Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge Kuhusu Mapendekezo ya Kurejea Katiba ya Tume ya Usafiri wa Anga ya Afrika ya Mwaka 2009

MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kulishawishi Bunge liridhie na kuunga mkono Katiba ya Tume hii ya African Civil Aviation Commission.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania sio kisiwa, hatuwezi tukaishi kama kisiwa na tukajifanya na sisi tunao uwezo wa kuwa na mabavu tukiwa peke yetu. Lazima tuungane na Nchi Wanachama wa AU (Umoja wa Afrika) ambao wameridhia pamoja na Tanzania kwenye Katiba ya Tume hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, industry ya usafiri wa anga kwa sasa inakua sana. Vile vile, Tanzania tumeanza kuingia huko kwa nguvu kubwa sana. Tunapokwenda kwa nguvu ni lazima tujue na tuungane na wenzetu ambao wako kwenye industry hiyo ili twende tukapate uzoefu na manufaa makubwa ambayo yanatokana na usafiri wa anga.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini turidhie? Kwanza, tayari nchi nyingine zimekwisharidhia. Pili, hivi tunavyoongea Tanzania inalipa ada bila kuridhia. Tunalipa ada ambayo haitakuwa na manufaa, lakini tukiwa tunalipa ada tukapa manufaa itasaidia zaidi. Hivi tunavyoongea mpaka mwaka 2023 Tanzania imekwishalipa dola 45,230 karibu milioni 108. Hizi pesa hatuwezi tukakubali ziende bure. Kwa maana hiyo, naomba na nilishawishi Bunge twende huko turidhie Katiba hii ambayo itakuwa ni silaha kubwa ya sisi kujinufaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kupata ajira kwa vijana wetu, tunakwenda kupata ajira kwa watu wetu kuingia kwenye eneo hilo, lakini pia tutafaidika na Sheria nyingi na mabadiliko yanayotokea ya ICAO

Mheshimiwa Naibu Spika, tukikaa huko ndani, tuna fursa kubwa ya kueneza lugha yetu ya Kiswahili na tutaweza kutumia fursa zote zinazopatikana ili kuwafanya wenzetu waone umuhimu wa Kiswahili ambacho tunakitumia kama lugha bora kabisa na ambayo inashika nafasi kubwa Afrika na duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Watanzania tumelelewa vizuri sana na Baba wa Taifa. Vile vile, Baba wa Taifa alikuwepo kwenye kuanzisha Umoja wa Afrika (OAU) mwaka 1963. Tulipoanzisha Umoja wa Afrika (AU) ndipo mabadiliko yalipotokea. Pia huko nyuma tulikuwepo na tulikuwa tumeunga mkono Katiba ya Umoja huu. Baada ya mabadiliko mwaka 2009, ndipo tulipokuwa nyuma. sasa niliombe Bunge hili tuungane kwa pamoja turidhie na sisi tuangalie faida tunazozipata ambazo ni kubwa na ni nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)