Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Hon. Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuhitimisha hoja. Kwa unyenyekevu mkubwa niwashukuru sana Wabunge wote kabisa kwa maneno mazuri ya faraja mliyotupa hapa, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maneno yenu ni chachu ya sisi kuendelea kuwa wasikivu, wanyenyekevu lakini kuchapa kazi kwa bidii kuhakikisha yale matarajio nyinyi mliyonayo lakini na wananchi wenu yanatimizwa lakini pia tunatimiza lengo la Rais kuanzisha Wizara hii lakini na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ahsante sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishieni Waheshimiwa Wabunge, maneno mengi mliyoyasema hapa ni ya ushauri sisi hatuna haja ya kuyarudia hapa, niwahakikishieni tumechukua neno moja baada ya jingine mahali ambapo panakasoro tutakwenda kurekebisha, mahali ambapo pana mapungufu tutaongeza ili pakae sawa sawa, mahahi ambapo mmetupa mawazo mapya mimi na wenzangu tutayafanyia kazi na kuhakikisha tunafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vitatu nataka kuvizungumza kwa dakika tatu. La kwanza; suala la maslahi ya Waandishi wa Habari, jambo hili haliwezi kutatuliwa kwa kauli za kisiasa, jambo hili lazima litatuliwe kwa sheria na ndiyo maana tumeileta sheria ya huduma za habari hapa ili Wabunge tuipitie mle ndani tuweke misingi ya kulinda haki za waandishi wa habari wa nchi hii. Tuondakane na utaratibu wa waandishi wa habari kupewa haki zao kwa hisani, wapewe kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua katika sekta zilizo hathirika na myumbo wa uchumi kutokana na vita ya Urusi na Ukraine lakini na Covid sekta ya habari imeathirika sana na ndiyo maana hali ya vyombo vya habari si nzuri. Uchumi wao unayumba, leo hata tukiwatungia sheria ikawa kali namna gani utekelezaji wake utakuwa mgumu, kwa sababu hali ya uchumi wao ni mbaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia tumeunda timu nzuri inayoongozwa na ndugu Tido Mhando na tumewachukua watu nguli wa sekta kwenda kuangalia hali ya uchumi wa vyombo vya habari lakini wanaenda kupitia na mikataba ya waandishi wa habari ili watuletee pamoja na sheria tutunge kanuni baada ya hapo nataka niwahakikishieni sekta hii itarudi na kupata heshima na hadhi inayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawaombeni pitisheni bajeti yangu tukamalizane na jambo hili kwa kuweka mifumo na ndiyo kazi ya Waziri, Waziri siyo matamko, Waziri ni kuweka mifumo ya kutatua tatizo na ndiyo kazi naenda kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili; ni suala la wizi wa matapeli mitandaoni. Ndugu zangu sekta hii nimesema hapa tuna line za simu karibia milioni 63 zaidi ya idadi ya watanzania maana yake watu wako wengi kwenye huu mfumo na katika wingi huo kwenye msafara wa mamba kenge wako wengi pia. Katika kulishughulikia hili tumefanyaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni usajili wa line ulikuwa holela baadaye mtu akifanya uhalifu mkimkamata mnakuta ile line imesajiliwa na mtu mwingine ile kesi inafia palepale, ukienda Mahakamani akiiruka inaisha. Tulichofanya tumezisajili line zile kwa kutumia alama za vidole na penyewe pakawa na utapeli. Ndiyo maana juzi tukafanya uhakiki, baada ya uhakiki wa juzi tunaamini line zote zilizoko mtaani zina mwenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapa nataka nitangaze kiama cha matapeli kwenye mitandao na nitaliomba Bunge lako litusamehe kidogo kwenye hili, tutafumba macho kidogo hata kwenye zile haki za msingi. Kwa sababu yako mambo yanaudhi. Kwa hiyo, leo natangaza kiama cha jambo hili, tumejipanga vizuri tutawaomba wenzetu wa polisi na wengine tuondoe huruma kwenye jambo hili tulikomeshe, tulifute kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu; na mwisho kaka yangu Mheshimiwa Eric amezungumza jambo kubwa hapa. Nikuhakikishie kaka yangu wala huna haja ya kukamata shilingi yangu, jana nimekuta na Airtel wamenieleza jambo hili nilipoingia Dodoma nikakutana na Waziri Mheshimiwa Profesa Mkenda tumelizungumza, asubuhi nimeongea na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tunaenda hakuna sababu ya kubaki nalo, hili jambo limeisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie hili jambo limeisha tunazitaka hizi data kwenye shule zetu na juzi Rais ametuagiza kwamba tusambaze kwenye mashule yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nakushukuru kwa maneno yako mazuri na naomba nisitumie muda mrefu kama nilivyofanya asubuhi. Waheshimiwa Wabunge tuaminini, pitisheni bajeti yetu, ahsanteni sana, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.