Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nami kwa kunipatia wasaa ili niweze kutoa mchango wangu kwa Azimio hili. Nitambue pongezi zilizotolewa na Wabunge wenzangu pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati yetu. Kwa hiyo, nami niunge mkono tu pongezi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio hili lina mawanda mapana na linatuonesha dira kama Taifa na manufaa mapana na makubwa ndani ya Taifa letu. Pamoja na hayo manufaa makubwa yanayoonekana kwenye hili Azimio, kuna mambo kadhaa ambayo kama nchi, kama Serikali lazima wayaangalie kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaomba kuyasema machache. La kwanza ni suala zima la biashara zetu za ndani kwanza. Leo biashara ndani ya nchi, bado kuna purukushani nyingi sana kuhusiana na suala zima la sheria, kodi na mambo kadha wa kadha. Sasa tunapokwenda kujiunga kwenye jumuiya hii ni lazima tuone: Je, hivi sisi kama nchi, changamoto zetu ndani ya nchi kwa wafanyabiashara wetu tumezitatua kwa namna gani? ili tunapotoka huko kwenda kushindana na wenzetu ili tuweze kuona sasa huku ndani tumemaliza, sasa tunakwenda nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wenzangu wamesema suala la leseni. Leo ndani ya Taifa letu tuna leseni; nikiwa nauza mandazi, natakiwa niwe na leseni, nina guest house, niwe na leseni, nina magari kama Waheshimiwa Wabunge walivyosema, lazima niwe na leseni ya magari, sijui nauza duka, lazima niwe na leseni ya duka. Hivi vitu wakati mwingine hebu kama Taifa tujitathmini. Kuna faida gani ya mfanyabiashara mmoja kuwa na leseni saba? Kuna faida gani ya mfanyabiashara Kunti kuwa na leseni saba za biashara? Hivi ni kwa nini kama nchi tusione kuna sababu sasa ya kutoka huko? Kama ni issue ya mapato ya Halmashauri, Serikali itengeneze mfumo kwamba mfanyabiashara awe na leseni moja, na Halmashauri itapata mapato yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali, tutakapoingia kwenye hili Azimio, tunapojiunga ni lazima tutoke sasa kwenye ule mfumo wa kuwa na leseni saba, tutengeneze mfumo wa kuwa na leseni moja ili pia hata hao wenzetu wanaokuja wakute tumeshajipanga kama nchi, tuko serious na tunajua nini tunachokifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Azimio watakaokwenda kuwajibika ni wafanyabiashara ama ni sekta binafsi na siyo Serikali. Kwa hiyo, ni lazima tutengeneze mazingira rafiki ya kuwa karibu na sekta binafsi na kuwatengenezea mazingira rafiki yatakayoweza kufanya kazi ama kufanya biashara zao bila usumbufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu hapa kuna Wizara mbalimbali ambazo kila Waziri anasimamia sera yake kwenye Wizara yake. Nafahamu Mheshimiwa Waziri ni mratibu kwenye suala la biashara. Sasa kama nchi, ni lazima Serikali muanze iwe na lugha moja. Bila ya kuwa na lugha moja, leo Waziri wa Nishati anasimama na ya kwake, Waziri wa Kilimo anasimama na ya kwake, Waziri wa Fedha akija hapa ana ya kwake, Waziri wa Habari ana ya kwake, Waziri wa Biashara nawe unakuja na story zako, hatutaeleweka kama Taifa na itifaki hii haitaleta tija kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ifike wakati pia kama Serikali, kama nchi, ni lazima muanze kuongea lugha moja. Atakachokisema Waziri wa Viwanda akiseme Waziri wa Fedha; atakachokisema Waziri wa Fedha vivyo hivyo Waziri wa Nishati, Serikali tuweze kuwa na lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye itifaki hii pia ni lazima tuandae rasilimali watu wenye ujuzi kwenda kushindana na hawa wenzetu. Tusipoandaa rasilimali watu yenye ujuzi, suala la uwepo wa ongezeko la ajira kwenye nchi yetu itakuwa ni ndoto za Abunuasi. Ajira zitachukuliwa na mataifa ya wenzetu na sisi tutabaki kuendelea kulalamika. Kwa nini? Ni kwa sababu kama Taifa hatukuchukua hatua kuwaandaa watu wetu. Kwa hiyo, ni lazima tuandae rasilimali watu ambao wana ujuzi ili tuende tukashindane na hizo fursa za ajira ikiwezekana tuzibebe nyingi zaidi kwenye Taifa letu tuweze kupunguza hilo wimbi la ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ubora wa huduma. Lazima huduma zetu ziwe na ubora, zikidhi viwango vya mataifa hayo mengine. Tusipokidhi ubora wa huduma zetu pia itakuwa ni changamoto, tutabakia kupokea huduma za watu kutoka kwenye hayo mataifa na sisi tutakuwa na shimo la taka la kujaza matakataka humu ndani ya nchi. Kwa hiyo, lazima tujipange kuwa na huduma ya ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano mdogo sana ambao ulinipata jana. Jana kulikuwa na shida ya umeme, ulikatika na baadaye umeme uliporudi, kukawa na maeneo umeme upo na maeneo mengine umeme haupo. Mimi nina namba mbili za emergency za TANESCO, nikapiga namba ya kwanza; cha kwanza cha kusikitisha, yaani ile namba ya simu ukipiga, kabla hujahudumiwa, tayari hela imeshaanza kutumika. Kabla hujahudumiwa, wameshachukua hela, halafu hiyo ni namba ya huduma ya mteja anayetakiwa kupewa huduma, unamkata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimepiga namba ya kwanza haikupokelewa, namba ya pili haikupokelewa, nikarudia. Namba ya kwanza ikapokelewa. Ilivyopokelewa nikapewa namba ya usajili wa tatizo nililoripoti, nikaambiwa baada ya nusu saa nitapata huduma. Sikupata hiyo huduma. Nikapiga ile namba ya pili, ikapokelewa, nikapewa namba nyingine tena ya huduma. Yaani taasisi hiyo hiyo moja, kwenye mfumo pale hawezi hata kuona kwamba mita namba hii imeshapewa namba ya huduma hii, tatizo lake linashughulikiwa. Nikapewa tena namba nyingine ya huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaona ni namna gani ambavyo kama nchi, hata mifumo yake tu yenyewe bado haijawa bora. Haiwezekani kitengo cha huduma kwa wateja, emergency call unapiga namba mbili unapewa majibu tofauti na watu tofauti na wako kwenye system. Nilifanya makusudi tu kupiga, niliamini angenijibu akaniambia tatizo lako limeshapokelewa, linafanyiwa kazi, lakini cha ajabu nikapewa namba nyingine tena nikaambiwa subiri nusu saa. Kwa hiyo, tuone changamoto zilizopo kwenye huduma zetu tunazozitoa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tuna Bwawa la Mwalimu Nyerere lile pale ambapo tutakwenda kuzalisha umeme ambao utahudumia Watanzania, tunatarajia tuwauzie na wengine. Kama changamoto hata za kwenye mfumo ziko hivi, nani atachukua huo umeme wetu? Hayupo. Kwa sababu watachoka, mtakuwa hamwasikilizi, mnawapa maneno, badala ya kuwapa huduma inayostahili. Kwa hiyo, lizingatiwe pia suala zima la ubora wa huduma zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni matangazo. Tunaweza tukawa na hizo fursa nyingi lakini tusipozifanyia matangazo ya uhakika, yenye tija, pia hali kadhalika hakuna atakayeweza kujua sisi kama Taifa la Tanzania tuna vitu gani ambavyo vinaweza vikaingia kwenye soko hilo la ushindani huko kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la amani ndani ya nchi yetu. Yote haya tunayoyafanya ni lazima kama Taifa tuwe na amani ambayo itaweza kutusaidia…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kunti, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista.

TAARIFA

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wake na amezungumza hapa jambo la msingi sana. Changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye sekta mbalimbali katika kutoa kuhuduma, biashara hizi za huduma na ametoa mifano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimpe taarifa kwamba kwa kuzingatia maelekezo ya Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali yetu kwa kuzingatia usikivu wa Serikali yetu. Bunge lilitushauri kuanzisha sasa kitengo ama idara maalum ya monitoring and evaluation ili kadhia zote zinazojitokeza, ikiwemo kama hii, changamoto za kimfumo katika utoaji wa huduma fungamanishi Serikali iwe na majibu ya jumla na hasa kupitia kwenye mamlaka zetu na hasa mamlaka ya Serikali mtandao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana naye na naomba tu nimpe taarifa kwamba jambo hili tumeshaanza kulifanyia kazi, idara imeshaanzishwa, uratibu unafanyika na huko tunakoingia kwenye protocol ya SADC haya ni mambo ambayo tulishayaona na tumeshajipanga ili iwe ni sehemu ya utatuzi wa changamoto tunazozipata. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kunti unaipokea taarifa hiyo, uendelee na mchango wako?

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nahisi Mheshimiwa Waziri hajanielewa.

Pili, kazi yangu mimi Mbunge na wajibu wangu ni kusema yale tunayoyaona na tunayokutana nayo na tunayoambiwa na wananchi, na kazi yao kama Serikali ni kusikiliza yale tunayoyasema yanayotoka kwa wananchi. Sasa suala la tatu, mkiamua kuyafanyia kazi ni juu yenu, mkiamua kuyapuuza ni hiari yenu. Kwa hiyo, mimi kama Kunti, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimetimiza wajibu na jukumu langu ndani ya Taifa langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee. Amani ndani ya Taifa letu. Hii amani tuliyonayo ni muhimu sana katika Taifa letu, na amani inakuwepo tu kama watu watatendewa haki ndani ya Taifa. Haki hiyo ya kwanza ni ya kusikilizwa ambayo ndiyo hii mnayoifanya; Serikali tusikilizeni. Nikisema hapa, mimi sisemi ya familia yangu, ninasema ya Watanzania huko nje kwa sababu wamekosa fursa ya kuja kuingia ndani humu na kuyasema haya. Kwa hiyo, haki ya kwanza, Watanzania tunahitaji kusikilizwa yale tunayoyasema ili ninyi muweze kuyachakata na kuona ni namna gani mnakwenda kuyafanyia kazi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoamua kuwa wasikivu, tukawa na yale maneno ya kusema Serikali sikivu ya mdomoni kwenye moyo haipo, hatutalisaidia Taifa. Kwa sababu hata wawekezaji tunaowategemea, wakiona Serikali yetu inasema bila kutekeleza kwa vitendo, bado watakuwa na hofu na sintofahamu kwamba nikienda pale nitaenda kufanya nini? Kwa sababu Taifa lao lenyewe halina uhakika, watu wao wana vinyongo ndani ya nafsi. Kwa hiyo, naomba amani na suala zima la kusikilizwa lilindwe na lifanywe kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nakushukuru kwa muda, ahsante sana. (Makofi)