Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi, na mimi nishukuru Serikali ya chama changu ya Chama Cha Mapinduzi kwa kazi hii ambayo sasa inaenda kuifanya nchi ifunguke kwa mawasiliano. Ni juzi tu tumeshuhudia pale Mheshimwa Rais akishuhudia kusainiwa kwa minara 758 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni tukio ambalo kwa hakika litakuwa Faraja sana minara hii ikijengwa katika nchi hii na mimi eneo langu lilikuwa na changamoto hii na tunatenda kutibu japo hatumalizi. Tumepata minara michache sana. Katika majimbo yaliyopata minara michache mojawapo ni la kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mimi nimepata minara minne tu. Mnara wa Rungwa, katika Kata ya Rungwa, Mnara wa Kintanura Kata ya Mwamagembe, Mnara wa Gurungo katika Kata ya Sanjaranda na Mnara wa Ipalari katika Kata ya Kintinku. Katika Wilaya ya Manyoni tumepata minara mingi sana lakini imeelemea jimbo moja. Kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri alione hili. na uhitaji wa minara michache sana mitatu tu tukipata tutafungua watu wetu. Mnara wa Mhanga katika Kata ya Ipande, Mnara wa Tulieni katika Kata ya Kalangali na Mnazi katika kata hiyohiyo ya Kalangali, tutakuwa tumelifungua Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi kwa mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto, minara mingi iliyopo katika jimbo langu ni ya 2G michache sasa inaanza kwenda katika 3G. Dunia imehama. Dunia imehama kutoka katika talking na sasa watu wengi wanatumia data, na hata wanapiga simu za kutumia data mawasiliano ya kimataifa Zaidi, ni pamoja na watu wangu, pamoja na kuwa ni wa maeneo ya vijijini lakin,i sasa hivi nao wamekwenda katika ulimwengu wa kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe sana Wizara hii ya vijana hawa ambao ni mahiri kabisa, na umemsifia Waziri wa Wizara hii kwa kutumia dakika chache kusoma taarifa yake kuliko Mawaziri wote katika Bunge hili. Kwa hiyo kwa umahiri huu ninaomba sasa autumie ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi hii yanafunguka, likiwemo jimbo langu. Minara hii mitatu ninaiomba, tuhakikishe wananchi wa eneo hili ambao nao wanasumbuka kupata mawasiliano nao wanapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo hili la bando, nimeendelea kuwaomba Wahesimiwa Mawaziri, watumishi na wadau katika Wizara hii. Watu wa umeme wana Luku. Ukiweka Luku yako kwa kadri ya pesa ulizoweka itakwisha pale matumizi yatakuwa umetumia lakini bando ukiweka hata muda ukiisha yaani haujatumia kwa sababu tu ni la muda maalum inakuwa imekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sasa basi tusaidiwe katika suala hili tufike mahali zihesabiwe kama ni unit kama ni kitu gani kutokana na utaratibu wenu basi matu matumizi yake ndio yalingane na malipo yale isiwe ni bando la muda maalum. Inawezekana ukaomba bando la wiki moja lakini matumizi yale ndani ya wiki moja yasiishe, kwa hiyo bando lile likatike na lisiishe. Mimi leo nimeshuhudia kwenye simu yangu, nilikuwa nimeweka bando lakini limeisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna changamoto nyingine, unaweka bando mwezi mmoja kabla ya mwezi unaambiwa limekwisha lakini ukiangalia matumizi hayakuwa katika kiwango hicho; hili ni jambo ambalo linatakiwa pia liangaliwe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, sisi watu wa Itigi tunachangamoto sana ya usikivu wa Redio. Watu wetu ni wananchi wa daraja la chini, wananchi ambao wanatumia Redio, TV mpaka wawe na madishi na TV yenyewe ni vitu vya gharama. Redio shilingi elfu 10 mtu anapata habari anaisikiliza dunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika ukurasa wa 125, kwamba umeiweka Manyoni, mnaenda kuongeza usikuvu wa Redio. Lakini changamoto kubwa Mheshimiwa Waziri ipo Itigi, siyo Manyoni. Kwa hiyo muangalie ni namna gani watu wa Itigi wanapata mawasiliano ya Redio. Pale kuna Redio imeweka mtambo wake sitaki kuitaja kwa sababu ndio tunayosikiliza. Sasa mnapoenda kufunga mhakikishe watu wa Itigi wanapata mawasiliano ya Redio ya TBC Redio yao ya Taifa, wamskie Mheshimiwa Rais wao anapohutubia Taifa kupitia redio yake ndogo, redio ya mkulima. Sisi kwetu kule wakulima ndio wengi. Kwa hiyo ninaomba sana hili jambo liharakishwe ili wananchi waweze kupata mawasiliano. Iko ahadi yako Mheshimiwa Nape, uliahidi hapa katika Bunge hili, kwamba mtakwenda kuanzisha Chuo cha Teknolojia ya Habari sijui mmefikia wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja basi utuambie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Jamhuri ya Muungano, vijana wetu. Dunia inahama kutoka kwenye elimu ile ya kizamani; hata hizi VETA zilizopo sasa zinapitwa na wakati. Sasa ninyi mtakapokuja na Chuo hiki cha Teknolojia ya Habari mtaisaidia Tanzania kwenda na upepo ambao upo duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja, ahsante sana.