Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, niishukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo yote ambayo amefanya kwenye Wizara hii lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri pamoja na timu nzima kwa ujumla kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Niipongeze na kuishukuru Serikali kwa baadhi ya minara ambayo tumepata ndani ya Jimbo la Momba kwenye Kata za Chululumo, Msangano, Nzoka na sehemu zingine. Tunaomba kueneelea kuboreshewa minara kwenye Kata za Kapelle, Tungwa, Mkomba lakini pamoja na Kata ya Chitete ikiwa ni sambamba na kuhakikisha mnatuchepushia Mkongo wa Taifa kufika makao makuu Chetete.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba kidogo niku-challenge Mheshimiwa Waziri in very positive way. Kwenye zile ajira ambazo ziko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi wewe ndiye mtu kwenye Wizara hii umebeba ajira nyingi sana za vijana kama ukiamua tu ukiamua kutumia teknolojia in very positive way.

Mheshimiwa Naibu Spika, Juzi wakati nachangia kwenye Wizara ya Profesa Mkenda ambaye Wizara yake ni Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia lakini Wizara yako ni Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tukaomba tungepata Wizara mpya ya Teknolojia ili tuweze kuendana na karne ya 21 ili tuweze kuendana na Fourth Industrial Revolution Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna namna tunaweza tukakwepa jambo hili ndiko wakati unakotupeleka lakini nishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi nataka kurejea; kwenye ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwenye sura ya nne ambayo inasema sayansi na teknolojia na ubunifu kwenye ukurasa wa 154.

Ilani yetu ambayo tuliinadi, inasema hivi “Chama cha Mapinduzi kinatambua kuwa uchumi wa kidijitali ni muhimu katika kuleta maendeleo kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji na utekelezaji wa shughuli mbalimbali na kutoa fursa za kuongeza vipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Uchumi huo umeonekana kuwa eneo muhimu katika kuchangia kukuza uchumi nchini kama ilivyofanyika katika nchi zingine za kipato cha kati. Aidha, uchumi wa kidijitali unalandana na mapinduzi ya nne ya viwanda yaani maana yake fourth industrial revolution yanayokuja na ambayo hayaepukiki. Hivyo basi, CCM itaendelea kusimamia Serikali kuhakikisha kuwa teknolojia mpya za kidijitali zinatumika kuongeza ufanisi katika sekta za uzalishaji na kuepuka madhara yanayoweza kutokea. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo Chama cha Mapinduzi kinaelekeza yafuatayo: -”

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo manne, lakini naomba niende kwenye jambo moja la muhimu. Kuimarisha kituo cha utafiti hapa Mheshimiwa Waziri amekwama; kuimarisha kituo cha utafiti, ubunifu na uendelezaji wa TEHAMA ikiwemo kujenga uwezo wa kuongeza matumizi ya teknolojia mpya za kidijitali na artificial intelligence.

Mheshimiwa Naibu Spika, yuko msanii wa Mheshimiwa Waziri pale Diamond, muulize ameshapeleka kazi zake kwenye NFT, bado. Vyote hivyo ni vitu vya muhimu. Ni msanii wetu ilibidi tulinde kazi zake NFT kazi zake ziende hapo ambapo kazi zake zisije kupata huko madhara. Block chain technology kwa research ndogo ambayo nimefanya hapa kwetu Tanzania kwa mambo madogo ambayo nimefuatilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano unamuuliza mtu unajua nini kuhusiana na block chain technology, unajua nini kuhusiana na digital currencies, unajua nini kuhusiana na crypto currencies. Mtu anakuuliza kwa hiyo Mheshimiwa nikitaka kujiunga kwenye Bitcoin nafanyaje? Yaani swali hili does not make sense, yaani ni sawa mtu ananiuliza kwamba Mheshimiwa Mbunge najiungaje kwenye T-shilling? Yaani mtu anajiungaje kwenye T-shilling yaani Tanzania shilling hela yetu mtu anajiungaje? Digital currencies, block chain technology ni teknolojia kubwa sana ambayo Chama Cha Mapinduzi kwenye Ilani yetu imesema, tuboreshe Kitengo cha Utafiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi akiwa kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwenye Wizara hii, nilishawahi kumfuata sana kuhusiana na mambo ya PayPal kila wakati nilikuwa nachangia. Akaniambia tunaendelea kufuatilia dada, tunafuatilia tunaongea na watu wa BOT. Siku moja nikamwona tena kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Ndugulile amekuja hapa anauliza mambo ya PayPal. Sasa nikashangaa huyu tena kaka yangu alikuwa ni Waziri, sasa tena amekuja kuuliza. Kwa hiyo unaweza ukaona utafiti huo Mheshimiwa Waziri angekua ametusaidia, amekaa vizuri na watu wa BOT. Tunatamani kuona teknolojia tunazozipata zisiende tofauti na kazi zetu ambazo tunazifanya na taratibu ambazo tumejiwekea kwenye nchi yetu, lakini tayari kama kungekuwa na utafiti tungejua namna ya ku-accept PayPal kama ni njia ya kulipa na kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi huko nje watu wetu hapa Tanzania wanalipa kwa PayPa,l hela zao zinapitia Kenya zinaishia huko, why not us? Yaani nini ambacho Kenya wanatuzidi ambacho sisi hatuna ambacho hatuwezi ku-adapt, nini ambacho South Africans they have sisi hatuwezi ku-adapt tukawa nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mdogo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, block chain technology si teknolojia ya kuidharau, ni teknolojia ambayo ina mawanda mapana. Huko ndani kuna watu wa mambo ya sheria, mambo ya smart contract, huko ndani kuna mambo ya watu ambayo yanahusiana na mambo ya ardhi kuna vitu vingi. Huko ndani kuna mambo ya NFT ambayo ni mambo ya wasanii kwa ujumla na hata waigizaji wetu, yaani viko vitu vingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Waziri kiamua tu kuikumbatia block chain technology vizuri kwa lengo zuri, bila kuathiri mila na desturi zetu. Ndio namwambia Mheshimiwa Waziri inaweza ikawa ni Wizara ya mfano ambayo itatoa ajira nyingi sana ambayo imeandikwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Wapo maprofesa kadhaa kwenye nchi hii ambao wameandika maandiko kuhusiana na block chain technology. Kwa nini tusimwombe akae nao, lengo tunataka jamii ijue, mara nyingi wananchi wamechukulia hivi. Kwa mfano kuna siku moja kuna mtu akawa ananiuliza block chain technology ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nikaona anafananisha, ni kama mtu umwambie mtoto mdogo unataka kuwa mwanasiasa? Aseme hapana, mimi sitaki, mambo ya kutukanana kwenye mikutano, mimi sitaki kuwa mwanasiasa, lakini siasa sio hivyo, siasa ndio tuko hapa sisi Wabunge tumekutana. Sisi ni wanasiasa, kwenye siasa ndiyo tunampata Mheshimiwa Rasi, kwenye siasa ndio tunampata Spika wa Bunge, kwenye siasa ndio tunampata Mheshimiwa Zungu, kwenye siasa ndio tunapata Baraza la Mawaziri, kwenye siasa hapa ndani tulipo Bunge ndio tunapitisha bajeti, ndio tunatunga sheria, ndio tunatetea mambo ya wananchi. Kwa hiyo yule mtu ameingolea siasa kwenye ka-negativity kadogo yaani tone yaani drop of water kwenye bahari, ndio ameongelea siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mtu anaposema Bitcoin ni wizi, sijui ni pyramid yaani ni kama mtu aseme mimi sitaki internet kwa sababu wanaonyesha pornography. Si sawa, internet inafanya vitu vingapi? Hayo ni madhara madogo ambayo yanatokana na kuwepo kwa internet. Kwa kuwepo kwa block chain technology, ni teknolojia ambayo lazima itaambatana na challenges nyingi tu ambazo hatuwezi kuziepuka, lakini unapoongelea block chain technology na vitu viliko ndani yake ni jambo kubwa, ni jitu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aende basi hata kukaa na timu yake, apitie hata vitu vichache tu mambo ya coin market, yaani aingie tu hata kwenye ile website, coin market cup. Aangalie pale, zile currencies zote, hivi kweli watu wote wale wanaweza wakawa ni wajinga wamekaa. Mheshimiwa Waziri atamani hata kumfahamu who is Santos Nakamoto. Huko tunapoenda Biblia yenyewe imeandika hakuna namna tutakavyokwepa kuja na one currency. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiko huko tunakoenda hakuna namna benki zitakwepa hilo jambo ndiko tunakoenda. Kizazi chetu ndio hiki hiki Waziri anavyotuona, miaka 20 ijayo ndio tutapata Rais hapo, ndio tutapata Waziri Mkuu hapo ndio tutapata viongozi wakubwa hapo. Kwa hiyo, hiki tunachokishauri muda huu hatutamani kupitwa. Hebu aangalie sasa hivi tulivyopokea internet, angalia internet ambavyo inatusumbua. Tulichelewa kutunga sheria ambazo zitafanana na wakati tulionao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu kwenye mitandao ya kijamii wanaweza wakamtukana hata Mheshimiwa Rais, hatujawahi kuona hata mahali wanashtakiwa kwamba walimtukana na wapo, wana challenge. Tunaona watu wanatukana viongozi mbalimbali matusi mengine makubwa. Tunaona watu wanaandika vitu vya ajabu, wanaposti vitu vya ajabu ambavyo viko nje na utaratibu na mila na desturi zetu, lakini hatuna sheria ambazo zinawabana kwa sababu tuliacha internet ikatutangulia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: …kuliko sisi. Kwa hiyo nimwomba Mheshimiwa Waziri aboreshe utafiti kama ambavyo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inasema na kama itawapendeza kama Serikali…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa malizia sekunde, ahsante sana muda wako umekwisha.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)