Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi nami niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Mimi kama mjumbe wa Kamati ya Miundombinu kwa kweli tulipata nafasi nzuri ya kupitia hoja hii na naunga mkono hoja ili turidhie Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Mwaka 2009 kwa sababu faida ni nyingi kuliko hasara, na nchi yetu si kisiwa useme kwamba kuna baadhi ya vitu tunaweza kujitenga navyo, japokuwa watu wanaweza kuwa waogawaoga na mambo haya ya maridhiano. Mimi nataka kuchangia maeneo kama matatu au manne.
Mheshimiwa Naibu Spika, chini ya Shirika la Usafiri wa Anga ICAO na wa OAU kama Mheshimiwa Waziri na Mwenyekiti wa Kamati walivyowasilisha hapa, Tanzania tuliridhia ile ya mwaka 1969 na kwa mujibu wa Katiba hii mpya ya 2009 ni wazi kwa kile kipengele ambacho kinasema kwamba nchi 15 zikisha saini utekelezaji unaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Tanzania tumeshaanza kusukumwa nje kwa sababu nchi 41 tayari zimeshasaini maridhiano haya na wenzetu wanaanza kunufaika kuliko sisi. Hata huko nyuma tulishawahi kupata hadi fedha za uwekezaji kwenye mambo ya ushirikiano wa usafiri wa anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano mmoja, mimi na baadhi ya Wabunge wenzangu tulisafiri hapa na Timu ya Wananchi tukaenda katika nchi mojawapo. Tukiwa na ile Timu ya Wananchi pamoja na Waheshimiwa na wanashabiki wengine wa hiyo timu katika nchi hiyo, tulivyotua pale airport tulitumia kama masaa matatu hivi, bila ya kujali hawa ni Wabunge ama sio Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mlolongo ulikuwa mkubwa sana. Sasa hatukufahamu kitu, baadaye katika upelelezi nitaeleza umuhimu wa maridhiano haya, tukawa tunaangalia wale watu wanaotuhudumia pale kama kuna wengine ni wanachama labda wa timu nyingine pinzani na sisi hata katika nchi yetu ama katika nchi ile nyingine na kujiuliza kwa nini tunapata usumbufu wa namna hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukajua, mojawapo ya sababu ni kwamba nchi hiyo tuliokwenda sisi hatukuwepo kwenye maridhiano ya pamoja ya anga. Kama tungekwenda katika nchi nyingine ina maana tungenufaika, tungefika pale wangeambiwa kuna Watanzania 50 wanakuja katika nchi yetu. Tungepokelewa vizuri, tungepita na ule usumbufu ungeondoka pale na ile furaha yetu ya kumtandika mtu katika nchi ile na kushinda ile mechi ingekuwa vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hata wakati wa kurudi usumbufu ulikuwa vile vile. Kwa hiyo, naridhia na nawaomba Waheshimiwa Wabunge turidhie jambo hili kwa sababu faida ni nyingi kuliko hasara. Ukiona uwekezaji mkubwa ambao Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawekeza sasa hivi katika kununua ndege na juzi tu tumepata ndege ya kusafirisha mizigo, tukiongeza network ya mashirikiano itatusaidia sana kuhakikisha kwamba ndege yetu inapeleka mazao sehemu nyingi sana na inaongeza wigo ndani ya nchi na katika nchi zingine za Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja Mheshimiwa Bashe anaweza akaelekeza ndege ikatua pale Ifakara ikachukua mchele, ikapeleka katika Nchi za Afrika hizo zitakazokuwa zimesaini kama ni 55 ama ni vipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la ajira; kuna watu wamekuja kusaidia Shirika letu la Ndege la Tanzania kutokana na uzoefu wao katika mahusiano ya umoja wa mashirikiano ya anga katika nchi nyingine. Tutamkumbuka vizuri sana marehemu Mheshimiwa Omary Nondo, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema, alitolewa katika mashirika haya ya kimataifa ya mashirikiano haya yaliyopita na akaja kutoa uzoefu mkubwa sana katika nchi yetu. Pia, tuna mifano mingi ya Nchi nyingine kama vile Misri, wanajiunga na hii Katiba ya Afrika lakini wanajiunga na Umoja wa Nchi za Kiarabu. Yote hii ni kuongeza network ya biashara katika safari ya anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwa kifupi kwamba, pamoja na mambo yote aliyoyasema ya mafanikio kwa mfano ya kupata miongozo ya ndege ya kutosha. Sisi sasa hivi tunaongeza ndege nne, nafikiri kwenye Kamati yetu tumepewa. Kama tunaongeza ndege nne halafu tunajifungia wenyewe kwenye East Africa na Nchi kama Tanzania, bado hatuna soko kubwa la kujiwekeza vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naijua tahadhali ambayo imesemwa na baadhi ya watu kwamba lazima tuweke kanuni au utaratibu mzuri tusije tukafungua anga tu halafu ikawa kama tunafungua soko la watu wengine. Hata hivyo, katika soko kubwa hilo hilo na sisi tunaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuuza ndege zetu, kuuza Kiswahili chetu, kupambania vijana kupata ajira katika shirika hilo na katika nchi nyingine. Pia, sambamba na kupata fedha za uwekezaji ambazo zitatolewa na hiyo AFCAC ili nchi yetu iweze kufanya vizuri katika biashara ya usafiri wa anga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumalizia kwa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge turidhie Mkataba huu, turidhie Katiba hii ya 2009 ili iweze kutumika na nchi yetu iingie katika network ya Afrika nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha. (Makofi)