chief Land Valuer. Kwa hiyo, utaratibu huo upo ni suala ambalo linafanyiwa kazi na ripoti italetwa na Serikali. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Ester taarifa unaipokea?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa yake, lakini Sheria ya Ardhi inasema fidia ya haki, kwa tafsiri hiyo, shilingi 400 ndiyo fidia ya haki kwa Serikali?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo fidia ya haki kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi? Mawaziri Nane walienda pale hamkuwatisha wananchi? Hamkuwatisha wananchi? Mnawatisha Diwani, mnawatisha Wenyeviti wa Vijiji. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Nyatwali hatutahama mpaka tupate fidia inayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Ester, muda wako umeisha.