Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nami kwa moyo safi tu kwanza nitambue kwamba sasa hivi walau wanahabari mwanga tunauona, tumepumua kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaanza kufanya kazi kwa uhuru, tunahitaji uhuru zaidi na hili Mheshimiwa Nape umelifanyia kazi, hongera sana Kaka yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine wadau wa habari wanajua kuna mchakato wa Marekebisho ya Sheria ya Habari wanaomba usiende haraka kwenye Bunge hili. Wanaomba waweze kupata nafasi ya kutoa maoni. Wameomba sana na wanajua wewe ni msikivu, hili utalisikiliza ingawa lengo lao ilikuwa sheria mpya lakini kwa sababu kuna amendment kuna mabadiliko ya sheria wanaomba wapate muda wa kutosha kama wadau kuja kutoa maoni yao kwenye Kamati ya Katiba na Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue kazi nzuri inayofanywa na vyombo vya habari na ubunifu pia kwa baadhi ya TV na redio ikiongozwa pale na mdogo wangu Diamond (Wasafi) wanafanya kazi nzuri kupitia kipindi chao cha Good Morning, kipindi cha Michezo lakini Global Online kipindi cha front page wanafanya vizuri, kuna kipindi cha TV cha 360 Clouds, Jahazi na Amplifier kinachoongozwa na Millard Ayo. Tunasema hayo kwa ajili ya kuwapa fursa wengine waweze kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua uwekezaji wa Azam TV wa kidijitali. Pale imeanguka siyo chini ya shilingi bilioni 15 na tunatamani Television yetu ya Taifa ifikie huko. Tunahitaji Television ya Taifa ifikie hadhi ya Al Jazeera, CNN, BBC haya yote yanawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nape unajua mimi ni Mwandishi wa Habari, nimekaa Newsroom nilianza kama Mwandishi wa Habari Mwanafunzi mpaka Mwandamizi, ninajua changamoto za wenzangu. Asilimia 90 ya Waandishi wa Habari hawalipwi. Hao asilimia 90 ni kwenye private sector, hawalipwi na wameshazoea hiyo hali na hawana mtetezi. Mheshimiwa Nape usikubali wewe kama Waandishi ambavyo wana imani na wewe na umewapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya, huu Muhimili usionekane tu upo upo, upewe heshima yake. Waandishi wapewe hadhi yao kwa kazi kubwa wanayoifanya kuwahabarisha Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mwandishi ategemee source kumpa chochote, siyo kwamba anapenda, Mwandishi anatakiwa alipwe na chombo chake vizuri. Akiamua kufanya investigation story kwa maslahi ya nchi awe na uwezo huo, asiwe mnyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nape kuna Vyombo vya Habari miaka 10 hailipi Waandishi, miaka 11 hailipi Waandishi. Kuna chombo kinadaiwa shilingi bilioni 3.5 na Waandishi. Zaidi ya miaka 10 Waandishi hawajalipwa, wafanyakazi zaidi ya 195 ambayo ni Sahara Media. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Waandishi wengine wanadai vyombo vyao shilingi milioni 100, milioni 200, milioni 300 hawalipwi lakini wapo huwasikii wakinung’unika. Wapo humu wanatuandika, wapo humu wanapeleka ujumbe kwa Watanzania nchi yao inafanya nini, kwa kinyongo lakini hawawezi kukaa nyumbani wana familia lazima watoke wakafanye kazi labda huko wataonana na watu wenye nia njema. Hii kazi siyo ya kujitolea, hii ni kazi kama Wakili, hii ni kazi kama Daktari, hii ni kazi kama Mwalimu. Wanahitaji wapate malipo yao Waandishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nape hata michango kwa wale ambao wanapata mshahara kidogo haiendi kwenye mifuko. Hivi hatma yao hawa Waandishi baada ya kazi iweje? (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
TAARIFA
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Napenda kumpa taarifa Dada yangu mzungumzaji kwamba anayoyazungumza ni mambo ya msingi kweli na tunajua jinsi gani Waandishi wa Habari wanavyopata taabu. Kwa hiyo nimuongezee tu siyo vibaya vilevile katika mchango wake kama ataihitaji Wizara iweze kupitia mikataba yote ya Waandishi wa Habari ili waweze kupata stahiki zao. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bulaya.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa yake na wewe unajua Waandishi wanavyopata taabu. Hata hao ambao wanafanya, yaani kuna kampuni Waandishi wameamua tu kufanya kazi bure. Hawana mikataba Mheshimiwa Nape, hawalipwi, michango yao haiendi. Mbali na ugumu wa maisha wanayopata sasa hivi, hatma yao baada ya kustaafu hawaijui. Mheshimiwa Nape nikasema hivi Serikali na yenyewe kwenye hili inachangiaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nape kazi ya umiliki wa vyombo vya habari haitegemei mauzo kwenye magazeti, haitegemei labda tu TV au redio kutangaza. Vyombo vya Habari survival yake ni matangazo. Leo Serikali ukichanganya Vyombo vya Habari vya private sector na hivi vya umma mnadaiwa karibia shilingi bilioni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnapewa huduma ya matangazo, hamlipi. Sasa huyu tu kwa mfano Sahara Media ambaye anadaiwa na watumishi wake zaidi shilingi bilioni tatu anasema anawadai Serikali shilingi bilioni sita. Tukija Daily News peke yake Serikali mnadaiwa shilingi bilioni 11. Hapo sijazungumzia redio na mpaka huko kwenye level za Wilaya na Mikoa. Sasa kwa nini hamuwalipi matangazo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli unawezaje sasa ukaanza oparesheni ya kutaka Waandishi walipwe kama Serikali hamuwalipi Vyombo vya Habari matangazo? Inabidi muonyeshe mfano. Wamewapa huduma ya matangazo, wamewarushia live lazima muwalipe ili na ninyi mpate sasa nguvu ya kwenda kufanya oparesheni ya media ambazo hazilipi Waandishi wa Habari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nape hilo unaliweza na Waandishi wana imani na wewe, ulikuwa radhi ku-sacrifice nafasi yako kwa ajili ya kulinda heshima ya Vyombo vya Habari. Nikuombe nenda kaanze msako wa kutetea Waandishi wa Habari wawe na mikataba, Waandishi wa Habari walipwe, michango yao iende vilevile hakikisha mnawalipa Waandishi, na vyombo vya habari vya binafsi na Serikali. Hapo TBC nilikuwa sijaitaja kabisa lakini ninataka majibu kwa nini sasa hivi kwenye bajeti ya maendeleo imepungua kwa asilimia 28? Hilo nitataka majibu, tulitarajia bajeti iongezeke zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati hapa tunasifia uwekezaji wa Azam private, huku kuhakikisha TBC inakuwa na usikivu bajeti yao shilingi bilioni 13 ili waweze kukamilisha huo mradi zimetoka shilingi bilioni tatu. Kweli tutaweza ku-compete na watu ambao wanakuja sasa hivi ili hii Redio yetu ya Taifa, Television yetu ya Taifa zifanye vizuri kama hakuna uwekezaji wa kutosha? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitahitaji majibu sahihi. Tunataka tujue hatma ya Waandishi wa Habari. Hii siyo kazi ya lelemama ni kazi muhimu sana. Waandishi wa Habari wakiwa vitani wengine wanakimbia, wao wapo mstari wa mbele kutoa habari. Sehemu yoyote kwenye crisis Waandishi wa Habari watakuwa mstari wa mbele lakini hawathaminiwi kutokana na kazi wanayoifanya. Nitaendelea kulisema hili na nitahitaji lifanyiwe kazi, jambo hili la Waandishi kama la kikotoo sitaacha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mwandishi wa Habari najua kazi ya kutafuta habari, najua risk wanazozipata, najua changamoto wanazozipata, I swear sitakubali Mheshimiwa Nape. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)