Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia suala lililopo mbele yetu, Azimio la Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Bara la Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo niongee mambo mawili makubwa ambayo huwa tunayapata baada ya kupitisha maazimio katika Bunge lako Tukufu. Awali ya yote, nipongeze mtazamo wa Wizara kwa ujumla kwa sababu dunia inapokwenda sasa hivi, sisi hatuwezi kukaa kama kisiwa. Dunia imeshakuwa globalized, mambo yanafanyika kwa pamoja. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwamba inawezekana hata kuridhia Azimio hili tumechelewa. Kwa kuwa sasa tumeamua kuridhia, nitakuwa na ushauri wangu katika mambo mawili kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni timing au kwenda na muda. Jambo la pili ni mindset, jinsi ya kuandaa akili za Watanzania ili kwenda sawa na mipango ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na timing, kila kitu lazima kiwe na muda maalum na ili ufikie malengo unayopanga, lazima ujipangie muda. Kamati imeeleza vizuri sana na imetoa ushauri mzuri sana kwamba tunakwenda kuridhia itifaki hii, cha msingi, ni lazima Serikali iangalie sera zetu, kanuni zetu na sheria zetu ziendane na wakati. Maana tunaweza tukaridhia hili, bado sheria zetu zikachelewa kurekebishwa, na kanuni zetu zikachelewa, bado na sera zetu zikawa ni zile zile, haitakuwa na maana ya sisi kuridhia haya. Kwa hiyo, tunaomba haya mambo tunapoyapitisha, yaendane na kasi na muda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Iringa kuna usemi tunasema hivi: “Ng’ombe anayewahi kufika mtoni, ndiye anayekunywa maji masafi.” Kwenye biashara kuna watu wanaoitwa innovators. Wale watu ambao ni innovators mara nyingi hawafilisiki na ndio ambao huwa wanaendelea, wanarithisha utajiri kizazi na kizazi. Wale ambao wanajifunza kwa kuangalia matokeo, mara nyingi ndio wale ambao wanafilisika kila wakati. Mtu ambaye anabuni kitu akakianzisha mwenyewe, mwingine anasubiri mwenzie abuni, aangalie kama atanufaika, yule ndiye ambaye sasa anakuja kufilisikafilisika na biashara zake haziendi vizuri; lakini mtu yeyote anayeangalia mapema akawahi ile fursa mapema, ndiye anayeweza kufaidi na kunufaika na hiyo fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaridhia Azimio hili kwa nia ya kwamba sasa tunaenda kuboresha utalii wetu, tunaenda kutanua mipaka yetu ya kunufaika kibiashara kwenye nchi ambazo zinaridhia Azimio hili, lakini wenzetu watanufaika, watafaidi kwenye nchi yetu, na sisi watu wetu wakawa bado wana-lag behind au bado hatujawaandaa katika ile attitude, ndiyo unakuja sasa kwenye aspect namba mbili ya mindset. Ni namna gani tunawaandaa watanzania kwenye haya maazimio mazuri ambayo Bunge linayapitisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, akili za Watanzania huwa zinashibishwa vipi maarifa, wakaelewa nia dhabiti ya Serikali inayokuwemo ndani ya haya maazimio? Kama tunapitisha hapa maazimio na Watanzania akili zao hazijaelewa vizuri, bado wanaona tunapoteza muda, lakini huwa yanageuka yanakuwa fimbo. Tunapitisha kwa nia njema kwa kuangalia ustawi wa Watanzania, kwa kuangalia kukua kwa uchumi kwa Watanzania, kwa kuangalia tunavyoongeza fursa za ajira, kwa kuangalia tunavyobadilisha maendeleo ya Watanzania, lakini kwa kuwa mindset zao ambazo zinakuja kuleta attitudes zao hazikusetiwa vizuri, yanatugeuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepitisha maazimio, lakini watu hawajui. Mheshimiwa Waziri lazima tukubali kwamba katika bajeti zetu tunatumia gharama kuwaelimisha watu. Mwalimu alishasema, kama wewe unaona kwamba elimu ni gharama, basi jaribu upumbavu au jaribu ujinga. Kama tunafikiri kwamba tutapitisha maazimio halafu Watanzania hawayaelewi yakaenda yalivyo, hebu tujaribu sasa kuyapitisha maazimio, watu hawayaelewi, halafu uone yakifika kwenye jamii jinsi yanavyoturudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatakiwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye kuhakikisha kwamba watanzania wanaelewa nini hasa nia nzuri na dhabiti ya Serikali kwa kuwapa elimu waelewe. Usipom-set mtu vizuri kwenye akili aka-download uongo akauweka kwenye moyo wake, kuja kuutoa huo uongo aliouweka moyoni ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, kwenye maazimio kama haya yasiishie tu hapa, lazima kuwe na program maalum ya kuhakikisha Watanzania wanaelimishwa, wanawekwa sawasawa, waelewe nia thabiti ya Serikali yao, kwamba nia ya Azimio hili ni kutanua mipaka yetu hata ya ajira. Hatuwezi tukakaa humu ndani ya Tanzania…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: … na Watanzania milioni 61 tukafikiri kwamba tunaweza kuajiri wote humu tukapata fursa, wakati kuna fursa ya ajira sehemu ya watu milioni 360…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge.

TAARIFA

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Msambatavangu kuwa katika hilo analolisema, ni jambo jema sana na Umoja wa Mataifa tayari imeshaweka Azimio la kwamba sharing misinformation can seriously harm those around you. Nafikiri ni wakati sahihi sasa ili watu waweze kuelewa maazimio yanayotolewa na Serikali kwa usahihi, tuunge mkono jitihada za Umoja wa Mataifa katika kampeni hii ya watu kuto-share taarifa zisizokuwa sahihi bila kuwa na uhakika wa taarifa hizo, ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca, taarifa unaipokea?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili, taarifa ya Engineer iliyoenda shule.

Mheshimwia Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba taarifa ni nguvu. Azimio hili limeongelea, na sifa kubwa ya nchi yetu ni kuwa na amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie amani na utulivu huwa inaanza kwanza kwenye choko choko za kupotosha taarifa. Tutachokonoa Mhimili wetu wa amani na kukorofishana humu ndani na tukapigana na tukaonekana hatuko sawa sawa baadaye tunakuja kuambizana kumbe kuna muongo mmoja alianzisha tu taarifa akaipeleka yeye isivyo wakati wenye taarifa sahihi hawakuzifikisha wakati sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe maazimio haya yamilikiwe na Serikali kama mnavyotumilikisha Wabunge na Watanzania wayamiliki haya ni mambo ya nchi yetu, wawe wanaelewa tuna desturi moja. Isiwe rahisi mtu anakuja tu kutuambia tumeuzwa, watu wengine pressure zinapanda mmeuzwa, mmeuzwa, mmeuzwa watu wanafikili. Mtu mwingine anaweza akatoka hapa na hili hili azimio akaenda kusema mmekodishwa, mmekodishwa SADC watu wakaona tumekodishwa au tumepangishwa. Kumbe nia siyo hiyo nia ni thabiti watu wapewe elimu tutumie fedha kutoa elimu kwa Watanzania wawe wanaelewa mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utali ni package, Watanzania waelewe utalini package, mtalii anataka kutoka Afrika Kusini mpaka Cairo atumie ile nini wanasema Cape to Cairo apite nchi zote ndani ya Afrika akafike Cairo atoke Kusini mpaka kule. Sasa sisi tukikaa tumejifungua hapa hatujaridhia azimio hili tumetanua utalii wetu kupitia royal tour watu watatoka Marekani watakuja Tanzania watataka kwenda Congo tayari kuna vifigisu figisu sisi hatujafungua mipaka na kushirikiana na wenzetu wa Congo utalii hautokua? mindset za Watanzania hapo wengine tayari ukishaambiwa tu nchi nyingine kama Congo unajua ni vita tu, ukumbuki kumbe na akina Awilo Longomba nao watatoka huko huko kama kuna vita tu hakuna mambo mengine ya starehe kwanini wanaweza kupata muda wakajifunza na muziki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii ni ku-unset mind zao wajue kwamba kuna fursa kwenye nchi zingine; lazima Watanzania wapate maarifa haya. Ndugu zangu tusipo wekeza kwenye mind set na altitude tunapitwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda nchi kama Nigeria wanakwambia moja ya sehemu ambapo wameajiri watu wengi ni kwenye utume ni missionary namna ambavyo wameshirikiana na Taasisi za kidini halafu wamezifundisha zile Taasisi za kidini wamezi-empower kwa kutengeneza kanuni na sera nzuri wamewaruhusu dini waende nje ya mipaka ya nchi yao. Kwa hiyo, wameweza kufungua huko mamisikiti, wameweza kufungua huko makanisa kwa watu wengine wamekwenda kuajiriwa hata nje ya Nigeria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajipanga vipi kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wenzetu, siyo tu sisi Watanzania, Taasisi za dini kuona kwamba tunawaita Viongozi wa dini tukawaambia kuna fursa hizi tunaomba mnaposimama mkitoa maelekezo yenu, mkitoa na nyaraka nyingine toeni na fursa hizi hapa ili Watanzania wajue kuna fursa sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hayo hatutayafanya tutabaki kulaumiana na tutaonekana sisi tunaandika vizuri sana, tunamipango mingi sana, tunamaazimio mengi tunapitisha lakini hayana tija kwa Watanzania…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jesca ahsante sana, malizia sentesi ya mwisho.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, narudia tena lazima tuhakikishe tunawekeza kwenye fahamu. Watu wetu wajue na wewe ndiyo Waziri wa Viwanda na Biashara, watu wetu wajue ni kitu gani hasa kiko ndani ya hili azimio?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)