Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa. Kwanza naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais ameendelea kuchanja mbuga kuhakikisha kwamba shughuli za kimaendeleo katika sekta zote zinakwenda kwa kasi kubwa na tumeshuhudia juzi zoezi la kusaini mikataba ya ujenzi wa minara na sisi Wabunge tumeshiriki na wadau wengine. Kwa kweli shughuli ile Watanzania wote wameiona kwa macho na ina kwenda kuongeza kasi ya upatikanaji wa mawasiliano katika Taifa letu la Tanzania kwa ujumla. Kwa hiyo tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa anazozifanya katika sekta hii muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze sana Mheshimiwa Nape, Waziri pamoja na Naibu Mheshimiwa Kundo…

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. BONIPHANCE N. BUTONDO:…kwa jinsi ambavyo wameendelea kushiriki pakubwa sana kuhakikisha kwamba…

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja…

NAIBU SPIKA: Husikiki, microphone yako imekaa vibaya. Mic yako ina nini, ina glitch?

(Hapa kipaza sauti hakikufanya kazi)

MHE BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshindwa kumsikia vizuri, lakini kwa ajili ya kulinda muda, naomba kulinda muda wangu, lakini kimsingi naamini atakuwa anazungumzia suala la muhimu sana la mawasiliano hasa katika Jimbo lake la Igalula na mimi ni mdau wa shughuli za maendeleo katika Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba pia niwashukuru watendaji wote katika Wizara hii kwa namna ambavyo wanafanya kazi zao vizuri. Sasa la pili nataka nizungumzie suala zima la minara; tumeshuhudia utiaji wa sahihi wa ujenzi wa minara 758, lakini 304 ambayo inaenda kuongezewa nguvu. Zoezi hili muhimu linaenda kuleta tija na kuharakisha shughuli za kimaendeleo kwa ujumla katika Taifa letu. Suala la mawasiliano ambalo lilikuwa linahangaisha hasa katika Jimbo la Kishapu, tunakwenda kunufaika pa kubwa sana kutokana na zoezi hili la kusaini mikataba ambalo limefanyika hivi karibuni. Katika hili narudia kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini tunakubaliana wote kwamba Sekta hii ya Mawasiliano ndiyo chachu kubwa ya maendeleo katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie katika maeneo haya ambayo yanaenda kunufaika na suala zima la minara hii. Mimi naenda kupata jumla ya vijiji 17 ambavyo vinaenda kupata manufaa na minara hii na minara hii iko minara 11. Hii ni pamoja na Busangwa mnara mmoja, Itilima ambayo ina Ikoma, Ileberebe na Mwajiginya B, lakini kuna Masanga pale panaitwa Dodoma, lakini kuna Mwakipoye Iboje na Mwakipoya yenyewe lakini pia na Shagihilo ambapo kuna Kijiji cha Mangu lakini kuna Mwamalasa ambapo Magalata wanaenda mnara, lakini Talaga ambayo ina Jijongo na Nendeghese inapata mnara. Pia maeneo haya yatakwenda kusaidia vijiji vyote jirani kupata mawasiliano kwa urahisi. Kwa hili namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Kundo kwa sababu alifanya ziara katika Jimbo langu na haya maeneo aliweza kuyabaini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumwomba Waziri kwamba, maeneo ya Kata ya Seke Bugoro, Somagedi, Mwasubi na Bunambiu bado yana changamoto ya mawasiliano. Niombe sana katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao, waweze kufanya consideration katika maeneo haya na yenyewe yaweze kupata mawasiliano kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie hapa ni suala zima la redio yetu ya TBC. Jukumu la TBC na hata katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri amezungumza kabisa wazi, ya kwanza ni kuhakikisha kwamba tunaielimisha jamii, kuihabarisha jamii lakini kuiburudisha jamii lakini na kuitafakarisha kwa kuzingatia kauli mbiu ya ukweli na uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kauli mbiu hii ya Ukweli na Uhakika lakini ikiwa ni pamoja na kuhabarisha, kuelimisha lakini na kuburudisha, bila mawasiliano ya uhakika ama bila usikivu wa uhakika, Watanzania wengi wanakosa mambo haya ya muhimu. Kwa hiyo naomba sana katika Jimbo la Kishapu maeneo makubwa sana Redio TBC haisikiki kabisa katika maeneo hayo. Niombe sana hili jambo liweze kufanyiwa kazi ili mradi wananchi wangu waweze kunufaika na redio hii muhimu ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumeona kabisa katika mwaka wa fedha 2022/2023, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba redio hii inasaidiwa na inakuwa na uwezo mkubwa wa kuhabarisha na kutoa taarifa zake, zilikuwa ni zaidi ya 13,133,000,000 lakini pesa ambazo ziliweza kupokelewa pekee yake zilikuwa ni bilioni 3.9 ambayo ni kama asilimia 30, unaweza ukaona kwamba ni fedha kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha kwamba redio hii katika kila tengo la fedha zinazotengwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba redio hii inapata ufanisi, umuhimu huu tuuone kwa sababu wananchi wetu wanaenda kunufaika pakubwa sana sana. kwa hiyo nataka niiombe sana na niirai sana Serikali katika eneo la bajeti, utekelezaji wa upelekaji wa fedha zinakuwa zinatengwa katika kila mwaka wa fedha, ziwe zinapelekwa kwa asilimia 100 ili Mheshimiwa Nape, Naibu Waziri wake pamoja na watendaji wake sasa waweze kuona ufanisi na mafanikio ya bajeti inayotengwa katika kila kipindi cha mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala zima la uandishi wa habari, waandishi wa habari wengi sana jamani wamekuwa wana shida, huwezi ukasema ni omba omba japokuwa lugha ile sio nzuri. Tabu kubwa ni mikataba kwa watumishi hawa. Waandishi wa Habari hawana mikataba, wamekuwa wana shida kweli. Maisha yao kama si sisi wanapokuwa kwenye majukumu hayo kutowajali na kuwapa chochote, wanaishi maisha ya tabu sana. Tunaomba hawa Waandishi wa Habari kwa sababu Waziri ni baba na mlezi, awatazame na kuhakikisha anawalea na kuhakikisha kwamba waajiri hawa wana mikataba. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la msingi ambalo nataka nilizungumzie…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Butondo kengele ya pili, malizia sekunde mbili.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ooh! Ninaunga mkono hoja, napongeza sana. Ahsante sana. (Makofi)