Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu, lakini nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetupa uzima siku ya leo na hata siku zingine zilizopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kujenga Taifa letu na Serikali yake yote kwa ujumla, Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri, Makatibu, Naibu Katibu Mkuu na wote ambao wanamsaidia Mheshimiwa Rais kufikia malengo yake ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa letu mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia mjadala huu kwa eneo la upimaji wa ardhi. Upimaji wa ardhi katika Taifa letu haiko vizuri na haliko vizuri kwa sababu kwanza wananchi kupata ardhi katika nchi yetu imekuwa ni changamoto. Changamoto yake ni kwamba upimaji wa ardhi bei ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya wananchi wetu katika vijiji na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa hati Tanzania ni kama kupata lulu, sijajua huwa ni kwa nini Tanzania ukitaka kupata hati inakuwa kama vile sijui una nunua nini? Ile karatasi sijui inapatikana katika misingi gani! Kwa sababu ni kwa nini ardhi haikubaliwi kupimwa kwa urahisi Tanzania na mtu akapewa hati kwa uharaka. Wataalam wanasema sijui wanafanya michoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, michoro inachukua muda mrefu, ardhi haipimwi matokeo yake migogoro kwenye vijiji, migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya Wilaya na Wilaya, Mkoa na Mkoa hatimaye tunaonekana tunaendelea kukataa kupima ardhi kwa sababu ya kuweka bei kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Wizara imeweka mawakala wa kupima ardhi, yale makampuni yamekwenda kule kwa wananchi wamekusanya fedha hawajarudi kuwapimia wananchi ardhi ili waweze kuwapa ardhi. Wengine wameingia mitini, lakini hii inatokana hivi kwa nini, nadhani ni kwa sababu Wizara mna jambo la kufanya kuhusu eneo hili la upimaji wa ardhi hasa makampuni ambayo mmeyaweka na kuyafanya yakapime ardhi kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaamini kwamba Serikali imetumia makampuni hayo ili iweze kuwachukulia fedha zao. Kila mwananchi ametoa shilingi 150,000 lakini hawajapimiwa ardhi, yale makampuni hayaonekani, sasa hii ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba baadae Mheshimiwa Waziri atoe tamko kuhusu fedha zilizochukuliwa wananchi kwa makampuni haya ambayo yamepima ardhi. Kwa sababu tunakwenda kuwaletea wananchi wetu matatizo kwa kuweka makampuni ambayo sio waaminifu na sio waadilifu. Najua nia ya Serikali ni njema, najua nia ya Wizara ilikuwa ni njema, lakini sasa katika utekelezaji wa jambo hili limeenda kutuletea changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wageni kumiliki ardhi, wakati mwingine hili suala la wageni kumiliki ardhi tunaambiwa sana wageni hawamiliki ardhi, lakini mimi naona ni kinyume sana tukisema hivyo kwa maana hii Derivative Right of Occupancy ambayo anapewa mgeni ni kama amemiliki tu. Unawezaje kumpa mgeni amemiliki ardhi miaka 99 halafu yeye anasema ni mwekezaji, sawa anakuja pale ile ardhi inakuwa ni yake wala hawekezi chochote pale anatumia ile hati aliyopata kwenda kukopa benki. Akikopa benki ule mradi anauacha, anakimbia na fedha, anatelekeza ardhi matokeo yake ile ardhi inakuja inauzwa tena kwa kufidia zile fedha au yule mwekezaji amekaa na ile ardhi yote pale kwa miaka hiyo yote 99 anaamua kuuza ile ardhi kidogo kidogo anauza kidogo kidogo kwa maana anasema ana sublease hii sio sawa. Mimi naona kama hili suala la kusema wageni wamiliki ardhi haliko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lazima Wizara, Mheshimiwa Waziri mkae muone namna ya kurekebisha hii ya sheria ya wageni kumiliki ardhi kwa sababu kama mtu amekuja na mtaja labda milioni 500 viwekwe vipengele ambavyo mtu haruhusiwi kuuza ardhi, haruhusiwi kutumia ile hati kwa kukopa fedha, anatakiwa aje na mtaji wake kama ile Sheria ya Tanzania Investment Centre inavyosema. Kama hatufanyi hivyo bado tunajidanganya kwamba wageni hawamiliki ardhi. Kama unammilikisha miaka 99 wakati hakuna binadamu ambaye hata kwenye vitabu vya Mungu ni miaka 70, miaka 80 ni ya tabu na huzuni, hiyo miaka 99 nani anajua kwamba atafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hapa bado kuna changamoto inatakiwa muangalie kwa sababu bado hatuwatendei wananchi haki katika maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Mabaraza ya Ardhi; Mabaraza ya Ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi (Land Act No. 113) ya mwaka 1999 na Sheria ya Land Disputes Courts Acts iliyoanzisha mabaraza hayo mwaka 2002 na ikaanza kufanya kazi mwaka 2003, ni miaka 20 sasa imepita nadhani tuna mabaraza 92 Tanzania nzima. Hii sioni kama ni haki kwa sababu ukiangalia hata kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza katika Ibara ya 107(a) kwamba lazima Serikali iweke mazingira ya kutochelewesha haki bila sababu zozote. Sasa katika mabaraza hayo hayana mfumo mzuri wa utoaji haki. Kama baraza linaweza kupiga kesi miezi sita, mwaka mmoja, miaka miwili, mitatu, mitano bila kutoa haki hii sio sawa kwamba wananchi hawa wanapata haki kupitia mabaraza haya. Martin Luther King aliwahi kusema; “A right delayed is a right denied” haki iliyochelewa ni sawa na haki iliyonyimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira hayo ya mabaraza haya hatuwezi kuona kwamba haki inatendeka katika mabaraza ambayo hayana mfumo mzuri wa kimahakama, na kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana kwamba mamlaka iliyopewa kutoa haki ni mahakama kwa nini mabaraza haya sasa isifike mahali tuachane na mfumo uliopo ambao udhibiti wake wa namna ya kutoa haki haupo sawa, tukaingiza kwenye mfumo wa mahakama ambayo itakuwa kwenye udhibiti. Mahakama imekaa vizuri sana katika utoaji wa haki kwa sasa. Kwa nini tunaendelea kung’ang’ania mabaraza hayo chini ya Wizara? Hatuoni tunawanyima wananchi haki? Ukizingatia kwamba tumeshindwa kufikia mabaraza yote katika Wilaya nzima. Unakuta katika Mkoa mmoja wenye Wilaya saba mpaka tisa kuna mabaraza mawili tu tena yapo pale Mkoani, hii haki iko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa hatutendi haki kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Rais amefika mahali anawataka wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wapate haki mpaka ameenda mbali zaidi ameunda Tume ya Haki Jinai; unafikiri anafikiria nini? Watu walioko magerezani na popote pale wakiteseka waweze kupata haki zao. Je, ni kwa nini sisi kama Wizara au ninyi kama Wizara msione sasa kwamba kuna haja ya ku-handover hayo mabaraza kwenye mfumo wa mahakama? Kuna tatizo gani na shida gani? Kwa sababu ukiangalia kwa maana ya research miaka 20 kama hamjaweza ku-meet vile vigezo vya kila Wilaya kuwa na mabaraza ina maana tume-fail.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe baadae Mheshimiwa Waziri hili suala mlitolee tamko na sio suala gumu. Tuna mfumo mzuri wa mahakama yetu kuanzia Baraza la Kata, Mahakama ya Mwanzo mpaka juu hata hayo mabaraza yakiendelea kuwepo, lakini yaingie kwenye mkondo wa kimahakama hii itasaidia wananchi waweze kupata haki na kuepuka kufata haki kule mbali ambako sio sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaamini Mheshimiwa Rais aliyewaweka pale, Mheshimiwa Waziri, Rais anakutegemea umsaidie katika kuleta mabadiliko katika Wizara hii ya Ardhi. Mabadiliko yenyewe ni haya ambayo inatakiwa wananchi waone haki inatendeka kwa sababu sio tu haki itendeke, lakini haki ionekane ikitendeka.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, wananchi wanakutegemea, wanakuangalia unavyoweza kuwatoa katika dhiki hii ya mabaraza haya. Tume ya Kurekebisha Sheria inatakiwa iyaone haya kwa sababu ni kazi yao kuleta sheria ambazo hazina tija na zimepitwa na wakati. Sheria ya Ardhi irekebishwe, Sheria hii ya Mabaraza irekebishwe na sheria zingine ambazo ni kandamizi na hazileti tija na mwelekeo mzuri kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)