Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nichukue nafasi hii kushukuru sana kwa microphone kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rasi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mema ambayo anaifanyia Taifa langu upande wa mawasiliano. Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa sana upande wa teknolojia kwenye kipindi hiki cha Awamu ya Sita. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu, rafiki yangu kwa kazi kubwa anayoifanya. Nakupongeza sana kwa sababu kumekuwa na uhuru mkubwa sana wa kujieleza kwenye kipindi cha Rais wa Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii naisema niki-declare interest kwamba mimi ni mdau wa habari. Nimekuwepo Awamu ya Tano, na Awamu ya Nne nikifanya kazi ya habari. Kwa hiyo, ninaposema kwamba Awamu ya Sita tuna uhuru zaidi ya tulikotoka, iko sababu kubwa sana ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na wewe Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana mdogo wangu Kundo kwa kufika mpaka jimboni kwangu na kujionea hali halisi ilivyo. Sasa wananchi wa Buchosa wamenituma. Buchosa ni jimbo kubwa, lina visiwa vingi sana. Watu wa visiwani hawana minara. Mawasiliano kwao ni magumu, na kuna wakati wanakuwa kwenye hatari ya kuzama, wanashindwa kuwasiliana. Kwa hiyo, naomba mwakumbuke sana watu wa visiwa vya Sosswa, Simbaya, na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema maisha ya vyombo vya habari ni magumu. Media houses zina-suffer. Sasa ombi langu kabla sijaenda mbali ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, msiwapatie ruzuku vyombo vya Habari. Ruzuku wapeni TSN, Uhuru na wengineo. Sisi tunachokitaka na wengine huko, vyombo vya habari vya Serikali vijitoe kwenye matangazo. Yaani ITV wasigombanie matangazo na TBC. BBC hawachukui matangazo, Voice of America hawachukui matangazo, vyombo vya Serikali, visigombanie matangazo na vyombo binafsi. Hiyo peke yake inatosha kuwasaidia vyombo vya habari viweze kukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zetu za bajeti hapa zikienda kwenye vyombo vya habari kwa ajili ya promotion na matangazo vyombo vitaweza kulipa wafanyakazi wake. Nami namshukuru sana dada yangu, Mheshimiwa Esther ameongea mambo mazuri kabisa hapa. Ahsante, Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, uongozi ni kutatua tatizo kabla halijatokea. Yaani uwe na uwezo wa kusema mwakani kutakuwa na njaa, kwa hiyo, unaweka chakula. Dunia imebadilika sana. Tanzania imebadilika sana. Mtu yeyote anaweza akashangaa kwamba zamani tulikuwa tunapiga picha; tunaweka filamu kwenye camera, lakini leo hii hamna. Tulikuwa tunatumia diskette, leo hii hazipo. Dunia inabadilika kwa kasi mno, lazima tubadilike nayo. Tusipobadilika sisi leo, utakuta tumechelewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaposimama hapa leo, nataka kusema hivi, huko tunakokwenda mambo yatabadilika. Sisi kama Taifa tufanye nini? Narudia yale yale ninayoyasema kila siku. Sisi kama Taifa tuelimishe watoto wetu, tuwekeze kwa kuelimisha watoto wetu. Katika hili, Mheshimiwa Waziri ni kweli wewe sio Wizara ya Elimu, lakini unashughulikia masuala ya TEHAMA. Naomba na ninasisitiza computer zisambazwe mashuleni, watoto wetu wafundishwe computer kuanzia primary schools ili matatizo yanayokuja huko mbele tuweze kukabiliana nayo. Tusipofanya jambo hilo, nataka niwahakikishie tutaachwa na hatutaweza kushindana na wenzetu kwenye ulimwengu unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aelewe kwamba suala la ubunifu na innovation ni jambo la muhimu sana. Wasaidie wabunifu wa Taifa hili. kuna vijana wengi sana wana ubunifu, nawe unawafahamu, lakini hawana mitaji, na wameshindwa kupiga hatua mbele. Benjamin Fernandes alianzisha mnara, kijana wa kitanzania, ameanzia hapa na matokeo yake amehamia nchi nyingine kwa sababu hapa nyumbani alikosa support.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kuna kijana anaitwa Magila Tech wote tunamfahamu, ame-invent mifumo mingi sana nyumbani. Ni kijana wa kitanzania, ana akili nyingi Mungu kamjalia, anafanya mambo mengi, lakini hapati support ya Serikali. Mabenki hayamtumii kutengeneza mifumo. Wanatoa kazi kwa mataifa ya nje, baadaye inaonekana kama mifumo waliyoiweka haifanyi kazi, wanamfuata Magila Tech huyo huyo aje atengeneze mfumo. Kwa hiyo, naomba tuwaelimishe sana watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, na la umuhimu na la kusikitisha ni kwamba, Rais wetu alikwenda Dubai akakutana na Mwenyekiti wa Makampuni ya Airtel akaahidi yule tajiri ya kwamba ataisaidia Tanzania kwenye mambo ya technology. Mheshimiwa Waziri kama hujui sasa unisikilize vizuri. Yule bwana ameamuru kampuni yake iliyoko hapa itoe data bure kwenye shule za msingi na sekondari katika nchi hii ambapo thamani yake ni Dola 830,000, lakini eti TRA wamekataa kutoa exemption ya VAT pamoja excise duty. Are we serious?

MBUNGE FULANI: We are not. (Makofi)

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashindwa kuelewa. Nakuomba Mheshimiwa Waziri kutana na Mheshimiwa Mkenda, kutana na Mheshimiwa Mwigulu mjadiliane suala hili. Baadaye mimi nitakamata shilingi yako kwenye hili. Hatuwezi kukubali tunapewa fedha zote hizi zisaidie walimu wetu tumewagawia vishikwambi huko vijijini, lakini hawana internet. Halafu mtu amekataa kutoa exemption ya VAT na excise duty.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili nitalisimamia na nitapambana na Waheshimiwa Wabunge naomba mniunge mkono nitakaposhika shilingi leo jioni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mengi ya kusema sana sina. Nakupongeza sana Waziri Nape na Makamu wako. Nakuamini sana na unajua. Nawe ni kijana mwenye akili, huwezi kushindwa kutatua matatizo yetu. Hakikisha kwamba Tanzania inakwenda mbele kiteknolojia. Jambo hilo linawezekana.

Mheshimiwa Spika, leo hii kwenye global innovation index, Tanzania ni ya 90 Duniani, Kenya ni ya 89, lakini Mauritius ni ya 35. Sisi tunashindwa nini? Akili tunazo, tutumieni akili zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)